Prime
Tafsiri ya ajabu kanuni za uchaguzi TFF

Muktasari:
- Mtu yeyote anayeamua kubadili kanuni na kuweka masharti magumu wakati uchaguzi umekaribia, huyo hafikirii maendeleo ya mchezo anaouongoza, bali anafikiria jinsi ya kujilinda aendelee kuwepo madarakani kwa udi na uvumba.
KUNA kila uthibitisho kuwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wajumbe wa mkutano mkuu wa chombo hicho hawakutaka mtu yeyote apambane na rais wa sasa, Wallace Karia kwa hoja kwamba amefanya mengi.
Mtu yeyote anayeamua kubadili kanuni na kuweka masharti magumu wakati uchaguzi umekaribia, huyo hafikirii maendeleo ya mchezo anaouongoza, bali anafikiria jinsi ya kujilinda aendelee kuwepo madarakani kwa udi na uvumba.
Na wajumbe wanapoamua kugeuza hoja za mkutano mkuu wa kawaida kuwa sehemu ya kumpigia mtu kampeni na kufikia maazimio ya kumpigia kura mgombea mmoja, hawataki mtu mwingine aingize changamoto katika kile walichokiona hata kama kipya kitakuwa kizuri zaidi.
Ndivyo ilivyofanyika mjini Moshi mwaka jana wakati Murtaza Mangungu aliyeingia mkutanoni akiwa mwenyekiti wa Klabu ya Simba alipoibua hoja ya kuweka azimio la kumuunga mkono Karia, halafu likaungwa mkono na rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na baadaye wanachama 45.
Lakini lililo kuu ni lile lililotamkwa na m,enyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kibamba Kiomoni wakati akitangaza matokeo ya usaili wa wagombea wa nafasi za urais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Alikuwa ameulizwa sababu za kutupa pingamizi lililowasilishwa na Klabu ya Yanga dhidi ya Karia lililodai kuwa alitumia madaraka vibaya kwa kuchukua udhamini wa wanachama 46, akijua kuwa baadhi ya haohao wanachama walitakiwa kudhamini wagombea wengine.
Pia walidai kugombea kwa Karia kunakwenda kinyume na sera ya michezo inayotaka rais akae kwa vipindi viwili vya miaka minne au vitatu vya miaka mitatu.
Lakini Kibamba aliwaambia waandishi kuwa walitupilia mbali pingamizi hilo eti kwa sababu aliyeliwasilisha, si aliyefika mbele ya Kamati ya Uchaguzi kulitetea. Na akasema hilo ni ‘cha mtoto’ kwa kuwa eti kanuni zinamtaka anayehudhuria mkutano mkuu, yaani rais au mwenyekiti wa klabu ndiye anatakiwa afike mbele ya kamati hiyo. Sijui alitoa wapi tafsiri hiyo.
Kanuni ya 11 (3) inasema “objections may be raised by only TFF members and /or elected official(s) of TFF and its member associations. Any objection shall be in writing stating clearly grounds for objection, accompanied with supporting evidence and shall bear the full name, permanent address and signature of the person or the chairperson/secretary of the respective member association filling the ojection.”
Au kwa tafsiri rahisi ni kwamba pingamizi linaweza kuwekwa na wanachama wa TFF tu na/au viongozi wa kuchaguliwa wa TFF na vyama wanachama wake. Pingamizi lolote ni lazima liwe la maandishi likieleza kwa uwazi sababu za pingamizi, likiambatana na ushahidi na litakuwa na jina kamili, anuani ya eneo na saini ya mtu aliyewasilisha pingamizi au mwenyekiti/katibu wa chama kilichoweka pingamizi.
Kwa tafsiri ya haraka hapo ni kwamba kanuni inajua kuwa kuna vyama au taasisi zinazoweza kuwasilisha pingamizi na hali kadhalika kuna viongozi wa kuchaguliwa wanaoweza kuwasilisha pingamizi.
Kwa hiyo, inataka majina kamili ya anayewasilisha pingamizi kama si taasisi au jina la mwenyekiti au katibu wa chama kilichowasilisha pingamizi.
Kwa hiyo huko mbele kanuni ya 11 (6) inaposema “the objector and candidate shall be required to attend in person at the hearing”- haimaanishi pekee kwamba aliyeandikwa jina au mwenye saini katika pingamizi hilo, ndiye atakayetakiwa kutokea mwenyewe katika usikilizaji wa pingamizi.
Kwa yule kiongozi wa kuchaguliwa atatakiwa afike mwenyewe kwa kuwa si taasisi, lakini kama kanuni imetambua kuwa watendaji rasmi katika taasisi au chama mwanachama ni ama mwenyekiti au katibu, inajua kuwa kuna taasisi ambayo inaweza kuwakilishwa ilimradi tu mmoja kati ya wawili hao awe amesaini hllo pingamizi.
Hakuna sehemu katika kanuni ambayo inataka aliyesaini pingamizi ndiye afike mbele ya kamati wakati wa usikilizwaji wa shauri. Huko ni kujaribu kubinya changamoto zinazoweza kuwekwa na wanafamilia. Kibaya zaidi ni kwamba hata hilo pingamizi halikusikilizwa eti kwa sababu tu ya hiyo tafsiri mbovu ya kanuni.
Mahakama au vyombo vyote vya haki vinavyofanya kazi nje ya mahakama za kiraia, huwa zinataka kufanya uamuzi kwa kupata ukweli wa jambo halisi na si kutumia mbinu za kiufundi kufikia uamuzi.
Katika mahakama ya kawaida, muwasilisha shauri anaweza asipate haki yake kwa sababu tu alikosea kiapo. Kwa hiyo hata kama alikuwa na hoja zenye mashiko, bado suala lake haliwezi kusikilizwa. Ndio maana kuna watu ni wachafu, lakini wanatumia mbinu hizo kushinda mahakamani.
Haya ni mambo ambayo mchezo kama soka ulitaka kuondokana nayo. Mpira unataka ukweli na si kukwamisha jambo kwa sababu za kiufundi. Hata aliyetunga kanuni hiyo ya mweka pingamizi afike mwenyewe na asipofika, atakuwa amepoteza haki yake, alikuwa na akili hiyo ya taratibu za kimahakama na si za kimpira.
Kama tuliondoka mahakamani kwa kuwa kuna ucheleweshaji, kuna ushindi wa mbinu za kiufundi na mengineyo, hatuna budi kufanya uamuzi kwa kutumia haki ambayo itausaidia mpira na si ujanjaujanja unaonufaisha wachache huku ukiua mpira wa miguu.
Suala la matumizi mabaya ya madaraka lilitakiwa lisukumiwe kwa Kamati ya Maadili ili ilijadili kwa kina na pengine kuamuru kanuni hiyo ya mgombea mmoja kuchukua karibu wadhamini wote ifutwe na kuandikwa upya. Ndivyo vyombo huru vinavyotakiwa kufanya kazi na si kama ambavyo Kibamba aliwaambia waandishi.
Kamati ya Uchaguzi iliwekewa mezani suala nyeti la matumizi mabaya ya madaraka. Ilitakiwa ilichukue suala hilo kwa uzito wake na kuiagiza sekretarieti iliwasilishe Kamati ya Maadili badala ya kuamua suala ambalo halikuwa chini ya mamlaka yake.
Kamati ya Maadili pia ilitakiwa iagize suala hilo la kimaadili liwasilishwe mezani kwake kwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ana mamlaka yote ya kuitisha jambo lolote la uvunjwaji wa maadili kama alivyofanya huko nyuma.
Wanasheria wamekaribishwa katika mpira ili wasaidie kuunyoosha mchezo kwa kutumia fani yao na si kutumia fani yao kuwaumiza wanafamilia wa mchezo wa soka. Taaluma yao ni muhimu sana katika maendeleo ya mpira wa miguu, lakini ni lazima wawe na jicho la kimpira na lengo la kutoa masuala ya michezo kwenye mahakama za kiraia.
Tafsiri hiyo ya Kibamba na wenzake ni ya mahakama za kiraia na si chombo cha haki katika soka.