Geay: Nilikimbia kilomita 45 kwa saa mbili

KATIKA toleo la jana, tuliona maisha ya mwanariadha Geay jinsi yalivyo, tuliona jinsi ambavyo aliweza kutoka kijijini kwao na kujichimbia kwenye Uwanja wa Ilboru ambao anautaja kama uwanja bora zaidi kwa wanariadha.
Lakini tuliona pia maandalizi yake kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi na alitufundisha kuwa yeye kule siyo jambo la ratiba kama wengi wanavyofanya kula asubuhi mchana na usiku, bali mara nyingi amekuwa akila kutokana na jinsi anavyosikia njaa.
Amesema kwake ni kawaida kula hata mara tano kwa siku moja, kutegemea na jinsi atakavyosikia njaa kwa siku hiyo, huku pia akieleza jinsi ambavyo mwanariadha Fabian Joseph alivyomvutia kuingia kwenye mchezo huu.
Leo tunaendelea, Geay ni kati ya wanariadha wenye rekodi kubwa hapa nchini, lakini akitajwa pia kuwa mmoja kati ya wanariadha matajiri kutokana na mkwanja ambao amekuwa akiukusanya kwenye mbio mbalimbali ambazo amekuwa akialikwa, kwenye mazungumzo yetu huko mbele amezungumza jinsi ambavyo amekuwa akiingiza fedha kutokana na mchezo huu.
VIPI KUHUSU MASHINDANO YA OLIMPIKI
Geay anasema alishiriki mashindano makubwa ya Olimpiki mwaka 2021, ikiwa ni ndoto yake ya kwanza ambayo alikuwa amejiwekea lakini anasema kuwa haukuwa mwaka mzuri kwake kwa kuwa alipata majeraha wakati wa maandalizi.
“Ukweli ndoto yangu kubwa ilikuwa kushiriki mashindano ya Olimpiki, siyo kushiriki tu bali kuhakikisha kuwa nafanya vizuri, nilipata nafasi hiyo mwaka 2021 na nilitamani sana kuhakikisha nafanya vizuri kwenye mashindano haya ambayo yalifanyika Tokyo Japan.
“Lakini kwangu hali ilikuwa tofauti wakati najiandaa na mashindano haya nilipata majeraha na hivyo sikuweza kufanya vizuri kule kwa kuwa nakumbuka hata sikumaliza, lakini nataka kukuhakikishia kuwa ninajiandaa vizuri kwa ajili ya Olimpiki ijayo, kama sikutakuwa na majeraha au shida yoyote nitahakikisha nafanya mambo makubwa sana.
“Unajua kikubwa hapa ni maandalizi tu kama nitajiandaa vizuri naamini nitakuwa kwenye wakati mzuri sana.
VIPI KUHUSU MEDALI, UNAZO NGAPI?
“Unajua mara nyingi kwangu naamini medali ni zile ambazo unashindana kwenye mashindano makubwa kama Olimpiki hizo mimi sina, medali nilizonazo nyingi ni zile ambazo nimeshinda zile za mialiko, lakini nakuhakikishia nina matarajio ya kutwaa medali nyingi huko mbele.
“Mashindano mengi nimeshiriki, mfano mwaka 2014 nilishiriki African Junior Championships nikashika nafasi ya nne, mwaka 2017 nilishikiri World Cross Country Championships na kushika nafasi ya 22, mwaka 2017 , World Championships nilishiriki mara mbili, sijafanya vizuri sana lakini naamini huko mbele, nitajipanga vizuri lakini pia mwaka huu niliweka rekodi ya kushika nafasi ya pili kwenye Boston ambayo nafikiri wengi walianza kunifuatilia kuanzia pale.
MAANDALIZI YA BOSTON YALIKUWAJE?
Geay ambaye amekuwa akitajwa kama mwanariadha mkimya sana, amesema wakati anajiandaa na mbio za Boston ambazo alishika nafasi ya pili alifanya maandalizi mazuri chini ya kocha wangu.
“Niliamini kuwa Boston ni mbio kubwa, na nilijiandaa vizuri, kule nilikuwa nakimbia kilomita 42, nikiwa najiandaa nilikuwa nakimbia kilomita 45 au 48 ndani ya miezi mitatu ya mwisho. Lakini nisishuke chini ya masaa mawili na dakika 59 na kukimbia hapa natumia mwendo wa kati siyo kama ule wa kwenye riadha.
“Unajua kwenye riadha lazima ulinde sana muda ambao unataka kuutumia kwenye mashindano, baada ya kuona nimeshika nafasi ya pili nilifurahi, unajua niliona kuwa naweza kushika nafasi ya kwanza hapo mbele, malengo yangu wakati najiandaa nilitaka nisitoke kwenye tatu bora na niliona kama jambo hilo linaweza kutumia.
KWANINI ALIONGOZA MUDA MREFU, AKASHINDWA MWISHONI
Geay anasema kwenye mbio zile aliongoza kwa muda mrefu na wengi waliamini kuwa anaweza kushika nafasi ya kwanza, lakini mwishoni akapitwa na Evans Chebet na kushika nafasi ya pili.
“Unajua riadha ni ishu nyingine, kuna siku tutaongea zaidi, lakini elewa kwamba huku nilikuwa na tageti zangu, ya kwanza nimalize ya kwanza ya pili nimalize wa pili na mwisho nimalize wa tatu, hivyo ikatokea ile ya pili ambayo hakika namshukuru Mungu, naamini kuna siku nitashika ya kwanza.
HUWA ANAZUNGUMZA NA ELIUD KIPCHOGE?
Geay anasema jinsi mwanariadha huyo wa Kenya anavyojiweka ni ngumu yeye kuzungumza naye, lakini kwa kuwa pia wamejenga kama upinzani huwa siyo watu wa kukutana na kuzungumza na wala haoni kama ni ishu.
“Jamaa nilimshinda kwenye Boston, jinsi anavyojiweka ni ngumu sana kwangu kukaa na kuongea naye, namheshimu kwa kuwa ni mwanariadha mkubwa, lakini huyu ni mpinzani wangu hivyo ni vizuri tu kila mtu akaendelea na maandalizi yake.
“Sisi sasa hivi riadha kwetu imekuwa kwa kasi kubwa, naamini hapo mbele bado tunaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa, lakini jambo kubwa ni wadau nao kutusaidia.
“Kuna mambo mengi ambayo wanaweza kuyafanya tukawa bora zaidi kulikuwa kutuacha hivihivi, hii ni kazi ya pamoja, tukifanya kwa juhudi basi tutakuwa bora.