Prime
HISIA ZANGU: Gamondi mwisho wa fungate na mwanzo wa talaka

Muktasari:
- Nakusimulia mtiririko wa mechi za watani kwanza. Namna inavyowakilisha kiujumla Yanga walipokuwa na walipo kwa sasa. Unaona kabisa namna chati inavyoshuka. Sio kwa bahati mbaya. Hakuna kitu kigumu katika soka kama kushikilia palepale ulipokuwepo. Wakati mwingine wanasema ni rahisi kuwa namba moja, lakini ni ngumu kuendelea kuwa namba moja.
ILIANZIA 5-1 Yanga wakaenda katika mabango. Ikaja 2-0 furaha ikaendelea kuwepo. Ikaja 1-0 Simba wakaondoka kwa furaha, ingawa walikuwa wamechapwa kwa sababu waliona pengo na watani limepungua. Ikaja bao 1-0 nyingine kwa bao la kujifunga la Kelvin Kijili ikaonekana ni mechi iliyoamuliwa na kitu kinachoitwa ‘bahati mbaya’.
Nakusimulia mtiririko wa mechi za watani kwanza. Namna inavyowakilisha kiujumla Yanga walipokuwa na walipo kwa sasa. Unaona kabisa namna chati inavyoshuka. Sio kwa bahati mbaya. Hakuna kitu kigumu katika soka kama kushikilia palepale ulipokuwepo. Wakati mwingine wanasema ni rahisi kuwa namba moja, lakini ni ngumu kuendelea kuwa namba moja.
Kushikilia hapohapo kunahitaji nidhamu na inaonekana hii sio moja ya sifa ya kocha wa Yanga, Miguel Gamondi. Yeye na wachezaji wake wameelekea kushindwa. Ukiachana na ‘graph’ ya mechi ya mtani kuanzia ushindi wa mabao 5-1 mpaka kufikia bao la kujifunga la Kijili, ziko wapi zile bao tano tano ambazo Yanga alikuwa akiwafunga watu pale Chamazi?

Kilikuja kisingizio kutoka kwa mashabiki na wachambuzi kwamba timu pinzani zimeisoma Yanga na sasa walikuwa wanakaa nyuma zaidi. Kisingizio cha uongo hicho. Moja kati ya kazi ya timu nzuri ni kuifungua timu iliyojifunga nyuma. Ni kitu ambacho unakitazamia wiki baada ya wiki na unalazimika kushinda mechi. Ndivyo wanavyofanya kina Manchester City.
Hata kwa wachezaji mmoja mmoja. Katika ubora wao makocha wa timu pinzani walikuwa wanajua kwamba Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ni watu hatari. Walitengeneza mipango mingi ya kuwadhibiti, lakini kila wikiendi walikuwa wanafunga tena. Erling Haaland tunajua kwamba ni hatari na tunamtengenezea mipango mingi ya kumdhibiti, lakini kila wikiendi anafunga tena na tena.
Hapo hapo Gamondi akaja na kisingizio kwamba wachezaji wake walikuwa wamechoka. Sijaona kocha mwenye raha ya kikosi kipana kama Gamondi. Ni kiasi kwamba watu huwa hatuielewi vizuri first eleven ya Yanga. Kama unajua mgawanyo sahihi wa dakika za wachezaji sioni wachezaji wa Yanga wakichoka ikiwa ndio kwanza tupo Novemba mwanzoni. Hapo pia michuano ya CAF na ile ya FA bado haijaanza katika hatua za mbele.

Nadhani Gamondi alijisahau. Raha zilimzidi kuliko kujali changamoto ambazo zilikuwa zinamkabili mbele yake. Huwa inatokea kwa wachezaji na makocha wengi ambao wanatua nchini na kufanya vizuri. Hakuna nchi tamu kuishi kama Tanzania. Maisha ni matamu. Maisha yana raha. Mashabiki nao wanaiangalia siku ya leo tu ambayo wametoka kushinda mechi.
Pale Zanzibar saa moja tu baada ya Yanga kuwafunga CBE, Gamondi aliungana na sisi kupata kinywaji. Hakuonekana kuijali tena mechi. Maisha yake yamejaa raha kwa sasa. Kuanzia nje ya uwanja na ndani ya uwanja. Ndani ya uwanja Yanga ina wachezaji wazuri kwa hiyo inaweza kushinda 1-0 na Gamondi akaenda zake kunywa bia.
Nje ya uwanja kuna maisha matamu ya Kitanzania. Naambiwa kwamba ni mtu wa kula bata. Wakati mwingine anaungana na wachezaji wake kula maisha. Na unapokuwa kocha wa Yanga au mchezaji wa Yanga, maisha yanakuwa matamu zaidi. Papo hapo kushika mambo mawili kwa wakati mgumu inakuwa shida. Yanga ya msimu huu sio ya msimu uliopita.

Aziz Ki anapoteza mipira ovyo. Ameridhika. Pacome Zouzoua naye ameridhika. Anacheza kawaida tu na wala hawaachi midomo wazi mashabiki kama ilivyokuwa msimu uliopita. Katika mechi ngumu lazima wapangwe na Clatous Chama akae katika benchi. Kisa? Gamondi amekariri na anataka kuendesha maisha rahisi kwa wachezaji wake.
Wakati Aziz akipoteza mipira ndani, Chama anakuwa ameshika tama katika benchi. Gamondi anaamini kwamba kuna jambo tu litatokea. Matokeo yake zile tano tano za msimu uliopita zimetoweka. Watu walikuwa wanaguna taratibu. Soka Gamondi likatoweka. Kwa namna walivyokuwa wanacheza siku moja niliwahi kukaririwa nikizungumza redioni Wasafi kwamba Yanga walikuwa wanakaribia kufungwa au kutoka sare.

Na kweli. Pambano dhidi ya Tabora hatimaye limevunja mzizi wa fitina. Limewaamsha rasmi Yanga kwamba wanapokwenda sio njia sahihi. Nasikia kuna mbu ambaye anatambaa katika sikio la Gamondi. Kuna wanaosema atafukuzwa muda mfupi ujao. Kuna wanaosema anaweza kuendelea kuwepo. Hata hivyo suala la kuwepo kwa uvumi tu ni dalili tosha kwamba fungate ya Gamondi na imefika mwisho.
Timu zetu hazijawahi kuwa na uvumilivu ambao Gamondi anadhani tunao. Timu zetu pia haziangalii sana historia wala rekodi zako katika msimu uliopita. Zinaishi kwa ajili ya sasa. Hata kocha aliyemuachia mikoba bwana Nasreddine Nabi hakuwa na dhambi nzito klabuni. Ilishangaza kuona Yanga wanaachana naye.
Kama akipewa nafasi ya kuendelea kuwepo kama Ally Kamwe alivyozungumza juzi, basi Gamondi anapaswa kupunguza mambo mengi ya nje ya uwanja na kuirudisha Yanga ya msimu uliopita. Yanga ya mbinyo kwa adui.
Yanga iliyo bora pindi wanapokuwa na mpira na wasipokuwa na mpira. Yanga hii ambayo iliwapa Tabora nafasi ya kuwa huru na mipira hata katika boksi inaweza kumfanya asifike Krismasi.

Yanga hii ambayo Aziz Ki anapoteza mipira anacheka huku akimtazama mrembo wake jukwaani inaweza ikamfanya Gamondi asifike Krismasi. Anahitaji kuwafanya wachezaji wasiwe katika ‘comfort zone’ kama ambavyo wamekuwa msimu huu. Ni mlokole Maxi Nzengeli tu ndiye ambaye anaonekana kuwa na hamu na mpira. Wengine wanacheza huku wakiwa wametanua makwapa.
Bahati mbaya ambayo Gamondi anaweza kupita kwa sasa na mwenyewe haijui ni kwamba kuelekea katika uvumi wa kufukuzwa hakuna mashabiki au wanachama ambao watajitokeza na kumkingia kifua. Hii ni kwa sababu wanachama na mashabiki wanaamini zaidi katika uamuzi wa rais wao kijana, Hersi Said na kamati yake ya utendaji. Kama anabisha akawaulize Nabi, Yannick Bangala na Djuma Shaban.
Waliondoka Yanga bila kuamini kilichowatokea. Na bahati mbaya kwao ni kwamba mapengo yao yalizibwa vyema na watu waliochukua nafasi zao ndio maana hata yeye Gamondi akiondolewa Yanga wanaamini atakuja mtu sahihi zaidi kuliko yeye.
Hii ndio bahati ya kufanya uamuzi sahihi. Kama uamuzi wa kuwaondoa Nabi, Bangala na Djuma ungekuwa mbovu basi Gamondi angeweza kupata wafuasi wa kumtetea.
Kama akiendelea kubaki, basi wiki chache zijazo zitakuwa na mvuto zaidi kuitazama Yanga inaibukaje kutoka katika kichapo cha Tabora. Kichapo ambacho kimekuwa na mvuto mkubwa katika mitandao ya kijamii.
Ilichosha kuisifia Yanga kila wikiendi na ilivutia kuona Yanga wakisimangwa na watani wao katika kila kona. Mabao matatu yalikuwa mengi. Walau wangefungwa moja kwa bahati mbaya.