Furuzi aeleza maisha chini ya makipa wakali Simba

Muktasari:
- Mwanaspoti lilifanya mahojiano na Feruzi akaeleza maisha ndani ya Simba ukiwa ni mwaka wake wa saba tangu alipojiunga na kikosi B mwaka 2019 akitokea Mbagala Market FC, na kupandishwa kikosi cha wakubwa 2021.
ILIHITAJI uvumilivu na utulivu kwa kipa wa Simba, Ahmad Feruzi Teru (22), kujifunza chini ya makipa wazoefu anaocheza nao katika kikosi hicho na sasa anaona yupo tayari kuonyesha kipaji chake kwa ukubwa.
Mwanaspoti lilifanya mahojiano na Feruzi akaeleza maisha ndani ya Simba ukiwa ni mwaka wake wa saba tangu alipojiunga na kikosi B mwaka 2019 akitokea Mbagala Market FC, na kupandishwa kikosi cha wakubwa 2021.
Feruzi anasema sio jambo rahisi kuishi na kutazama wengine wakicheza, kwani kuna muda alitamani angalau apewe mechi za Ligi Kuu Bara kudaka, lakini haikuwezekana kutokana na uwepo wa makipa wazoefu waliopo kwenye fomu.
“Haikuwa rahisi kupenya katikati ya kaka zangu ambao ni Beno Kakolanya, Aishi Manula, Moussa Camara, Ayoub Lakred, Hussein Abel na Ally Salim, kitu kilichokuwa kinanipa moyo wao wenyewe walinipa moyo na kunisisitiza niendelee kujituma na kujifunza, itafika siku yangu nitacheza na kuaminiwa,” anasema.
“Nilijifunza uvumilivu kutoka kwa Salim ambaye alipandishwa kama mimi. Ilimchukua muda mrefu hadi kuanza kupewa nafasi ya kucheza na alikuwa ananiambia nina uwezo nisichoke mbeleni kuna kitu kizuri kinakuja kwa ajili yangu.
“Vipo vitu vingi ambavyo nimejifunza kwao mfano Camara ni kipa ambaye ana uamuzi wa haraka anafanya hivyo kuanzia mazoezini hadi mechi za mashindano, ndio maana anakuwa anaokoa hatari nyingi. Kuhusu Manula ana sifa nyingi siwezi kusimulia moja baada ya nyingine.”
Anapoulizwa hajawahi kuonja mechi ya mashindano tangu apandishwe kikosi cha wakubwa 2021 inampa picha gani?
Feruzi anajibu: “Nilicheza Kombe la FA, mechi za kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan na niliingia kipindi cha pili dhidi ya Asante Kotoko.”

ALICHOJIFUNZA HIKI HAPA
Kipa huyo anasema yapo mambo mengi aliyojifunza muda wote aliokaa Simba, na anaona ni muda mwafaka wa kwenda kuyafanya kwa vitendo ili kuona kama anafiti kiwango chake kizidi kukua na tayari kuna timu zimepeleka ofa Msimbazi.
“Baada ya kupandishwa mwaka 2021 nilisaini miaka mitano lengo lilikuwa ni kupata muda wa kuendelea kujifunza zaidi, hivyo mkataba wangu unaisha mwaka 2026,” anasema mchezaji huyo.
Anaongeza: “Kocha aliyenipandisha kikosi cha wakubwa ni Didier Gomes Da Rosa. Aliniambia nina kipaji kikubwa, ila nahitaji niwe mvumilivu wa kujifunza kutoka kwa wazoefu, hivyo alinijenga mapema kiakili ndio maana nilipata nguvu ya kuendelea kujituma mazoezini.”
Pamoja na kukosa nafasi ya kucheza kupitia timu hiyo amefanya vitu vingi vya maendeleo, ingawa hakutaka kuviweka wazi.
“Nina hatua ya maendeleo. Kwa bahati mbaya siyo muumini wa kutaja vitu vyangu nje ya soka,” anasema.

HAKUWATARAJIA HAWA
Feruzi anasema Simba imemkutanisha na mastaa ambao ilikuwa ni ndoto yake kukutana nao akiwataja baadhi kuwa ni Clatous Chama ambaye kwa sasa yupo Yanga, John Bocco (JKT Tanzania), Moses Phiri, Pascal Wawa (walioondoka nchini), Joash Onyango (Dodoma Jiji), Manula, Kakolanya na Pape Ousmane Sakho (Raja Casablanca).
“Nilipata bahati ya kubadilishana nao mawazo, walinijenga kujua anavyotakiwa awe mchezaji mkubwa kuanzia maisha ya uwanjani hadi nje. Mfano kama Wawa nikidaka vizuri mechi za kirafiki alikuwa ananipa pesa, vifaa vya michezo na alikuwa ananisisitiza fanya sana mazoezi hayadanganyi. Manula ananipigia simu ananipitia na gari na kunirudisha nyumbani na hao walioondoka bado nawasiliana nao,” anasema.
HAKUWA KIPA
Wakati anaanza kucheza soka alikuwa mchezaji kiraka (namba 6, 8, 10), anasema ilitokea siku moja kipa wa timu yake ya mtaani alipata changamoto akaambiwa awe anadaka na tangu siku hiyo akalazimishwa acheze nafasi hiyo.
“Nilidaka mechi nyingi, baada ya kurejea kipa nikamwambia kocha sihitaji tena kucheza nafasi hiyo, lakini wachezaji wenzangu wakanikusanyikia na kuniambia niwe nadaka. Ikanichukua mwezi kukubaliana na hilo. Nakumbuka nilikuwa na miaka 16 ndio ikawa hivyo hadi sasa,” anasema.

TUKIO HILI LILIMTISHA
Feruzi anasema anasimulia tukio aliloliona 2016 akiwa na timu yake ya mtaani iliyokuwa inaitwa Vigezo FC ya Mbagala. Hakumbuki walicheza dhidi ya timu gani, lakini kilichobaki katika akili yake ni mchezaji mwenzao kuvunjika mguu.
“Yule mchezaji alijitangulizia mpira kuna mtu akawa anauwahi bahati mbaya akaruka ili akaupige akavunjika mguu hadi ukapinda. Niliogopa sana na kujiuliza maswali kama nitaweza changamoto za mpira. Kilichonipa moyo nikakumbuka darasani sina akili kubwa ya kufaulu mitihani ikanibidi nikaze,” anasema.
Mbali na hilo, anamtaja mchezaji anayemkubali Ligi Kuu Bara kuwa ni beki wa Simba, Abdulzack Hamza.
“Kwa beki wa aina yake kwa kipindi hiki sijamuona bado. Kwa mara ya kwanza namuona mazoezini kuna mtu nilimwambia huyu jamaa hata maproo hawawezi kumuweka benchi,” anasema Feruzi.
Mchezaji huyo anaitaja pesa yake kubwa mara ya kwanza kuikamata katika soka kuwa ni Sh5 milioni baada ya kwenda kucheza Msumbiji.
“Kuna timu ya Daraja la Kwanza ilinichukua Msumbiji kabla ya kujiunga na Simba. Sikufikisha miezi sita nikarudi Tanzania, Simba ikaniona ikanisajili makocha walioona kipaji changu ni Nico Kiondo na Nico Nyagawa.”