ZeKICK: Tulieni tunatoboa huko huko kwao

Simba yakwepa figisu za Wasauzi

HOMA ya mchezo wa marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wa Orlando Pirates dhidi ya Simba SC, inazidi kupamba moto huku makocha wa timu hizo, Mandla Ncikazi na Pablo Franco kila mmoja akiumiza kichwa ni kwa namna gani anaweza kutegua mitego ya mwenzake.

Simba ambao wanaenda Afrika Kusini wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 4-0 kwenye robo fainali yao iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chief, wana mtaji wa bao 1-0 ambalo walilipata kwenye mchezo wa kwanza kwa Mkapa.

Urejeo wa beki wake wa kati, Joash Onyango na kiungo, Sadio Kanoute ni kati ya faida ambazo kocha wa Simba, Pablo anazo kwenye mchezo huu wa marudiano maana alikosa huduma za wachezaji hao kutokana na kutumikia kwao adhabu ya kuonyeshwa kadi tatu za njano kwenye hatua ya makundi.

Wakati Pablo akiumiza kichwa kwa namna gani atawazuia Orlando Pirates ambao wamekuwa na rekodi nzuri hasa wanapokuwa nyumbani, mwenzake Mandla ambaye alipiga kelele kwenye mchezo wa kwanza baada ya kupoteza akidai mwamuzi hakuwa upande wao na walifanyiwa vitendo vya hovyo.

Atakuwa na kibarua cha kuifungua Simba na kukomboa bao ambalo walifungwa na Shomary Kapombe kwa mkwaju wa penalti baada ya kufanyiwa madhambi kwa mchezaji wa zamani wa timu hiyo ya Soweto, Bernard Morrison.

Licha ya kwamba, Pablo atakuwa na faida ya urejeo wa wachezaji wake wawili muhimu, Onyango na Kanoute, atakuwa na changamoto ya kuunda safu yake ya ushambuliaji bila ya Morrison ambaye ana kizuizi cha kuingia Afrika Kusini hivyo hatakuwa sehemu ya mchezo huo.


ORLANDO NYUMBANI

Kati ya michezo minne ambayo Orlando Pirates imecheza nyumbani kwenye michuano hiyo ya kimataifa, imeshinda mitatu na kutoka sare mmoja, haijaruhusu bao hata moja hivyo Pablo na vijana wake wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuvunja mwiko wa wapinzani wao.

Msimu huu, Orlando Pirates ilianzia hatua ya raundi ya pili kwa kupigania tiketi ya kutinga makundi ambapo walicheza dhidi ya CSMD Diables Noirs ya Congo, walitoka suluhu mjini Brazzaville na waliporejea nyumbani kufunga hesabu waliitandika timu hiyo bao 1-0 lililofungwa na mkongwe, Happy Quinton Jele.

Jele ndiye mchezaji mwandamizi zaidi kwenye kikosi cha Orlando Pirates kiasi cha kukabidhiwa mikoba ya unahodha ndani ya timu hiyo ambayo kwenye ligi yao ya ndani mwenendo wao sio mzuri. Yupo na klabu hiyo tangu 2006, ameichezea zaidi ya michezo 400 kwenye mashindano yote.

Katika hatua ya mchujo ‘Play-off’ ambayo imekuwa ikihusisha timu zilizopenya kutoka raundi ya pili na zile zilizofungashiwa virago upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Orlando ilipangwa kucheza dhidi ya LPRC Oilers ya Liberia ambapo ulichezwa mchezo mmoja tu wakiwa ugenini walishinda kwa mabao 2-0, hapakuwa na mchezo wa marudiano baada ya wapinzani wao kujiondoa.

Wababe hao wa Afrika Kusini kwenye hatua ya makundi walipangwa kundi B na katika hatua hiyo wakiwa nyumbani walizitandika JS Saoura kwa mabao 2-0, Royal Leopards kwa mabao 3-0 huku wakitoka suluhu dhidi ya Al-Ittihad ya Libya. Hawakuruhusu bao nyumbani na ndio waliokuwa vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi 13 huku wakifuatiwa na Al-Ittihad (11).

Ndani ya michezo minne waliyocheza nyumbani, wamefunga mabao sita na manne kati ya hayo wamefunga kipindi cha pili kuanzia dakika ya 45 hadi 75 huku mawili yakiwa kipindi cha kwanza (Dk 0-30).


SIMBA UGENINI

Ndani ya msimu minne kwenye michuano ya kimataifa, Simba imetinga robo fainali ya michuano ya kimataifa mara tatu, ikifuzu hatua hiyo mara mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na mara moja msimu huu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, gazeti hili limebaini kuwa kitu kikubwa kilichoikwamisha timu hiyo kutinga nusu fainali mara mbili mfululizo ni kuruhusu kipigo kikubwa katika mechi za ugenini.

Msimu wa 2018/2019 Simba ilitinga robo fainali baada ya kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi dhidi ya timu za JS Saoura ya Algeria, AS Vita ya Congo na Al Ahly ya Misri.

Licha ya kwamba ilipoteza mechi zote tatu ugenini kwa mabao 5-0 dhidi ya Al Ahly na AS Vita na mabao 2-0 dhidi ya JS Saoura lakini ushindi katika mechi zote tatu za nyumbani uliwabeba hasa mechi ya mwisho ilipoichapa AS Vita mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Machi 16, 2019 kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa.

Baada ya ushindi huo Simba ikatinga robo fainali lakini licha ya kutoka suluhu ya 0-0 na TP Mazembe katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa (Aprili 4, 2019) lakini ikajikuta ikishindwa kutinga nusu fainali baada ya kuruhusu kichapo cha mabao 4-1 ugenini nchini DR Congo, Aprili 13, 2019.

Wekundu wa Msimbazi wakapata tena nafasi ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita lakini gundu la kukomea hatua hiyo likawaandama tena.

Licha ya kwamba kwenye hatua ya makundi ilijitahidi kukomaa katika mechi za ugenini kwa kushinda moja kati ya tatu huku ikipoteza moja na kutoka sare mchezo mmoja lakini ikajikuta iki tupwa nje ya mashindano hayo kwenye hatua ya robo fainali baada ya kuruhusu mabao mengi ugenini.

Simba ilichapwa mabao 4-0 ugenini dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali uliofanyika Mei 15 mwaka jana lakini ikashinda mabao 3-0 nyumbani katika mchezo wa marudiano uliofanyika Mei 22 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa na kutolewa kwenye mashindano hayo.


MAKOCHA WAFUNGUKA

Kocha wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa alisema Simba wanapaswa kucheza kwa tahadhari sana ugenini lakini wahakikishe kila nafasi wanayopata wanaitumia vizuri.

“Mechi za ugenini huwa zina aina ya kuzicheza. Jambo kubwa wanatakiwa kuangalia mpinzani wake anachezaje akiwa nyumbani hii itamsaidia sana kujua ubora na udhaifu ambao utakuwa ni silaha ya kumpatia matokeo chanya yatakayowawezesha kutinga nusu fainali msimu huu,” alisema Mkwasa.

Kocha wa Biashara United, Vivier Bahati alisema vipigo vya mara kwa mara vya ugenini ndio changamoto kubwa kwa timu hiyo kutinga nusu fainali kwenye mashindano ya kimataifa jambo ambalo wanatakiwa kulifanyia kazi haraka wanapoenda kuikabili Orlando nchini Afrika Kusini.

“Lazima wajue kwanza kucheza mechi za ugenini waangalie wapi walikuwa wanakosea mwanzo na kurekebisha. Kwenye mechi hiyo ya Jumapili wanatakiwa kucheza kwa uangalifu kama timu kwa maana ya kuzuia na kushambulia kwa pamoja, hii itawapa ari na kuwaongezea presha wapinzani wao.”


MWAMUZI NI KIBOKO

Bernard Camille, 46, kutoka Shelisheli ni kati ya waamuzi ambao wamekuwa wakichezesha kiungwana sio muumini wa kumwaga sana kadi kwani kwenye michezo yake minne iliyopita ana wastani wa kutoa kadi mbili.

Michezo hiyo minne aliyochezesha ni dhidi ya ASEC Mimosas dhidi ya SGN hawa walikuwa kundi moja na Simba na mchezo huo ukamalizika kwa mwenyeji kushinda kwa mabao 2-1, hakutoa kadi yoyote.

Kwenye mchezo kati ya Sagrada Esperanca dhidi ya Zamalek ambao ulikuwa na kashikashi na hapa na pale alionekana kuumudu na kutoa kadi tatu tu za njano, kadi nyingi alizotoa ni nne na ilikuwa kwenye mchezo wa Afcon 2021 kule Cameroon kati ya Mali na Mauritania (2-0).

Watanzania wanakumbuka vizuri, Camille kwani Novemba 11, 2021 alichezesha mchezo wa kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Mkapa, Taifa Stars dhidi ya DR Congo, alitoa kadi mbili za njano.

Katika mchezo huo ambao Taifa Stars ilichapwa mabao 3-0, kadi hizo za njano walionyeshwa, Fuka-Arthur Masuaku na Chadrac Ababa wa DR Congo.


KERR ATIA NENO

Kocha Dylan Kerr ambaye amekutana na Orlando Pirates kwenye michezo mitano ya ushindani akiwa na Moroka Swallows, alisema siri ya mafanikio kwake kuwamudu wababe hao wa soka la Afrika Kusini imetokana na mbinu ambazo amekuwa akizitumia.

Muingereza huyo ambaye aliwahi kuinoa Simba na Gor Mahia hakuficha, alisema mbinu hizo ni kucheza kwa kujilinda kama timu na jambo hilo lisiwe jukumu la mabeki tu, huku akitumia mtaji wa kasi kwa washambuliaji wake, Lebohang Mokoena na Keletso Makgalwa kuwashambulia wapinzani wao pindi wanapoacha mianya.

“Nakumbuka mara mwisho kucheza dhidi ya Orlando nilitumia mfumo wa 4-3-3, tulitengeneza vizuizi vitatu kila pembe, haikuwa rahisi kufika eneo letu, tulifunga njia, kila mpira ambao tulikuwa tukiupata tulihakikisha unakuwa na madhara kwao,” alisema na kuongeza:

“Haikuwa rahisi kupata pointi dhidi yao lakini iliwezekana kwa sababu tulijua kuwa ubora wao upo sehemu mbili, eneo la kiungo (kati) na pembeni (wingi) kuwa na vikwazo vingi ambavyo tuliviandaa iliwapa wakati mgumu, ilikuwa wakija tunapishana nao maana kila ambapo tuliupata mpira tulikuwa tukifika kwa haraka kwenye eneo lao. Kasi, kasi, kasi ilitubeba.”

Katika michezo mitano ambayo Kerr ameiongoza Moroka Swallows kucheza dhidi ya Orlando Pirates, ameshinda mchezo mmoja kwa mabao 2-1 ambao ulikuwa wa hatua ya robo fainali ya Kombe la MTN 8, ametopeza mara moja tu na ilikuwa kwa kufungwa bao 1-0 na michezo iliyosalia wametoka sare.

Kerr alisema Simba wanatakiwa kuwa tayari kwa kukabiliana na upinzani mkubwa kutokana na uhitaji wa wapinzani wao kutaka kupindua matokeo ya jijini Dar es Salaam hivyo presha ambayo wenyeji watakuwa nayo kama wakitulia inaweza kuwa faida kwao kwani wanaweza kuacha mianya nyuma.

“Kinachotakiwa ni kuandaa mbinu ambazo zinaweza kuwasaidia kufika kwa haraka kwa wapinzani wao, vinginevyo mambo yanaweza kuwa magumu,” alisema kocha huyo.