Hawa ndio waliobadili upepo wa Simba Kimataifa

WAITE Wakimataifa, hujakosea. Waite wana robo fainali wa Caf, hujakosea pia. Hayo mambo wameshazoea. Ndio maana hata Ofisa hawabai wao, Ahmedy Ally anajiita ‘Semaji la Caf’. Ni haki yao.

Simba kucheza kimataifa kwa mafanikio kwa sasa acha watambe. Haikuwa kazi rahisi kufika walikofika. Kuna kipindi mashindano ya kimataifa waliyasikia kwenye Bomba. Ni kama yalikuwa hayawahusu. Lakini sasa, wameyazoea.

Mwaka 1993 Simba ilitisha na kufika fainali ya Kombe la CAF ila ikakosa ubingwa kwa kufungwa jumla ya mabao 2-0, na Stella Adjame ya Ivory Coast, mwaka 1994 ilikaza tena kimataifa na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kisha kutolewa na Nkana Red Devils ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3 na ugumu wa Wanamsimbazi Kimataifa ukaanzia hapo.

Ikaanza kusuasua kimataifa na mara nyingi iliishia hatua za awali hadi mwaka 2003 ilipotinga hatua ya makundi (Top 8) ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikamaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi A, nyuma ya Enyimba ya Nigeria, Ismaily ya Misri ikashindwa kusonga mbele sambamba na Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyoburuza mkia kwenye kundi hilo.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa Simba kwa karne hiyo kufika hatua ya makundi kwenye michuano ya Caf na baada ya hapo ilikuwa ikiishia kwenye hatua za awali na wakati mwingine kutoshiriki kabisa.

Mwaka 2013 ilishiriki Ligi ya Mabingwa na kutolewa katika hatua za awali kabisa na baada ya hapo ilisota miaka mitano bila kushiriki mashindano ya Caf. Nyakati hizo Azam na Yanga ndizo zilikuwa zikishiriki mara kwa mara na Simba ikaanza kutaniwa kwa kupewa majina ya kejeli ikiwamo ‘Wamchangani’ na ‘Wahapahapa’.

Ni kama miaka hiyo mitano waliyosota bila kucheza michuano ya Caf walikuwa wanasuka bomu na mwaka 2018 ilikuwa ndio wakati sahihi wa kulipua bomu hilo.

Baada ya msoto wa muda mrefu, msimu wa 2018-2019 Simba ilirejea katika makali yake kwenye michuano ya Caf ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kufika robo fainali.

Mwaka huo ulikuwa wa kuamka kwa Simba kwani baada ya hapo imekuwa ya kimataifa kweli kweli na kucheza makundi ya Caf imekuwa jambo la kawaida kwao huku sasa wakiwaza zaidi ubingwa.

Hadi sasa Simba imefika robo fainali michuano ya Caf mara nne na msimu huu iko hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ikiitafuta robo fainali ya tano tangu ilipoamka na kuwa ‘Wakimataifa’.

Mwanaspoti linakuletea kikosi kamili kilichofanya mapinduzi hayo ya Simba mwaka 2018 na kurejesha heshima Msimbazi jambo linalowapa kiburi mashabiki wa timu hiyo hadi sasa wanajiita ‘Wakimataifa’.


MAKIPA

Ili kuhakikisha mapinduzi hayo yanafanyika, Simba ilitinga Azam FC na kumng’oa kipa Aishi Manula na kumrejesha nchini kipa Deogratius Munishi aliyekuwa University of Pretoria FC ya Afrika Kusini, huku kipa namba tatu, Ally Salim akipandishwa kutoka timu ya vijana wakati huo.

Manula na Munishi walisimama vyema langoni kwa Simba na kuhakikisha heshima inarejea Msimbazi. Kwa wakati huo Ally alikuwa hachezi mechi bali kuchota maarifa na uzoefu kutoka kwa wawili hao.

Manula na Ally bado wapo Simba hadi sasa huku Munishi akikipiga Namungo.


MABEKI

Msimu huo Simba ilijiimarisha katika safu ya ulinzi kwa kuwa na mabeki 10. Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Asante Kwasi, Nicholaus Gyani, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili, Paul Bukaba, Vicent Coasta na Salim Mbonde.

Kapombe, Hussein ndio mabeki pekee wamebaki Simba hadi sasa huku Kwasi, Wawa, Costa na Mbonde wakiwa hawana timu hadi sasa, Gyani akiwa Singida Fountain Gate, Mlipili akicheza Tanzania Prisons, Bukaba akiwa Biashara United na Nyoni akiwa Namungo.


VIUNGO

Katika usajili wa Simba kwa msimu wa 2018/2019, eneo la kiungo lilikuwa limesheheni mafundi 12 ambao ni Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Clatous Chama, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga, Mohamed Ibrahim, Marcel Kaheza, Abdul Hamis ‘Sopu’, Rashid Juma, Saidi Ndemla na James Kotei.

Kati ya hao Mzamiru na Chama ndio pekee wamesalia Msimbazi, Mkude yupo Yanga, Kichuya, Ndemla na Dilunga wapo JKT Tanzania, Niyonzima anacheza Taawon Ajdad ya Libya, Sopu yupo Azam, Juma anacheza Mtibwa, Kotei, Mo Ibrahim na Kaheza wako huru.


WASHAMBULIAJI

Ili kuhakikisha nyavu zinatikiswa kisawa sawa, Simba iliandikisha washambuliaji watano, Emmanuel Okwi, John Bocco, Meddie Kagere, Adam Salamba na Mohamed Rashid.

Bocco pekee ndiye amesalia Simba huku Kagere akiwa Namungo, Salamba Ly Stade Club ya Libya wakati Okwi na Mo’ Rashid wakiwa huru.


BENCHI LA UFUNDI

Pamoja na kuwa na wachezaji wengi kikosini hapo, lakini kazi kubwa ya kurejesha heshima ya Simba ilifanywa na benchi la ufundi lililokuwa imara zaidi.

Kocha mkuu wa wakati huo alikuwa Patrick Aussems, msaidizi wake akiwa Masoud Djuma Irambona, Mwalami Mohamed alikuwa kocha wa makipa kuku Adel Zrane akiwa kocha wa viungo na Daktari wa timu alikuwa Yassin Gembe  ambaye kwa sasa ni marehemu.

Kwa sasa wote hao hawapo Simba, Aussems kwa sasa hana timu, Djuma yupo huru, Zrane ni kocha wa viungo wa APR ya Rwanda huku Mwalami akiwa hana timu akiendelea kusota rumande.

Kiufupi katika wachezaji 30 waliokuwepo Simba iliyofanya mapinduzi ya kimataifa mwaka 2018, saba tu ndio wamesalia, Manula, Ally, Kapombe, Hussein, Mzamiru, Bocco na Chama aliyeondoka kwenda RS Berkane ya Morocco lakini baadae akarejea Msimbazi.