KUNA KITU! Mastaa wa Ligi ya Ureno walivyonaswa na klabu za EPL

Muktasari:
- Je, Gyokeres atakuwa Islam Slimani au Bruno Fernandes? Hii hapa orodha ya mastaa walionaswa na klabu za Ligi Kuu England wakitokea kwenye timu kubwa za Ureno.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL inakaribia kwenye dili la kumsajili straika wa Sporting CP, Viktor Gyokeres.
Je, Gyokeres atakuwa Islam Slimani au Bruno Fernandes? Hii hapa orodha ya mastaa walionaswa na klabu za Ligi Kuu England wakitokea kwenye timu kubwa za Ureno.
Hii orodha inawahusu wachezaji waliotoka Ligi ya Ureno kwenda kwenye Ligi Kuu England kwa ada inayoanzia Pauni 15 milioni kwenda juu kwa mujibu wa Transfermarkt.
Wakati sasa Gyokeres akikaribia kutua Arsenal, maswali yanayoulizwa kama atakwenda kutoboa kama Fernandes alipotua Man United au kuchemsha kama Slimani, kilichomtokea Leicester City.
Kuna mastaa 30, ambao walivuka kutoka ligi ya Ureno kwenda England kwa uhamisho wa pesa nyingi.
30) Fabio Silva (Porto - Wolves, Pauni 35.6m)
Huu ni usajili ghali uliofanywa kwa makosa makubwa. Mara zote kusajili kinda kwa pesa nyingi ni kama kucheza kamari. Na sasa mchezaji huyo bado anajifunza tu huko Wolves.
29) Lazar Markovic (Benfica - Liverpool, Pauni 20m)
Liverpool ilisajili mchezaji ikiamini atakuwa bora uwanjani, lakini Markovic alishindwa kufikia malengo, huku sasa akiwa na miaka 31 hana timu baada ya kuachwa na FC Baniyas ya UAE.
28) Adrien Silva (Sporting - Leicester, Pauni 22m)
Leicester City ilifanikiwa kumsajili Adrien Silva ikiwa na matumaini makubwa, lakini staa huyo hakufunga bao lolote katika mechi 21, akatolewa kwenda Monaco hakufunga katika mechi 40.
27) Giannelli Imbula (Porto - Stoke, Pauni 18.3m)
Imbula alikuwa na kiwango bora wakati ananaswa na Stoke kutoka Porto ya Ureno kwa Pauni 18 milioni. Alikuwa akitamba kwenye eneo la kiungo, akicheza mechi 28 na kufunga mabao mawili.
26) Islam Slimani (Sporting - Leicester, Pauni 29.7m)
Slimani alifunga mabao 61 katika mechi 123 akiwa Sporting - lakini hali ilikuwa tofauti alipotua Leicester City, alifunga mara saba tu katika mechi 23 Ligi Kuu England msimu wa 2016/17.
25) Eliaquim Mangala (Porto - Man City, Pauni 32m)
Manchester City ilitoa pesa nyingi kunasa huduma ya beki wa kati Mangala, lakini kile alichokwenda kukifanya kwenye kikosi chao, walimwondoa haraka kwenye timu yao, akaondoka.
24) Darwin Nunez (Benfica - Liverpool, Pauni 85.4m)
Liverpool ilikubali kulipa Pauni 64.2 milioni kwanza kumsajili Nunez, huku wakihitajika pia kuongeza Pauni 21.2 milioni kumpata mchezaji huyo, ambaye ameshindwa kufanya jambo la maana Anfield.
23) Nico Gonzalez (Porto - Man City, Pauni 50m)
Kuna mazungumzo Nico ameondoka Man City, wakati alisajiliwa Januari tu hapo, tena kwa pesa nyingi. Mkali huyo ameshindwa kuonyesha makali ambayo yamewafanya Man City wamsajili.
22) Fabio Vieira (Porto - Arsenal, Pauni 34.2m)
Umbo la Vieira limemfanya ashindwe kutamba kwenye soka la England. Msimu uliopita alirudishwa kwa mkopo Porto na kinachoaminika kwenda kutokea atafunguliwa mlango wa kutokea Emirates.
21) Marcos Rojo (Sporting - Man United, Pauni 16m)
Rojo alikuwa mburudishaji, lakini alikuwa na kiwango kisichokuwa kibaya sana ndani ya uwanja, akipiga soka la kibabe kama ilivyo kwa Waargentina wengi, lakini si ugumu wa Lisandro Martinez.
20) Javi Garcia (Benfica - Man City, Pauni 15.8m)
Mhispaniola huyo alijiunga na Man City akitokea Benfica katika kipindi ambacho kocha Roberto Mancini aliamini angefanya jambo la maana kwenye kiungo. Alicheza mechi 76 Man City.
19) Victor Lindelof (Benfica - Man United, Pauni 39.5m)
Beki wa kati wa Sweden, Lindelof alinaswa na Man United iliyokuwa na matumaini makubwa. Kiwango chake kimekuwa cha kupanda na kushuka na mwaka huu ameachwa aondoke baada ya mkataba kuisha.
18) Jose Bosingwa (Porto - Chelsea, Pauni 16.2m)
Ni ngumu kusikia jina la Bosingwa kisha usikumbuke kile alichomfanya Yossi Benayoun na hakuonyeshwa hadi kadi ya njano. Alikuwa mchezaji aliyekuwa akikupa nyakati zote mbaya na nzuri.
17) Anderson (Porto - Man United, Pauni 20m)
Baada ya msimu wake wa kwanza Old Trafford, Anderson alishinda tuzo ya Golden Boy 2008. Alikuwa fundi wa Kibrazili, akicheza soka matata kabisa chini ya kocha Sir Alex Ferguson.
16) Matheus Nunes (Sporting - Wolves, Pauni 42.2m)
Wolves ilishinda mbio za kumsajili kiungo Nunes, aliyekuwa chini ya wakala Jorge Mendes na hakika uliokuwa usajili mzuri kwenye kikosi hicho japo si sana na aliuzwa kwa faida kwenda Man City.
15) Diogo Dalot (Porto - Man United, Pauni 19m)
Si usajili mbaya sana uliofanywa na Man United, ambako staa huyo wa Kireno amekuwa kiwapa timu hiyo machaguo mapana kwenye kikosi, akicheza pembeni kama beki, winga na wing-back.
14) Evanilson (Porto - Bournemouth, Pauni 39.5m)
Kwenye kumbadili Dominic Solanke siku zote lilikuwa jambo gumu, lakini Bournemouth iliamini Evanilson ataweza. Ni mchezaji msumbufu kwenye safu ya ushambuliaji na kuwa ingizo bora kwao.
13) Raul Jimenez (Benfica - Wolves, Pauni 30m)
Raul Jimenez alipopata majeraha ya fuvu la kichwa hili lilipunguza kiasi makali yake kwenye maisha yake ya soka huko Wolves. Kiwango chake hakikuwa kama awali, lakini bado alikuwa usajili mzuri.
12) Ricardo Pereira (Porto - Leicester, Pauni 21.8m)
Pereira hakuwa kwenye kiwango chake tangu alipopata maumivu ya goti Machi 2019. Amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha na hilo linamharibia ubora wake wa kuwa beki wa kushoto mahiri.
11) Enzo Fernandez (Benfica - Chelsea, Pauni 106.8m)
Ulikuwa usajili wa pesa nyingi, wakati kiungo Enzo Fernandez alipotua Chelsea akitokea Benfica. Amekuwa akiboresha kiwango chake msimu hadi msimu, huku sasa akitamba na kipa Enzo Maresca.
10) Pedro Porro (Sporting - Tottenham, Pauni 39.7m)
Tottenham Hotspur ililipa pesa ya kutosha kunasa saini ya beki Porro na hakika amekuwa na kiwango bora kwenye timu hiyo tangu kocha Antonio Conte, Ange Postecoglou na sasa kocha Thomas Frank.
9) Ramires (Benfica - Chelsea, Pauni 18.2m)
Benfica imekuwa ikifanya dili nyingi na Chelsea na moja ya hilo ni usajili wa kiungo wa Kibrazili, Ramires, ambaye alikwenda kuwa moto huko Stamford Bridge akibeba mataji kibao.
8) David Luiz (Benfica - Chelsea, Pauni 21.3m)
Chelsea imekuwa hodari kwa kusajili wachezaji wenye vipaji wanaotamba kwenye ligi ya Ureno. David Luiz alicheza kwa awamu mbili Chelsea, lakini ni moja ya wachezaji waliofanya vizuri Stamford Bridge.
7) Luis Diaz (Porto - Liverpool, Pauni 49m)
Kwa sasa anasakwa na Barcelona na Bayern Munich, lakini Liverpool inasita kumuuza mchezaji ambaye amekuwa na kasheshe zito kwa wachezaji wa timu pinzani anapokuwa uwanjani.
6) Joao Palhinha (Sporting - Fulham, Pauni 20m)
Kile ambacho alikifanya kiungo Joao Palhinha huko Craven Cottage kilikuwa cha viwango bora sana akiitumikia Fulham, jambo lililomfanya apate dili la kibabe la kwenda kujiunga na Bayern Munich.
5) Ederson (Benfica - Man City, Pauni 34.7m)
Baada ya kumwondoa kipa Joe Hart, kocha Pep Guardiola alimsajili Claudio Bravo kabla ya kumwondoa na kwenda kuvamia kwenye ligi ya Ureno kumsajili kipa wa boli, Mbrazili Ederson.
4) Ricardo Carvalho (Porto - Chelsea, Pauni 19.85m)
Wakati Jose Mourinho alipojiunga Chelsea kutokea Porto baada ya kuwapa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, aliandamana na wachezaji wake wachache, akiwamo beki wa kati, Ricardo Carvalho.
3) Nemanja Matic (Benfica - Chelsea, Pauni 21m)
Chelsea mara ya kwanza ilimsajili Matic kutoka MFK Kosice ya Slovakia, kisha ikamuuza kwenda Benfica kabla ya kumsajili tena kwa pesa nyingi ili kuwapa mataji ya kutosha huko Stamford Bridge.
2) Bruno Fernandes (Sporting - Man United, Pauni 74m)
Kwenye usajili wa kiungo staa Bruno Fernandes, Man United ililipa Pauni 47 milioni kwanza, kisha nyongeza ya Pauni 20.7 milioni kutokana na ubora wa staa huyo wa Kireno uwanjani. Ndiye nahodha.
1) Ruben Dias (Benfica - Man City, Pauni 65m)
Man City ilitanguliza Pauni 62 milioni kwanza kumnasa beki Ruben Dias, kisha baadaye iliongeza Pauni 3 milioni baada ya huduma matata ya staa huyo wa Ureno. Kiwango chake hakina mashaka.