JICHO LA MWEWE: Jinsi Simba ilivyorahisisha maisha Kinshasa

WAKATI Chris Mugalu aliposimama mbele ya mpira na kisha kupiga penalti iliyompita kipa wa Vita katika dakika ya 61 ya pambano la Ijumaa usiku pale Kinshasa, Simba ilikuwa imerahisisha maisha yake katika michuano ya Ligi ya mabingwa hatua ya makundi msimu huu.

Dakika 26 zilizofuata Mwamuzi alimaliza pambano na kwa mara ya kwanza katika historia Simba ilikuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kupata ushindi wa ugenini katika hatua ya makundi ya michuano hii. Miezi 24 iliyopita ilishindwa kufanya kitu kama hiki katika hatua kama hii.

Walishindwa kupata walau bao la ugenini katika mechi tatu dhidi ya Saoura, Al Ahly na AS Vita. Lakini hapo hapo ikashindwa kupata ushindi wowote huku Aishi Manula akiruhusu mabao 13 katika mechi tatu za ugenini. Ijumaa maisha yalibadilika Kinshasa.

Ni kweli maisha yamebadilika sana. Awali nilikuwa nawashutumu mashabiki wa Simba kwa kukariri matokeo ya kundi lao lililopita. Kwamba Simba watashinda mechi zote nyumbani na labda wajaribu kusaka pointi moja ya ugenini hili waweze kupita kundi lao. Ukitazama kundi lilivyo Simba wanaweza kupoteza hata pambano moja pale Temeke na bado wakapita katika kundi lao.

Simba inaweza kufungwa na Al Ahly pambano lijalo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na bado wakawa na nafasi kama itashinda dhidi ya As Vita na Al Marreikh huku pia ikisaka pointi ya kupumua pale Sudan. Hauwezi kubisha kwamba hawawezi kufanya lolote Khartoum kwani wamefanya nini Kinshasa?

Kwa ushindi wa Ijumaa, Simba wamejipa nafasi ya kupumua katika kundi. Katika hesabu za kawaida Simba watasaidiwa na mambo mawili. Kwanza ni ugumu wao katika uwanja wa taifa lakini pili ni kwa mbabe wa kundi Al Ahly kushinda mechi zake zote dhidi ya AS vita na Al Marreikh. Ni kitu ambacho kinawezekana.

Nimeitazama Vita ya Ijumaa nadhani inaweza kufungwa na Al Ahly katika mechi zake mbili za Kinshasa na Cairo. Vita hawa ni bora walipokuwa na akina Tuisila Kisinda, Tanombe Mukoko, Fabrics Ngoma, Jean Makusu na wengineo ambao walikuwepo katika lile kundi la zamani la Simba.

Nilidhani kwamba wametengeneza vita kali zaidi lakini kumbe wameporomoka zaidi. Haishangazi kuona mchezaji anayedenguliwa na Yanga anakwenda kuanza katika kikosi chao cha kwanza. Siamini kama wana timu ya kuizuia Al Ahly nyumbani na ugenini. Bado siamini hasa ukizingatia kwamba mechi zao zitakuwa zinamuhakikishia Al Ahly kusonga mbele.

Sijawaona vizuri Al Marreikh na ingawa timu za Sudan huwa zina ugomvi mkubwa dhidi ya timu za Misri ambao ni Waarabu wenzao lakini nadhani Al Ahly ambaye ni bingwa wa Afrika anaweza kushinda mechi zote mbili bila ya shida. Kocha wao ameondoka ghafla kwenda Simba na ingawa wamenunua mastaa wapya lakini bado hawajakaa sawa.

Kama Simba atashinda dhidi ya Vita na Al Marreikh pale Temeke basi uwezekano wa kupata pointi 10 ni mkubwa hasa kama atapata sare Khartoum au atapata sare Dar es salaam dhidi ya Al Ahly. Kwanini naamini Ahly ataidhibiti Simba? Ukweli ni kwamba hawa ni mabingwa wa Afrika ambao wamepiga hatua kubwa kuanzia pale tulipowaona mara ya mwisho.

Al Ahly wamemchukua mchawi wa soka la Afrika kwa sasa Pitso Mosimane lakini pia wanaonekana kuimarisha kikosi chao zaidi tangu walipofungwa na Simba katika uwanja wa Taifa pale Temeke. Mechi zao mbili dhidi ya Simba ndizo mechi ninazozihofia zaidi kwa Simba na hapana shaka hawatakuja Dar es salaam kijilinda kama walivyofanya mara ya mwisho.

Ukitazama jinsi walivyocheza pambano la nusu fainali klabu bingwa ya dunia dhidi ya Bayern Munich wiki iliyopita unapata picha kwamba kwa sasa ni klabu bora zaidi Afrika. Haishangazi unapoisifu Simba kwamba wamefanya kazi nzuri Kinshasa kwa sababu lolote likitokea uwanja wa taifa dhidi ya Al Ahly bado wanakuwa wamefidia pointi zao kwa Vita ugenini.

Hata hivyo hizi ni hesabu za karatasi tu. Simba bado wana kazi ngumu ya kufanya katika kundi lao. Kuna timu huwa zinaanza vibaya katika michuano lakini zinaimarika kadri michuano inavyosonga mbele na kuna uwezekano zikasababisha nikala maneno yangu.

Mfano mzuri nadhani Simba wenyewe watakuwa wameushuhudia kwa Saoura katika kundi lao miezi 24 iliyopita. Saoura walianza vibaya kwa kuchapwa mabao 3-0 na Simba katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Sio tu walifungwa lakini kwa jinsi walivyocheza ilionekana wazi kwamba hawakuwa na jipya.

Kuanzia hapo waliimarika zaidi na kwenda kushika nafasi ya pili katika kundi nyuma ya Al Ahly. Huenda Vita wakafanya hivyo kwa sababu wana uzoefu na soka la Afrika na kocha wao pia ni mtu mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika akiwa na mafanikio mbalimbali. Hatuwezi kuwadharau kupita kiasi.

Hawa Wasudani hatujawajua vizuri licha ya kumpoteza kocha wao aliyekuja Simba. Kuanzia hapo wamenunua mastaa wengi kwa fujo kama ambavyo Simba wamefanya hivi karibuni. Hatujui wataibadili timu yao kwa kiasi gani lakini tunachofahamu ni kwamba wengi wanaipima Al Marreikh kwa kupitia kiwango cha wapinzani wao Al Hilal.

Al Hilal walikuja Dar es salaam wiki chache zilizopita na kuonyesha kiwango kibovu dhidi ya Simba ambapo walichakazwa mabao 4-1. Kama utalipima soka la Sudan kwa kupitia Al Hilal basi huenda Simba akawa na nafasi kwa Al Marreikh hata ugenini.

Tukiachana na hilo, kocha wa Simba mheshimiwa Gomes anaonekana kuwa na uwezo wa kutibu matatizo ya Simba ambayo walikuwa nayo katika kundi lao miezi 24 iliyopita. Simba hii imecheza kwa mbinu zaidi kuliko Simba ile ya bwana Patrick Aussems. Simba hii imecheza kwa namna ya kucheza michuano kama hii na si kucheza kama Ligi Kuu.

Simba wamecheza kwa nidhamu kubwa ya ukabaji kitu ambacho hawakuwa nacho katika mechi zilizopita. Hauwezi kucheza ugenini kama upo nyumbani. Na hauwezi kucheza ugenini kama vile upo katika Ligi ukicheza dhidi ya Mbeya City au Azam.

Mwisho wa siku kila la kheri kwa Mnyama. Wanaweza kufanya maajabu na kufika mbali zaidi kama wataendelea kuamini. Katika soka achilia mbali kipaji na uwezo lakini kuamini ni kitu muhimu zaidi. Kwa sasa Simba wanaamini na wataamini zaidi jinsi wakiwa wanapata matokeo njiani.