GSM alivyotingisha ufalme wa Mo Dewji

Friday June 17 2022
GSM pic
By Khatimu Naheka

MASHABIKI wa Yanga wako kwenye kilele cha furaha msimu huu na ukijaribu kuwagusa utasikia “sisi mabingwa wapya”, ukiendelea watakwambia “hatujapoteza taji lolote”, ukijifanya mbishi kama wewe ni Simba watakumalizia kwamba “msimu huu tumekufunga na hupati taji lolote.”

Jeuri hiyo ipo Yanga, lakini kwa upande wa pili wao Simba maisha yamebadilika kuna hali haijatulia kidogo wakiwa hawana msimu mzuri na sasa wanapambana kusuka upya timu yao.

Kumbuka Simba imetamba kwa misimu minne wakiinyanyasa Yanga, ila ikiwa na matokeo mazuri katika mashindano ya Afrika. Hali hii ikaifanya Yanga msimu kuja kwa nguvu zaidi. Nyakati nzuri za Simba katika miaka minne ilijivunia fedha na nguvu ya mwekezaji wao Mohamed ‘MO’ Dewji ambaye fedha na uongozi wake viliifanya Simba itambe na Yanga nao wakamleta mfadhili wao Ghalib Said Mohamed ‘GSM’.

GSM katika miaka yake miwili tu ikatosha kabisa kumaliza ubabe wa MO na jamaa amemvuruga mwenzake namna hii na kuifanya Yanga kurudi juu huku Simba kukiwa na vurugu nyingi.


MATAJI MATATU SIMBA

Advertisement

Yanga msimu uliopita ilikaribia kuchukua taji la ligi ikashindwa, ikafika fainali ya FA ikalikosa kombe ikipoteza kwa Simba. Lakini, msimu huu kuna dalili ya kuchukua mataji matatu - tena yote yakitokea kwa watani wao.

Yanga ilishaichapa Simba katika Ngao ya Jamii ikachukua taji hilo, ikaja na gia ya ajabu kwenye ligi jana ilikuwa ikivaana na Coastal Union na kama imepata matokeo ya ushindi, basi itakuwa imelibeba taji hilo lililoshikiliwa na Wekundu wa Msimbazi kwa misimu minne mfululizo.

Ikitoka hapo itaenda kukutana tena na Coastal Union katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kama itashinda tena italikomba taji hilo lililoshikiliwa kwa misimu miwili na Simba.

Yanga waliimaliza kabisa Simba wakiihakikishia patupu baada ya kuichapa katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA na sasa kama wataichapa Coastal Union kwenye fainali hiyo, basi watakuwa wamechukua yote. Hii ni nguvu ya GSM.


YANGA MECHI KIBAO

Yanga ikiwa inatambia fedha za GSM msimu huu imewaachia Simba pointi nne pekee kufuatia suluhu mbili kwenye ligi, lakini imeichapa Simba katika fainali ya Ngao ya Jamii. Pia majuzi ikaichapa kwenye nusu fainali ya ASFC na kuwanyima hata taji la kufutia machozi Wekundu pale CCM Kirumba.

Hata hivyo, GSM tangu aanze kuifadhili Yanga ameshinda mechi nyingi dhidi ya Simba ya MO - Wekundu wameshinda mechi mbili wakati Yanga ikishinda mechi nne wakitoa sare tatu.


KILELENI DAIMA

Kama kuna kitu Yanga imeifanyia unyama Simba, basi ni kwamba Wekundu hao msimu huu hawajafanikiwa kuongoza ligi hata kwa sekunde moja wakizidiwa hata na Polisi Tanzania.

Hapa lazima Yanga wazishukuru fedha za GSM ambapo baada ya kufanya usajili mzuri ulioleta mastaa wa nguvu kikosini walifanikiwa kuanza kuongoza ligi tangu Oktoba 27 wakiwa na michezo mitatu tu wakichukua usukani kutoka kwa Polisi Tanzania.

Tangu Yanga ipande juu haijawahi kutingishwa na yoyote mpaka inakwenda kuchukua taji, jambo ambalo lilionyesha utofauti wa ubora wa kikosi ukilinganisha na watani wao, Simba.


YANGA HAIJAPOTEZA

Jeuri ya kikosi cha maana iliifanya Yanga mpaka sasa kuwa klabu pekee ambayo haijafungwa kwenye ligi na matokeo yao mabaya yakiwa sare, ikiwa nazo saba wakati Simba ina sare tisa, lakini kibaya ikiwa imeshapoteza mechi mbili mpaka ligi ilipofikia.


JEURI YA FEDHA

Baada ya Simba kuinyanyasa Yanga kifedha kwa kuizidi kete kwenye usajili wa kiungo Rally Bwalya miaka miwili iliyopita, Luis Miquissone, beki Henock Inonga na Bernard Morrison Yanga imejibu ikiwabeba beki Djuma Shaban, Fiston Mayele, Bakar Mwamnyeto, Khalid Aucho na sasa Stephan Aziz KI. Hawa ni mastaa ambao wanakwenda kuendelea kuipa Yanga thamani ya ubora uwanjani msimu huu na hata msimu uliopita.

Kuna uwezekano mkubwa pia yanga wakamrudisha winga wao wa zamani, Bernard Morrison msimu ujao ikikumbukwa kwamba Mghana huyo alichukuliwa na Simba akitokea Yanga.

Ukiacha matukio ya kinidhamu mchezaji huyo ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo mkubwa anapokuwa uwanjani akiwasaidia Wekundu wa Msimbazi kufanya vizuri msimu uliopita.


DENI LIPO HAPA

Kutamba huko kwa GSM hata hivyo anabakisha deni moja tu kubwa kwa MO ambalo ni kuhakikisha sasa Yanga inatamba pia katika mashindano makubwa ya Afrika ambako Wekundu wa Msimbazi wamekuwa na mafanikio zaidi uwanjani.

Simba katika miaka minne ikiwa chini ya MO imefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali mara mbili na pia hatua ya makundi wakiizoea huku Yanga chini ya GSM ilipojaribu msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa ilitolewa hatua ya kwanza, ilhali msimu ujao ikitarajiwa kurudi tena kujiuliza.

Advertisement