Hawa wetu, Simba wapewa mbinu za mwisho

Hawa wetu, Simba wapewa mbinu za mwisho

SIMBA haitaki kurudia makosa ya nyuma na hesabu yao ni moja tu ambayo ni kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati leo itakapokabiliana na Orlando Pirates ugenini kwenye Uwanja wa Orlando, Johannesburg, Afrika Kusini kuanzia saa 1:00 usiku.

Wakati mashabiki wa timu hiyo wakiusubiri mtanange huo kwa hamu, beki Pascal Wawa ametamba kwamba lazima kieleweke akisisitiza kwamba wamejipanga kufanya maajabu, huku kocha Pablo Franko akisema kikosi kipo tayari kwa vita.

Baada ya kushindwa kuandika historia ya kutinga hatua hiyo mara mbili tofauti hapo nyuma tangu mfumo wa mashindano ya klabu Afrika ubadilike, Simba inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote katika mechi hiyo ya marudiano baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 mechi ya kwanza ili kuvuka na kucheza nusu fainali ya mashindano hayo jambo ambalo uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wana imani linawezekana.

“Lengo letu ni kutinga nusu fainali. Kama uongozi tumejipanga kuhakikisha hilo limetimia na tunaamini linawezekana. Maandalizi yote yako vizuri na tunachukua tahadhari zote kuhakikisha kile tunachokihitaji tunakitimiza. Hatutaki kurudia makosa,” alisema mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Mulamu Nghambi.


Mbinu, ufundi utaibeba Simba

Benchi la ufundi linapaswa kuandaa mbinu na mpango sahihi ambavyo ni lazima vifanyiwe kazi vyema na kwa kujitolea ndani ya uwanja wachezaji wake ndani ya dakika 90 ili kupata matokeo mazuri ambayo yatawafanya wasonge mbele na kutinga nusu fainali. Eneo la katikati ndilo la muhimu Simba wanalopaswa kuhakikisha wanalitawala na kuvuruga mipango ya wapinzani ili wasitengeneze nafasi ambazo zinaweza kuwa mwiba kwao na kuwanufaisha Orlando.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa moja ya mambo yaliyoiathiri Simba ni kukosa ubunifu eneo la kiungo kupenya au kutengeneza nafasi za mabao kwenda kwa wachezaji wa mbele na pia kasi ilikuwa chini kujenga mashambulizi ingawa mwishoni iliamka na kuonekana tishio kwa wapinzani wao. Pia Simba inapaswa kuwa makini na kujilinda zaidi pembezoni mwa uwanja hasa upande wa kushoto kwani kumekuwa kukitumika zaidi na Orlando kujenga mashambulizi na nafasi za mabao hasa kwa mipira ya krosi.

Washambuliaji Thembinkosi Lorchi na Deon Hotto ndio wanapaswa kuchungwa zaidi kwani ndio wamekuwa ubongo wa Orlando kuichezesha timu.

Na kufanikisha hilo, benchi la ufundi linaweza kuanza na mabeki wa kati watatu ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha lango linakuwa salama zaidi.


Mastaa kuoga noti

Matokeo yoyote mazuri katika mchezo huo ambayo yatawafanya wasonge mbele yatakuwa na neema kwa nyota wa Simba kwani watavuna kiasi kikubwa cha fedha za bonasi ambazo wameahidiwa na uongozi.

Kwa timu inayoingia nusu fainali za michuano hiyo hupewa Dola 450,000 (takriban Sh1 bilioni) na CAF ambazo zimeelezwa kuwa mabosi wa Simba wamewaahidi wachezaji wao kuwa endapo watapambana na kutinga hatua inayofuata, basi watapewa asilimia 75 ya pesa hizo wagawane.


Takwimu za presha

Kumbukumbu ya mechi za nyuma zinaonyesha Orlando wamekuwa timu tishio sana pindi wanapocheza mechi katika uwanja wao wa nyumbani na kinyume chake Simba wamekuwa dhaifu ugenini pindi wanacheza mechi za mashindano ya kimataifa. Katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo Orlando Pirates wamecheza nyumbani wameibuka na ushindi mara sita na kutoka sare nne huku wakifunga mabao 14 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu tu.

Hali ni tofauti kwa Simba ambayo katika mechi 10 za mwisho walizocheza ugenini za mashindano ya kimataifa, wameibuka na ushindi mara mbili, wametoka sare mbili na kupoteza michezo sita huku wakifunga mabao matano tu na kufungwa mabao 14.


Refa muungwana

Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Bernard Camille kutoka Shelisheli ambaye huwa sio mwamuzi anayependa kugawa kadi kama njugu kulinganisha na baadhi ya waamuzi barani Afrika.

Mwaka huu, refa huyo mwenye umri wa miaka 47 amechezesha mechi tatu za kimataifa na kutoa kadi sita zote ni za njano ikiwa ni wastani wa kadi mbili tu kwa kila mchezo.


Kikosi kimetimia

Urejeo wa kiungo Sadio Kanoute na beki Joash Onyango unalipa wigo mpana wa uteuzi kikosi benchi la ufundi la Simba katika mchezo huo watakaomkosa Bernard Morrison ambaye hajasafiri kwenda Afrika Kusini.

Kikosi cha Simba leo kinaweza kuwa hivi; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Pascal Wawa, Joash Onyango, Enock Inonga, Pape Sakho, Jonas Mkude, Chris Mugalu, Sadio Kanoute na Rally Bwalya.


Kikosi matumaini kibao

Kocha wa Simba, Pablo alisema kuwa ana imani timu yake itafanya vizuri na kufuzu nusu fainali. “Ni mechi ngumu na tumekuwa hatuna historia nzuri ugenini, lakini jambo muhimu kukabiliana na hilo ni kujiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huu ambao tutakuwa ugenini. Orlando ni timu nzuri na wachezaji wangu wanapaswa kufanya kazi ya ziada ili tuweze kusonga mbele,” alisema Pablo.

Beki wa Simba, Pascal Wawa alisema: “Kama nilivyowahi kusema awali lengo sio kufika nusu fainali pekee, bali tunahitaji kuvuka na kufika fainali. Tunamtanguliza Mungu atuongoze kwenye hili nasi wachezaji tutapambana kufanikisha.

“Tunafahamu mchezo wa marudiano utakuwa mgumu, Orlando watataka kupindua matokeo, lakini tumejipanga kuhakikisha tunawazuia ili tupate nafasi ya kusonga mbele.”


WAMBURA AIBUKA

Wakati kocha na wachezaji Simba wakitamba kupambana ili kupata ushindi, aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na katibu mkuu wa Simba, Michael Wambura alikuwa na jambo la kuwaambia wachezaji wa timu hiyo. “Waingie uwanjani wakiwa na hali ya kuwaheshimu wapinzani wao wakishakuwa hivyo naamini watashangaza sana. Najua kocha wao kuna vitu amewataka wavifanye basi wahakikishe dakika zote 90 wanafanya walichoelekezwa,” alisema.

Alisema, historia sio ishu kwa sasa kutokana na Simba kupoteza michezo yake iwapo ugenini, na kwamba waliwahi kuifunga Zamalek kwao hivyo lolote linaweza kutokea kutokana na mpira kubadilika kwa sasa.

“Sijui wachezaji wetu wawapo nje wanakuwa na wasiwasi gani, maana siwaelewi kabisa hata wa timu ya Taifa na wao wanakuwa hivyo hivyo, lakini wakija uwanja wa nyumbani wanacheza vizuri, wanatakiwa kuacha uoga huo.”