Hii ndio 'Firt Eleven' 2021

MSIMU uliopita ulikuwa na ushindani mkubwa kwa wachezaji kuwania nafasi za kucheza ili kuzipambania timu zao kupata matokeo.
Hata hivyo, gazeti hili lililokuwa likifuatilia michezo yote ya Ligi Kuu msimu huo, linakuletea nyota 11 ‘first 11’ ikiwa ni kikosi cha msimu kutokana na viwango vyao.
Kwenye kikosi hicho kocha atakuwa, Didier Gomes aliyekuwa kocha wa Simba aliipa timu hiyo mafanikio ikiwamo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na mafanikio mengine kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Aishi Manula
Kipa chaguo la kwanza Simba msimu uliopita alikuwa kwenye kiwango bora na kutetea tuzo ya kipa bora wa msimu kwa mara ya sita mfululizo.
Ndiye kipa aliyecheza michezo mingi bila kuruhusu bao ikiwa ni katika michezo ya ndani na ile ya kimataifa Simba inayoshiriki.
Mbali na kuingia kwenye kikosi hiki bora cha Mwanaspoti pia alitwaa tuzo ya kipa bora wa Kombe la Shirikisho (ASFC) pamoja na ile ya ligi.
Shomari Kapombe
Kutokana na kiwango chake bora kimemfanya adumu kwenye kikosi cha kwanza cha Simba na timu ya Taifa Taifa Stars. Amekuwa bora kwenye kukaba na kuanzisha mashambulizi kwa kupiga pasi na krosi za maana kwa washambuliaji na muda mwingine kufunga mwenyewe.
Pamoja na Simba kufanya mabadiliko ya makocha kwa nyakati tofauti ndani ya msimu mmoja, lakini ubora wake ulimfanya kuendelea kucheza kikosi cha kwanza na kumweka benchi, David Kameta.
Mohammed Hussein
Pamoja na makosa madogo ya kiulinzi anayoyafanya hasa Simba inaposhambuliwa, ubora wake hakuna asiyeutambua kwenye kukaba na kufanya mashambilizi na hii imemfanya adumu kikosi cha kwanza cha Simba kwa muda mrefu.
Uwezo wake mkubwa ni kwenye kushambulia na imemsaidia kuendelea kuwepo kikosi cha kwanza kwa muda mrefu na kuwa nahodha akimweka nje Gadiel Michael.
Ubora huo alionyesha Tshabalala ulimfanya kuingia katika kikosi bora cha msimu pamoja na kutwaa tuzo ya beki bora.
Joash Onyango
Wakati anasajiliwa msimu uliopita hakuwa beki aliyetegemewa kuonyesha kiwango bora na kufanya makubwa kutokana na wengi kuamini ameshazeeka tayari.
Mambo yalikuwa tofauti kwa Onyango aliyeonyesha kiwango bora katika michezo yote aliyocheza akizuia mashambulizi na wakati mwingine kufunga na amekuwa nguzo muhimu kikosi cha Simba.
Dickson Job
Alisajiliwa na Yanga kutokea Mtibwa Sugar. Hakuna aliyetarajia atafanya makubwa kutokana na kimo chake pamoja na wachezaji waliokuwa kwenye nafasi hiyo. Ilikuwa ngumu kufikirika kama atawapokonya namba.
Ameonyesha kiwango bora na kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza cha Yanga akicheza beki wa kati akizuia washambuliaji wasumbufu kama Chriss Mugalu kushindwa kufunga.
Alikuwa na maelewano mazuri na Bakari Mwamnyeto ambaye muda mwingi ndio walicheza pamoja lakini nidhamu yake kubwa uwanjani ilimfanya mwisho wa msimu kutwaa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu.
Mukoko Tonombe
Ndiye alikuwa staa na nguvu katika kiungo cha Yanga msimu uliopita kutokana na ubora wake kwenye kukaba viungo washumbufu wa timu pinzani pamoja na kuifungia timu yake mabao muhimu.
Mukoko ambaye aliingia katika kikosi bora cha msimu uliopita alitimiza majukumu yake ya kiungo mkabaji pamoja na kufunga mabao muhimu katika mechi na Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Polisi Tanzania.
Alifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Yanga msimu uliopita kutokana na ubora aliokuwa nao ingawa msimu huu amekutana na wakati mgumu mbele ya Yannick Bangala na Khalid Aucho.
Clatous Chama
Katika kikosi bora cha Mwanaspoti msimu uliopita winga wa kulia atakuwa Chama ambaye aliweka rekodi mbalimbali katika ligi pengine hadi kuwavutia RS Berkane ambao walimsajili kwa pesa ndefu.
Chama msimu uliopita alifunga mabao nane na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyetoa pasi nyingi za mabao (zaidi ya 14), jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji hatari.
Kwenye mechi nyingi zile za kimataifa na ndani, Chama alihusika katika mabao mengi ambayo Simba walifunga lakini kama haitoshi msimu ulipomalizika alitwaa tuzo ya kiungo bora.
Feisal Salum
Yanga msimu uliopita haikufanikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya ndani kwani mbali ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, mengine kama Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ligi Kuu Bara yalikwenda Simba ambayo walitwaa yote.
Fei Toto licha ya Yanga kushindwa kufanya vizuri kama timu kwa upande wake alikuwa mchezaji bora katika michezo mingi ya Yanga kama si kufunga basi alihusika katika mabao.
Mwisho wa msimu Fei Toto alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la ASFC, kutokana na makali yake aliyoonyesha na hata msimu huu yamekuwa kama mwendelezo katika kila mechi.
John Bocco
Hakuanza vizuri msimu kutokana na majeraha na baada ya kurejea alionyesha makali yake na kazi kubwa aliyokuwa anafanya ni kufunga mabao katika michezo ya ligi na kumaliza kama mfungaji bora akiwa na mabao 16.
Ubora huo ulimfanya kufikisha zaidi ya mabao 120, katika ligi tangu alipocheza kwa mara ya kwanza 2009, akiwa na kikosi cha Azam.
Mwisho wa msimu alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu (MVP), ambayo wengi wao walikuwa wakifikiria itarudi tena kwa Chama.
Prince Dube
Hakumaliza msimu kutokana na majeraha lakini ndani ya muda mchache aliocheza alionyesha ni mchezaji wa aina gani hasa kwenye kufunga.
Alimaliza msimu akiwa na mabao 14, ambayo kama angepata nafasi ya kucheza mechi nyingi zaidi pengine angeongeza kasi ya ushindani ya ufungaji bora ambayo juu yake alikuwepo, Bocco, Chriss Mugalu na Meddie Kagere.
Aliachaguliwa kuingia kikosi bora cha msimu kutokana na makali yake ya kufunga mabao muhimu na makali kama lile alilowafunga Yanga mzunguko wa pili kwenye ligi.
Luis Miquisson
Alikuwa mchezaji muhimu Simba kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza mpira, hasa wakati timu hiyo inapokwenda kufanya mashambulizi.
Luis aliifungia Simba mabao muhimu kwenye mechi za ligi ndio maana alimaliza msimu akiwa na mabao tisa pamoja na zile mechi za kiamataifa kama bao la kideoni dhidi ya miamba ya soka la Afrika Al Ahly.
Pengine umahiri huo alioonyesha ndio uliwavutia matajiri hao wa Afrika Al Alhaly na kumsajili kwa mkwanja mrefu zaidi ya Sh1.5 Bilioni. Katika ligi Luis alitoa pasi za mwisho kwa wachezaji wengine kufunga mabao ambazo zilikuwa zaidi ya saba na alichaguliwa kuingia katika kikosi bora cha msimu.