Hakimu sahihi wa Jonas Mkude ni umri na muda

Tuesday January 05 2021
mkude pic

KIUNGO mmoja wa zamani wa Yanga na Taifa Stars hakuwa na nidhamu. Siku moja nikaandika makala ndefu kama hii na kuchambua tabia zake za ovyo. Wapambe zake wakamuonyesha. Akanipigia simu akiwa na hasira. “Kwa nini umenishambulia?”

Nikamjibu kwa urahisi tu. “Hauna nidhamu. Unajiona staa kwa sasa lakini mpira una muda wake. Mimi na kazi yangu hii ya uandishi ninaweza kuandika hata nikiwa na miaka 65 huku nikikusanya visenti. Mchezaji ukiwa na miaka 34 unaitwa mzee. Na kama haujajipanga utafulia tu.”

Maisha yamekwenda kama nilivyofikiria. Kwa sasa ni kitu cha kawaida kwa yule staa wetu wa zamani kunipigia simu kuniomba shilingi elfu kumi. Kwa sasa akiniona amenipachika jina la ‘tajiri’. Nacheka sana. Umri wangu ni mkubwa kuliko wake lakini mimi bado nipo kazini. Yeye alipochokwa na timu kubwa alijaribu kubahatisha hapa na pale lakini mpira umemshinda. Mambo yamekuwa magumu.

Hakuna raha kubwa kama kuwa staa wa Simba au Yanga. Hasa ukiwa mchezaji mzawa. Dunia unaiweka mkononi. Unapendwa na kila shabiki. Unapendwa na kila kiongozi. Unaringa. Unadeka. Unafanya unachojisikia. Wageni wengi hawapo hivi. Wanajua hapa sio kwao. Wamekuja kusaka noti.

Hawa wa nyumbani wanasikia raha zaidi. upo nyumbani. Una pesa. Unapendwa. Kila unapopita unaitwa jina lako. Kuna hisia tamu zaidi ya hizi? Hakuna. Tatizo kazi wanayoifanya ni ngumu. Kazi ya kutumia nguvu za mwili na akili.

Unahitaji kujitunza kimwili, kisha kujitunza kiakili. Wachezaji wetu wanashindwa kufanya vyote hivi viwili. Wanashindwa kuelewa kwamba wapo katika kazi ya kitumwa. Kazi ya muda mfupi ambayo nyakati zako zikipita watu wanakusahau.

Advertisement

Hizi ndizo nyakati ambazo anapitia kiungo wa Simba, Jonas Mkude. Staa wa klabu yake, staa wa timu ya taifa. Staa mkubwa. Ni nyakati ambazo anashindwa hata kukukumbuka kwamba Hamis Gaga alipitia, Athuman China alipitia, Issa Athuman alipitia, Athuman Idd ‘Chuji’ alipitia. Wengineo kibao walipitia.

Bonde hili la mauti linawaacha wachache wakiwa na nidhamu nzuri. Wengi wanaangukia kuwa na nidhamu mbovu. Jonas amejichagulia hili la nidhamu mbovu. Anashindwa kutabiri hali ya hewa inayokuja. Naambiwa anawasumbua Simba kwelikweli. Katika hili la majuzi hata wachezaji wenzake wamechukia.

Mambo ya kumkumbusha ni haya hapa. Kwanza kabisa soka ni mchezo wa kazi ya muda mfupi. Ndani ya muda huo huo inabidi ukusanye kilicho chako kwa ajili ya kujiandalia maisha mazuri marefu ya siku za usoni.

Bahati mbaya kwa wanasoka wengi duniani ni kwamba vipindi wanavyotumia kucheza soka ndivyo vipindi ambavyo walitakiwa kuwa shule. Hawa kina Lionel Messi hawajaenda shule. Wameyatoa maisha yao katika soka tu na ndio maana wanaitwa wanasoka wa kulipwa (professional footballers).

Wachezaji wengi wa kulipwa huwa hawachezei maisha yao kwa sababu wanajua wana muda mchache wa kukusanya pesa na hata muda huo ukiisha wanajikuta hawana mambo mengi ya kufanya kwa sababu hawakwenda shule. Inabidi wasimamie miradi yao. Wachache wanaangukia kuwa makocha au wachambuzi.

Sijui kama Mkude ana digrii au diploma. Lakini hata kama anavyo hivi vitu basi awaulize vijana jinsi ambavyo wanateseka na bahasha za kaki kusaka ajira hapa mjini. Wanatembea mpaka soli za viatu zinachubuka. Lakini pia tumuulize Jonas, kama hana elimu ataweza kurudi shule? Sidhani. Hapa ndipo wanaposoka wa kulipwa hawataki kabisa kuchezea maisha yao. Wanapambana kweli kweli. Jiulize mchezaji kama Saido Ntibanzokiza alivyocheza hadi Ligi Kuu ya Ufaransa lakini leo anaendelea kukusanya noti chache zilizobaki katika maisha yake ya soka akicheza pale Jangwani.

mkude pic 2

Unaachana na jambo hilo. Jambo jingine la kumkumbusha Mkude ni namna ambavyo kazi hii ya mpira ilivyokuwa kazi ya kitumwa. Mastaa wanakusanya pesa nyingi lakini wanafanya kazi ya kitumwa kwelikweli. Wao ni burudani ya watu. Wao inabidi wateseke ili watu wafurahi. Kwa mfano ilivyo sasa pale England. Kilikuwa kipindi cha Krismasi na Mwaka mpya. wachezaji walikuwa wanateseka katika barafu wakicheza ili sisi tupate burudani. Hatujajali kama inabidi wawe nyumbani wanakula pilau na familia zao, hapana. Desemba 26 walikuwa nyumbani wakati sisi tulilala hoi Desemba 25. Wao hawakupaswa kulewa wala kula ovyo.

Haya ni maisha ya kawaida kwa wanasoka. Huwa wanapata nafasi ya kupumzika vema wakati wakishastaafu. Hapa ndipo wanapoanza kunenepa vizuri. Vinginevyo akina Mkude hawana muda mwingi wa kula raha. Wanafanya kazi za kitumwa ili mashabiki wafurahi.

Wanasheria, Walimu, Waandishi wa habari, wakandarasi na watu wa taaluma nyingine wana muda mzuri wa kupumua wikiendi au katika sikukuu lakini sio wachezaji. kama Jonas na masala wenzake waliamua kuingia katika kazi hii basi lazima wajitoe mhanga.

Kitu cha mwisho cha kumkumbusha Mkude na masala wenzake ni hiki hapa. Kazi yao kwa hapa nchini ina utamu mwingi wakati unacheza. Wakati huo unacheza unaweza kudhani kwamba kuna mastaa hawakuwahi kupendwa kabla yako.

mude pic 3

Jonas hajawahi kupendwa kuliko Gaga wala Hussein Marsha. Hajawahi kupendwa kuliko Nicodemus Njohole wala Michael Paul. Hajawahi kupendwa kuliko viungo zaidi ya hamsini ninaowafahamu ambao waliwahi kuvaa jezi nyekundu na nyeupe pale Msimbazi.

Hata hivyo nani anawazungumzia hao wachezaji kwa sasa? Zama zao zimepita. Zama zikipita hakuna anayekukumbuka. Hakuna anayekutazama mara mbili usoni. Waulize wachezaji wa zamani waliong’ara zamani jinsi ambavyo wanakwepwa na mashabiki kwa sasa. Nakumbusha tu kwamba mashabiki wenyewe hawana adabu kabisa.

Pale baa za nje ya uwanja wa taifa tunakaa na wachezaji wengi wa zamani ambao watu hawataki kuwatazama usoni mara mbili. Wanahisi watawaomba hela. Lakini enzi zao walipendwa katika hizi timu za Kariakoo kuliko Mkude, kuliko Nzitanzokinza, kuliko Meddie Kagere, kuliko mchezaji yeyote ambaye unadhani anapendwa kwa sasa.

Kama ilivyotokea kwa rafiki yangu staa wa zamani wa timu ya taifa aliyenipigia simu kwa hasira na sasa ananiomba shilingi elfu kumi nimegundua kwamba tatizo la mastaa wetu wanaong’ara na kusumbua kambini ni muda tu. Klabu ziweke misingi yake lakini zisijishughulishe nao sana. Zisiteseka sana na nidhamu zao. Muda ukifika watatia adabu tu. Wakati huo atakuwa anapendwa staa mpya ambaye kwa sasa si ajabu anacheza mchangani Kisarawe au Newala.

..........................

Imeandikwa na EDO KUMWEMBE

Advertisement