GRACE: Kukosa wapinzani kulivyompa ulaji jeshini

Muktasari:
- Keko ilikuwa maarufu miaka 1980 hadi 1990 kutokana na uwepo wa familia ya Mzee Matumla iliyojawa vipawa lukuki vya ngumi za ridhaa na baadaye za kulipwa.
HISTORIA ya Kitongoji cha Keko Magurumbasi, jijini Dar es Salaam na mchezo wa ngumi itaendelea kuishi milele.
Keko ilikuwa maarufu miaka 1980 hadi 1990 kutokana na uwepo wa familia ya Mzee Matumla iliyojawa vipawa lukuki vya ngumi za ridhaa na baadaye za kulipwa.
Kuanzia Rashid Matumla, Mkwanda Matumla, Hassan Matumla na Bwana Matumla kwa nyakati tofauti na waliifanya Keko kutambulika kama kitovu cha mchezo huo.
Grace Mwakamele asili yake ni kutoka Jiji la Mbeya, lakini amekulia mitaa hiyo ya Keko Magurumbasi, kitongoji maarufu zaidi Dar es Salaam kutokana na uwepo wa bingwa wa zamani wa mchezo huo, Rashid Matumla ‘Snake Boy’.
Wakati Rashid anastaafu mchezo huo, Mwamakele alikuwa binti mdogo akijitafuta na anasema hajawahi kufirikia atafika aliko sasa.
Ni mwajiriwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ‘JWTZ’ akiwa na cheo cha Koplo. Eneo lake la kazi ni kamandi ya Jeshi la Kujenga Taifa ‘JKT’ Mgulani 831 KJ.

SAFARI YAKE HADI JESHINI
Anaeleza namna safari yake katika mchezo huo ilipoanzia akiwa nyumbani kwao mitaa ya Keko ambayo kwa kiasi kidogo anaendesha shughuli za ujasiriamali kwa lengo kuongeza kipato chake licha kazi yake jeshi.
Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 14 katika ngumi za kulipwa ambayo sawa na raundi 70, ameshinda 10 kati ya hayo saba ni kwa Knockout na amepoteza mapambano manne kati ya hayo mawili ni kwa Knockout.
Amejaliwa uwezo wa kushinda mapambano yake kwa asilimia 70 ya Knockout kutokana na nguvu yake ya asili, huku katika upande wa ngumi za ridhaa rekodi inaonyesha amepigana mara moja dhidi ya bingwa wa Olimpiki mwaka huu Ufaransa, Iman Khaleif alilopoteza kwa mwamuzi kusimamisha pambano RSC.
Anashikilia rekodi ya kuwa bondia wa kwanza wa kike nchini tangu Tanganyika ipate Uhuru kupata medali ya fedha kabla ya kushinda tuzo ya mwanamichezo bora wa kike kwa mwaka 2023.
ALIVYOINGIA KWENYE NGUMI
Mwakamele anasema safari yake katika mchezo huo imechangiwa pakubwa na bondia mkongwe, Fredy Sayuni aliyekutana naye mara ya kwanza akiwa barabarani akifanya mazoezi peke yake na kumshawishi kuingia kwenye mchezo huo.
“Mtu wa kwanza kunishawishi kuingia kwenye ngumi mwaka 2012 ni Fredy Sayuni. Ni bondia wa zamani wakati huo alikuwa na Gym yake karibu na Magereza Keko. Alinikuta njiani nafanya mazoezi mwenyewe, akaniomba niende kwenye gym yake.
“Wakati naenda kufanya mazoezi kwenye Gym yake, ndiyo nilikutana na bondia Ayubu Mwansasu aliyekuwa akifanya mazoezi kwake ila sasa Ayubu ni kocha wa JKT Mgulani upande wa ngumi.”

ATUA JESHINI, ABEBA DHAHABU
“Ayubu ndiye alinishawishi kwenda kufanya mazoezi pale JKT wakati huo sijui kama nitakuja kuwa askari, nashukuru JKT nikawa nafanya vizuri hadi mwaka 2014 nilipata nafasi ya kufanya mafunzo ya kwanza ya Jeshi la Kujenga Taifa ila nikarudishwa tena Mgulani nikawa naendelea na ngumi.
“Lakini mwaka 2015, nikapata kozi rasmi ya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania na baada kumaliza kozi yangu nilishiriki mashindano ya wazi ya ngumi za ridhaa yaliyofanyika Ilala kwenye Ukumbi wa Panandipanandi, nilicheza na bondia anaitwa Sara Andrew.
“Nikashiriki mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki yaliyofanyika nchini na nilishinda medali ya dhahabu.
ATUA NGUMI ZA KULIPWA
Nini kilisababisha ukaingia kwenye ngumi za kulipwa kutoka ngumi za ridhaa?
“Unajua nilitoka kule siyo kwa sababu labda muda wangu wa kucheza ngumi za ridhaa umeisha, hapana ila nilikuwa napata changamoto ya upande wa wapinzani wa kucheza nao hawakuwepo kabisa.
“Kuna wakati yalifika mapambano matano wapinzani wanakimbia yaani nafanya mazoezi halafu sipigani, ndiyo klabu yangu pamoja na Meja Seleman Semunyu (promota wa ngumi za kulipwa) ilibidi waniombee nicheze ngumi za kulipwa.
“Wakati naingia kwenye ngumi za kulipwa nilitakiwa nipande ulingoni kwenye pambano la Queen of the Ring mwaka 2021 ila kwa bahati mbaya nikakosa mpinzani.
“Nikaja kupata nafasi kwenye pambano lingine lililofanyika Kinesi na nilipigana na Ridia Mdethele ambaye nilimpiga kwa Knockout ya raundi ya pili lakini mwaka huohuo nikapigana na Asha Ngedere yeye nilimpiga kwa pointi Morogoro.
“Nashukuru Mungu nikaendelea kupata mapambano mengine kabla ya kuwekewa pambano la mkanda wa ubingwa wa PST ambao pambano nilipoteza kwa pointi dhidi ya Ruth Chisale kutoka Malawi.
“Kiukweli niliumia kupoteza lile pambano la mkanda wa ubingwa kwa sababu sikutegemea kama ningepoteza lakini nakiri mpinzani wangu kuna maeneo alinizidi mbinu.

MTAKA TENA CHISALE
“Lakini kwa upande wangu bado nina ndoto ya kurudiana naye kwa sababu nataka kuonyesha sikustahili matokeo yake na kuna wakati tulitaka kurudiana ila mpinzani akawa na dharura ya uzazi.”
ARUDI NA MEDALI YA KWANZA AFRIKA
Ilikuwaje ulipata nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika na kurudi na medali kama bondia wa kwanza wa kike nchini?
“Unajua kwanza, sheria zimebadilika yaani sasa naweza kupigana ngumi za kulipwa na ngumi za ridhaa na hasa ikiwa upande wa kimataifa naruhusiwa japo kuwa pia inapoelekea hata ndani tunaweza tukacheza kwa sheria zinaendelea kubadilika.
“Sasa nafasi ya kucheza hayo mashindano ilitokana na sheria, nilienda kama bondia wa semi pro kupitia timu ya taifa ya ngumi na safari haikuwa rahisi kabisa kwa sababu katika mashindano yale yaliyofanyika Cameroon nilianzia hatua ya robo fainali.
“Nilianzia hatua hiyo kwa sababu mpinzani alikuja lakini tatizo alikuwa amezidi kilo, nikapewa ushindi wa Walkover.”
“Nikaingia nusu, nikapewa Msenegal, alikuwa mrefu na alinisumbua raundi ya kwanza lakin raundi ya pili na tatu nilimsumbua kwa kumpiga na ndiyo nikamshinda.
“Lakini pambano langu la fainali ndiyo nilipoteza kwa bondia wa Msumbiji ambaye ni bingwa wa dunia katika uzani wa 67 Super walter, nikashinda medali ya fedha yeye akashinda dhahabu kwa sababu alikuwa mshindi wa kwanza.
Uzito wa rekodi uliyoweka inaendana na heshima ya taifa uliyoweka?
“Unajua hii ni medali ya kwanza katika mchezo wa ngumi za ridhaa upande wa wanawake tangu nchi ipate uhuru ila linapokuja suala la uzito binafsi sijaliona.
“Pongezi zilikuwa nyingi kutoka mataifa ya nje hata kuliko ndani, nilipokea pongezi za kutoka Uingereza na Wakenya wengi walinipongeza.
“Nilitegemea kupata mapokezi makubwa lakini haikuwa hivyo, siku tuliyorejea kutoka Cameroon maana medali zilikuwa mbili mimi na Yusuph Changalawe lakini mapokezi yakawa ni kawaida.
Unadhani atatokea bondia wa kike kuvunja rekodi yako?
“Inawezekana mtu akatokea na akaweza kuivunja au mimi mwenyewe kwa sababu ndoto yangu ni kuona nachukua medali ya dhahabu kwa kuvunja rekodi ambayo nimeweka sasa.

Unahisi nini kifanyike kutokana na ukubwa wa medali yako?
“Binafsi nilitamani kumpelekea medali, Rais wangu Daktari Samia Suluhu Hassan kwa sababu yeye mwanamke na mimi nimekuwa bondia wa kwanza wa kike kuleta medali kubwa ya kimataifa kupitia ngumi.
“Hii kwangu imekuwa kama kidonda, bado natamani kuona zawadi hii ya medali inafika kwake.
“Lakini nje ya maombi yangu ya medali kumpelekea mama, tulipokea salamu za serikali kupitia Waziri Mkuu pamoja siku ya Uhuru wa watu wa India, walitupongeza.
Ulitegemea kushinda tuzo ya mwanamichezo bora wa kike kwa mwaka 2023?
“Ulikuwa ukiniuliza nani anastahili, kwangu nilikuwa namwona yule mchezaji wa soka, Opa Clement na hata siku ambayo tunaenda ukumbini pale Masaki, niliulizwa na waandishi nilimtaja Opa tena nilimwambia hata mwamuzi Pendo Njau ambaye alikuwa mshiriki mwezangu.
“Lakini ndani nilitangazwa mshindi wa jumla na nikachukua tuzo, naishukuru kamati ya tuzo ya Baraza la Michezo la Taifa kwa kuona nastahili.
Uliwahi kufikiri kukutana na waziri Mkuu?
“Kitendo cha yeye kunikabidhi tuzo kwangu ilikuwa ni ‘suprise’, sikutegemea, ilinijia hofu na nililia kwa furaha, nakumbuka maneno yake alisema serikali ipo pamoja na mimi akanipongeza.”
“Lakini heshima yangu imeongezeka katika mitaa ambayo natokea maana siku ile watu Keko hawakulala walifunga muziki wakafanya pati ya kunipongeza.
“Watu wengi wa Keko kwangu ni nguzo, wamekuwa wakiniunga mkono Keko Furniture wamekuwa na mimi sambamba mtaani kwangu kama kijana mwenzao, nawashukuru.
Maisha nje ya ngumi yapoje?
“Maisha nje ya ngumi kiukweli nimekuwa mtu wa watu najivunia hilo ambalo limetokana na msingi mzuri ambao nimejengewa na wakuu wangu.
“Namshukuru sana Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa majeshi na mkuu wa JKT, kurugenzi ya michezo na mkuu wa kambi ya Mgulani 831KJ kwa sapoti kubwa wanayonipa katika utendaji wangu.
Ipi changamoto kubwa unayokutana nayo?
“Tatizo kubwa ambalo lipo katika mchezo wa ngumi hasa sisi mabondia wa kike hatupewi kipaumbele cha mapambano ya kupigana mara kwa mara tofauti na wanaume, naomba mapromota na viongozi wa mchezo waliangalie hili jambo kwa mapana, vipaji vinakufa,” anasema.