Simba ugenini pia noma

Pablo! Kwa Orlando imeisha mapema tu

KAMA unaamini Simba haiwezi kupata sare au ushindi ugenini kwenye mechi za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) sahau, kwani imewahi kufanya hivyo mara kibao na kusonga mbele zaidi.

Simba kesho itakuwa ugenini Afrika Kusini kucheza mechi ya marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo inahitaji matokeo ya ushindi au sare ili kutinga nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kushinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza nyumbani Aprili 17, mwaka huu.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936, Simba imeshiriki michuano mbalimbali ya Afrika lakini kubwa zaidi ni ile iliyo chini ya shirikisho la soka Afrika (CAF), ambako pia imeweza kushinda na kupata sare ugenini matokeo ambayo inayataka kesho dhidi ya Orlando Pirates.

Hizi ni mechi za Simba za CAF ambazo imetisha ugenini kwa kutoa sare na kushinda hivyo huenda kesho rekodi zikajirudia na kutoa sare au kushinda kisha kutinga nusu fainali.


KOMBE LA MABINGWA

Ikishiriki kwa mara ya kwanza Kombe la Mabingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), Simba iliichapa Linare FC ya Lesotho 3-1 nyumbani kwake na kushinda 2-1 kwenye mechi ya marudiano nyumbani na kusonga hatua ya pili mwaka 1974 ambapo pia iliichapa Green Buffaloes 2-1 nyumbani kwake Zambia na kushinda 1-0 nyumbani matokeo yaliyoipeleka robo fainali. Katika robo fainali hiyo, Simba pia ilishinda 2-1 ugenini Ghana dhidi ya Hearts of Oak na kutoa suluhu Tanzania kwenye mchezo wa marudiano kisha kutinga nusu fainali ilipotolewa na Ghazi El Mahalla ya Misri kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1 kila timu ikishinda kwake 1-0.

Mwaka 1977 pia ilipata suluhu ugenini Nigeria katika hatua ya pili ya mtoano dhidi ya Water Corporation FC lakini ikafungwa 1-0 nyumbani na kuondoshwa kwenye michuano hiyo.

Katika hatua ya kwanza ya mtoano 1994, Simba iliichapa Al Merrikh ya Sudan bao 1-0 nyumbani kwao Sudan na kuichapa tena 1-0 Tanzania kisha kuvuka hatua ya pili ilipokutana na BTM Antananarivo ya Madagascar na kuichapa 1-0 nyumbani kisha kutoa suluhu ugenini na kutinga robo fainali ilipoondoshwa na Nkana Red Devils kwa matokeo ya jumla ya mabao 4-3. Simba mwaka 1995 pia ilitoa sare ya bao 1-1 ugenini Zambia dhidi ya Power Dynamos matokeo yaliyojirudia Tanzania na kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-3, kisha kutinga hatua ya pili ambapo ilitolewa na Asec Mimosac ya Ivory Coast kwa matokeo ya jumla ya mabao 4-2.


LIGI YA MABIGWA AFRIKA

Simba ikishiriki kwa mara ya pili michuano hii baada ya kubadilishwa jina, mwaka 2003 ilishinda 1-0 nyumbani dhidi ya BDF XI ya Botswana na kwenda kushinda ugenini 3-1 kwenye mechi za awali na kufuzu hatua ya kwanza ya mtoano ilipopangwa na Santos ya Afrika Kusini na kutoa suluhu (0-0), nyumbani na ugenini na kufuzu hatua ya pili kwa penalti 9-8.

Hatua iliyofuata ilicheza na Zamalek ya Misri na kushinda 1-0 na kwenda ugenini ikafungwa 1-0 na kuwatoa Zamalek kwa penalti 3-2 na kutinga makundi ilipomaliza nafasi ya tatu kwenye kundi A lililokuwa na Enyimba ya Nigeria, Ismaily ya Misri na Asec Mimosas ya Ivori Coast.

Mwaka 2005 ilicheza hatua ya awali ya mtoano na Ferroviario Nampula ya Msumbiji na kushinda 2-1 lakini ikaenda ugenini na kutoa sare ya bao 1-1 matokeo yaliyoivusha hatua ya pili ikatolewa na Enyimba ya Nigeria.

Mwaka 2008 ilicheza tena hatua ya awali ya mtoano Ligi ya Mabingwa dhidi ya Awassa City ya Ethiopia na kushinda 3-0 nyumbani kisha ugenini kutoa sare ya bao 1-1 na kutinga hatua ya pili ikatolewa na Enyimba tena kama mwaka 2005.

Mwaka 2011 pia ishinda ugenini kwenye hatua ya awali dhidi ya Elan Club ya Comoro kutoa suluhu nyumbani na matokeo ya jumla kuwa 4-2 na kusonga hatua inayofuata na kutolewa na TP Mazembe.

Msimu wa 2018-19 pia ilionyesha ubabe kwa Mbambane Swallows ya Eswatini kwa kuichapa 4-1 nyumbani na kwenda kushinda 4-0 ugenini na kwenda hatua ya mtoano ya pili ikaiondosha Nkana kwa jumla ya mabao 4-3 kisha kutinga makundi ambapo ilivuka na kufika robo fainali ilipotolewa na Mazembe kwa matokeo ya jumla 4-1. Licha ya kutolewa kwa bao la ugenini, msimu wa 2019-20 na UD Songo lakini Simba ilionyesha kuwa inaweza kupata matokeo yoyote ugenini baada ya kutoa suluhu Msumbiji na kupata sare ya bao 1-1 nyumbani.

Msimu uliopita pia ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Plateau United ya Nigeria katika hatua awali ya mtoano na kutoa suluhu nyumbani ikatinga hatua ya kwanza ya mtoano na kuitoa FC Platinum ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 4-1 kisha kutinga makundi ambako nako iliifunga AS Vita nyumbani kwake DRC bao 1-0 na kutoa sare Sudan dhidi ya Al-Merrikh matokeo ambayo yaliifanya iongoze kundi hilo mbele ya vigogo Al Ahly na kutinga robo fainali ikatolewa na Kaizer Chief kwa jumla ya mabao 4-3.

Msimu huu pia iliuanza kwa kishindo ikishinda 2-0 ugenini Botswana dhidi ya Jwaneng Galaxy lakini mambo yalikuja kubadilika baadaye ikapigwa 3-1 nyumbani na Galaxy kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.


KOMBE LA WASHINDI

Simba ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1985.

2001: FC Djan ya Madagascar 0 - 3 Simba (Djan ikajiondoa haikuja Dar) Simba ikatolewa katika raundi ya pili na Ismaily ya Misri.

Katika michuano hiyo Simba ilishiriki mara tatu mwaka 1985, 1996 na 2001.


KOMBE LA CAF

Mwaka 1993 kwa mara ya kwanza Simba ilishiriki Kombe la CAF kwa mafanikio na kufika hadi fainali huku ikishinda na kupata sare mechi za ugenini.


Hatua ya kwanza:

Nyumbani: Simba 0 - 0 Ferroviario de Maputo ya Msumbiji

Ugenini: Ferroviario 1-1 Simba

Hatua ya pili mtoano

Nyumbani: Simba 1-0 Manzini Wanderers ya Eswatini

Ugenini: Manzini 0-1 Simba

Robo fainali

Ikaitoa USM El Harrach Algeria kwa mabao ya jumla 3-1.


Nusu fainali

Nyumbani: Simba 3-1 ASA ya Angola

Ugenini: ASA 0-0 Simba

Fainali

Ugenini: Stella Adjame (Ivory Coast) 0-0 Simba

Nyumbani: Simba 0-2 Stella

Mwaka 1997:

Simba 4-1 Dire Dawa Locomotive ya Ethiopia

Ugenini: Dire Dawa 0-1 Simba

Hatua ya pili mtoano

Simba ilitolewa na AFC Leopards ya Kenya kwa jumla ya mabao 4-1.


KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

Mwaka 2007 ilishiriki kwa mara ya kwanza kombe hili baada ya kubadilishwa kutoka kuitwa Kombe la Washindi ambapo ilitoa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Textil do Pungue ya Msumbiji na kuchapwa 4-2 nyumbani kisha kutolewa.


Mwaka 2010:

Hatua ya kwanza (mtoano)

Ugenini: Lengthens (Zimbambwe) 0-3 Simba

Nyumbani: Simba 2-1 Lengthens

Hatua ya pili (mtoano)

Ikatolewa na Haras El Hadood ya Misri kwa kichapo cha jumla cha mabao 6-3.

Mwaka 2018:

Hatua ya kwanza

Nyumbani: Simba 4-0 Gendarmerie Nationale ya Djibouti

Ugenini: Gendarmerie 1-0 Simba

Hatua ya pili

Nyumbani: Simba 2-2 Al Masry ya Misri

Ugenini: Al Masry 0-0 Simba.

Msimu huu

Hatua ya makundi:

Ugenini: US Gendamerie 1-1 Simba.


MAKOCHA WAFUNGUKA

Kocha wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa alisema Simba wanapaswa kucheza kwa tahadhari ugenini, lakini wahakikishe kila nafasi wanayopata wanaitumia vizuri.

“Mechi za ugenini huwa zina aina ya kuzicheza. Jambo kubwa wanatakiwa kuangalia mpinzani wake anachezaje akiwa nyumbani hii itamsaidia sana kujua ubora na udhaifu ambao utakuwa ni silaha ya kumpatia matokeo chanya yatakayowawezesha kutinga nusu fainali msimu huu,” alisema Mkwasa.