Prime
Fei Toto anyemelea ufalme mpya Bara

Muktasari:
- Ajibu ndiye mfalme wa asisti katika Ligi Kuu Bara aliyoiweka misimu saba iliyopiota kwa kufikisha 17 kabla ya Chama kujijitumua kwa nyota wa kigeni na kufikisha 15 misimu miwili iliyopita, hivyo Fei Toto amesaliwa na asisti mbili katika mechi nne zilizobaki za Azam kufikia rekodi ya Chama.
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto, ndiye anayeongoza orodha ya wakali wa asisti katika Ligi Kuu Bara msimu huu hadi sasa akiwa nazo 13, lakini akikabiliwa na kazi mbili nzito za kuvunja rekodi zilizopo, ikiwamo kufikia ufalme wa kiungo wa sasa Yanga, Clatous Chama na ile ya Ibrahim Ajibu.
Ajibu ndiye mfalme wa asisti katika Ligi Kuu Bara aliyoiweka misimu saba iliyopiota kwa kufikisha 17 kabla ya Chama kujijitumua kwa nyota wa kigeni na kufikisha 15 misimu miwili iliyopita, hivyo Fei Toto amesaliwa na asisti mbili katika mechi nne zilizobaki za Azam kufikia rekodi ya Chama.
Akimalizana na rekodi ya Chama, kiungo mshambuliaji huyo wa zamani wa JKU na Yanga atakuwa na kazi ya kuisaka ile ya Ajibu aliyoiweka 2018-2019 wakati akiitumikia Yanga, kitu ambacho kitampa heshima kubwa mchezaji huyo anayehusishwa na klabu za Simba na Yanga kutaka kumtoa Azam.

Ajibu kwa sasa anakipiga Dodoma Jiji, lakini akiwa amepoteza makali tangu aliporejea Simba kisha kupita Singida Big Stars na Azam. Fei Toto alimaliza mfungaji namba mbili wa Ligi Kuu msimu uliopita akitupia 19, mawili pungufu na aliyokuwa nayo kinara Stephane Aziz Ki aliyefunga mabao 21 katika msimu uliopita alimaliza na asisti saba.

Mbali na asisti 13 alizonazo, Fei Toto pia ana mabao manne katika Ligi Kuu huku Azam ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51 baada ya mechi 26.
Kiwango alichoonyesha Fei Toto hadi sasa kimemfanya kocha mkuu wa Azam, Rachid Taoussi kumwagia sifa kiungo huyo kwamba ni mmoja ya wachezaji walioibeba timu hiyo hadi ilipo, huku akiwa amempangia majukumu mengi tofauti na aliyokuwa nayo msimu uliopita.
Katika msimu uliopita Fei ndiye aliyekuwa mshambuliaji tegemeo, kitu kilichomfanya ahusike na idadi kubwa ya mabao akifunga 19 na kuasisti saba, lakini chini ya Taoussi amempa kazi ya kuichezesha timu ndio maana amekuwa kinara wa asisti na kufunga kawaachia wachezaji wengine wakiamo Nassor Saadun, Jhonier Blanco na Gibril Sillah.
Hata hivyo, Taoussi anasema hamzuii kiungo huyo kufunga, ila kwake kipaumbele ni kuisaidia timu kupata ushindi kwanza, kwani anafahamu uwezo wake vizuri na anaamini hilo analiweza.

KAZI IKO HAPA
Azam imesaliwa na mechi nne,ikiwa imekwishacheza 26 na kufunga mabao 39, ikishinda 18, sare sita na kupoteza mitano na ikiwa imefikisha pointi 51.
Kwa sasa Fei yupo karibu sana na rekodi za kiungo wa zamani wa Simba anayekipiga Yanga, Chama, ambaye alimaliza msimu 2022/23 akiwa na asisti 15.
Huku kwa upande Ibrahim Ajibu aliyewahi kuzichezea Simba, Yanga na Azam aliweka rekodi tamu msimu wa 2018/19 kwa kuasisti 17 ambayo haijafikiwa hadi sasa.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto anasema bidii yake ni kubwa kuhakikisha anamaliza msimu akiwa amejiimarisha hasa kwa upande wa rekodi nzuri.

“Kwanza sio kazi nyepesi kuhakikisha mimi kama mchezaji naisaidia timu kupata matokeo na kuimarisha rekodi zangu. Mpaka hapa nilipofika najipongeza,” anasema mchezaji huyo.
“Kufikia rekodi za mastaa kama Ajibu na Chama kwangu linawezekana kabisa ni suala la muda tu na katika mechi nne zilizosalia uwezekano huo upo.”
Azam imesaliwa na mechi nne dhidi ya Kagera Sugar, Dodoma Jiji, Tabora United na Fountain Gate, huku ni Tabora tu ndio aliyoikosa katika mechi za duru la kwanza, kwani Azam ilipoteza ugenini kwa mabao 2-1, lakini wapinzani wengine watatu aliwagusa kwa kuasisti na kufunga mabao.
Rekodi zilizopo ni kwamba alifunga bao moja na pekee katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, kisha akaasisti mara mbili dhidi ya Dodoma waliyoinyuka mabao 3-1 ugenini na nyingine moja Azam ilipovaana na Fountain Gate na kuwanyuka mabao 2-0 yaliyotupiwa kimiani na Gibril Sillah na Alassane Diao.
Kama alivyoisaidia Azam msimu uliopita kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu na kukata tiketi ya Ligi tya Mabingwa Afrika, Fei Toto ana kibarua kupitia mechi hizo nne zilizosalia kumaliza kama mfalme mpya wa asisti, lakini kuiwezesha timu kumaliza nafasi ya tatu ili kukatab tiketi ya CAF.

Azam imetolewa Kombe la Shirikisho (FA) katika hatua ya 32 Bora, hivyo tiketi pekee iliyosalia kwa timu hiyo kushiriki tena michuano ya CAF ni kumaliza nafasi ya tatu inayonyemelewa na Singida Black Stars yenye pointi 50 kwa sasa, ambaypo pia ipo nusu fainali ya Ko-mbe la Shirikisho (FA).