UCHAMBUZI: Kim Poulsen kurudi Bongo ni ukweli tulioukimbia

ACHA kwanza niweke ubani wa Utanzania wiki hii kutakuwa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambapo wawakilishi pekee wa nchi, Simba watakuwa jijini Kinshasa wakikutana na AS Vita ya huko ukiwa ndio mchezo wao wa kwanza katika hatua hiyo.

Dua ya uzalendo ni moja kuwaombea wawakilishi hawa wawe na Ijumaa njema katika mchezo huo ili kujiweka katika hatua nzuri katika kundi lao. Simba inatakiwa kusahau kipigo ambacho walikutana nacho miaka miwili iliyopita kutoka kwa AS Vita katika mchezo wa hatua kama hiyo, lakini kusahahu huko wanatakiwa kuonyesha ukomavu mbele ya vigogo hao.

Hakuna shaka kwamba mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa kila timu ina uborta wake na binafsi naamini mechi itakuwa kwa kocha Didier Gomes na jinsi atakavyochanga karata kikosi chake.

Huu ni mchezo wa ufundi zaidi na akili ya haraka unatakiwa ufanye kipi ndani ya dakika 90. Litakaposhindikana hili kuna uwezekano mkubwa Simba ikaanguka lakini kama Gomes atakuwa sawa sidhani kama kutakuwa na shida. Salam zangu ni kuwatakia kila la heri wawakilishi hawa. Tuachane na Simba turejee katika hoja ya msingi ya hivi karibuni kumeenea taarifa njema kwamba kuna uwezekano wa kurejea kwa mkufunzi Kim Poulsen, raia wa Denmark hapa nchini kuendeleza majukumu ya kutuvumbulia vipaji.

Uongozi wa Rais Walace Karia umeona kuna sababu za Kim kurejea kuendelea na kazi yake ingawa haijajulikana anarudi kwa jukumu lipi katika timu ya taifa au eneo lingine tofauti, hiyo itajulikana baadaye atakapofika nchini.

Binafsi sishtushwi na kurejea kwa Kim kwani hatua ya mkufunzi huyu kurejea ni hitimisho la ukweli kwamba tulifikiria kurudi nyuma badala ya kwenda huko hatua ambayo hapa kwetu ni jambo la kawaida ambalo wanaopewa mamlaka makubwa hasa katika soka huamua kufikiria hivyo. Sishangai na wala siwashangai kabisa.

Haukuwa uamuzi sahihi wakati ule wa utawala wa aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kumtimua Kim kwani nafikiri TFF au hata taifa ndio tulikuwa na matatizo kuliko hata upungufu ambao waliuona na kuamua kutoendelea na mkufunzi huyu. Wakati ule mpaka sasa pengo la Kim limeonekana wazi na hata wakubwa walipoamua kujaribu kulificha tulifanikiwa kwa muda tu kwani baadaye lilionekana na kujitokeza hadharani kwamba bado tulikuwa tunamhitaji Kim kuliko yeye anavyotuhitaji sisi.

Nakumbuka wakati anataka kuondoka Kim niliwahi kuongea naye akaniambia maneno ambayo kadri muda ulivyosogea yalizunguka katika soka letu, akisema kuondoka kwake ni kiashiria tumeamua kupunguza kasi ya kutafuta mafanikio akiangalia mipango iliwekwa kabla kisha yaliyofanyika na mzigo wa kazi iliyobaki.

Sasa anarejea naamini TFF itatulia na kwanza kujua wapi tumeanguka na kipi tunatakiwa kukifanya ili turudi katika kasi ya kutafuta mafanikio, namwamini Kim katika kuzalisha vijana wazuri washindani katika soka ndio huyu aliyetuboreshea kina Frank Domayo, Saimon Msuva na wengine wengi kazi ambayo hapa kati ilipotea kabisa na kurudi zama za kuokoteza na kuwatupa.

Tunahitaji mtu ambaye atatungenezea njia ya kuwalea vijana kwa ngazi mbalimbali kisha takwimu zao zikatunzwa, kuendelezwa na kufuatiliwa kila hatua ya ukuaji wao na sio kuzalisha na kuwatupa.

Niwapongeze TFF ya Karia imefanya kazi kubwa ya kulea timu za vijana ambazo baadhi ya hizo sasa zipo katika mashindano makubwa ya Afrika, na Kim atatusaidia kuzipa ubora akishirikiana na makocha wazawa ili kama nchi tupate mafanikio.

Ukiacha hilo naamini pia Kim ambaye alikuwa akifanya kazi na Fifa katika kutoa elimu kwa makocha, sasa tutatumia kurejea kwake hata makocha wetu kuchota ujuzi wake ili ubaki katika vichwa vyao na baadaye kama taifa tunufaike.

Karibu sana Kim Poulsen tutasifishe uchafu ambao utaukuta ndani ya nyumba yetu.