Fadlu amevuka mtego wa kwanza Simba

Muktasari:
- Fadlu aliyetambulishwa na Simba Julai 5 akichukua mikoba ya Abdelhak Benchikha, alikuwa akisubiriwa kwa hamu na kila mwana Simba kuona ataanzaje msimu wa Ligi Kuu Bara ili kumlinganisha na wenzake waliomtangulia ndani ya misimu 10 iliyopita.
KWA dakika 180 ni sawa na mechi mbili ambazo Kocha Fadlu Davids amekiongoza kikosi cha Simba SC kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara, unaweza kusema kwamba amevuka mtihani wa kwanza aliokuwa nao, huku kwa namna moja ama nyingine akiwafunika watangulizi wake.
Fadlu aliyetambulishwa na Simba Julai 5 akichukua mikoba ya Abdelhak Benchikha, alikuwa akisubiriwa kwa hamu na kila mwana Simba kuona ataanzaje msimu wa Ligi Kuu Bara ili kumlinganisha na wenzake waliomtangulia ndani ya misimu 10 iliyopita.
Ukiachana na kupoteza Ngao ya Jamii, katika ligi Fadlu ameonekana ameanza vizuri zaidi kuliko wenzake waliotangulia kuanzia msimu wa 2014/15 na hadi sasa unaposoma Mwanaspoti ni kwamba, Simba ndani ya misimu 11 timu hiyo imenolewa na makocha zaidi ya 12 wakiwemo waliokaimu nafasi ya kocha mkuu kama Juma Mgunda, Suleman Matola, Hitimana Thierry, Denis Kitambi na Masoud Djuma.
Kati ya makocha wakuu wa Simba katika kipindi hicho cha kuanzia 2014/15 hadi sasa, Fadlu katika mechi mbili za kwanza za ligi ameonekana kuwafunika wenzake kitu ambacho unaweza kusema ni kama ameushinda mtihani wa kwanza aliokuwa nao wa kuhakikisha timu inaonyesha mwanga mzuri mwanzoni.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, mwenye umri wa miaka 43 aliyesaini mkataba wa miaka miwili, rekodi zinambeba kwa kuvuna pointi sita na mabao saba bila bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Fadlu alioyejiunga Simba alitokea kuwa, kocha msaidizi wa mabingwa wa Morocco, Raja Casablanca, mechi zake mbili za kwanza dhidi ya Tabora United na Fountain Gate akiwa nyumbani ameshinda zote kwa 7-0, akiichapa Nyuki wa Tabora 3-0 na kuichakaza Fountaini kwa 4-0.
Wakati Fadlu akifanikiwa kushinda mechi mbili za kwanza bila ya kuruhusu bao wakati kikosi chake kikifunga mabao saba, anafuatiwa na Patrick Aussems ambaye naye alifanya hivyo msimu wa 2018/19 lakini anahukumiwa kwa idadi ya mabao kwani kocha huyo Mbelgiji timu yake ilifunga mabao matatu pekee. Pia msimu uliofuatia 2019/20, Aussems pia alianza ligi vizuri kwa kukusanya pointi sita katika mechi mbili za kwanza lakini alifunga mabao matano na kuruhusu mawili.
Kocha Dylan Kerr raia wa Uingereza, msimu wa 2015/16 naye aliuanza vizuri kwa kushinda mechi mbili za kwanza lakini kwa mabao machache ambayo ni matatu na clean sheet mbili.
Zoran Maki ambaye hakudumu sana ndani ya Simba, lakini ameacha rekodi nzuri akishinda mechi mbili za mwanzoni mwa ligi kwa jumla ya mabao matano na clean sheet mbili. Ilikuwa msimu wa 2022-2023.
Kocha mwingine aliyeanza ligi kwa ushindi wa mechi mbili za kwanza alikuwa Roberto Oliveira ‘Robertinho’ katika msimu wa 2023/24 akiifunga Mtibwa Sugar 2-4 ugenini na nyumbani akashinda 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji. Hapa Simba ilifunga mabao sita na kuruhusu mawili. Bado amepitwa na Fadlu katika suala la clean sheet na mabao ya kufunga.
Goran Kopunovic ambaye kwa sasa anainoa Pamba Jiji, ndiye kocha aliyeanza vibaya zaidi ya wenzake Simba kwani ilishuhudiwa msimu wa 2014/15 akikusanya pointi mbili kwa maana ya kutoka sare mechi mbili za kwanza za msimu huo, timu yake ikifunga mabao matatu na kuruhusu matatu.
Kocha Pierre Lechantre alianza ligi kwa mkwara katika msimu wa 2017/18, kwani mechi ya kwanza alitoa dozi nzito ya mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, lakini mechi ya pili matokeo yakawa 0-0 dhidi ya Azam. Hapa kikosi chake kilifunga mabao mengi kama Simba ya Fadlu hivi sasa, lakini amepigwa bao katika pointi kwani alikusanya nne huku mwenzake akiwa nazo sita.
Akizungumzia kiwango cha timu yake na mwanzo mzuri wa msimu, Fadlu alisema: “Tumecheza vizuri na kushinda mechi. Nimefurahishwa na kiwango walichoonyesha wachezaji. Umekuwa ni mwendelezo wa kile tunachokitaka. Tunataka Simba iwe imara zaidi hivyo bado kuna mambo tunapaswa kuyafanyia kazi zaidi kwenye uwanja wa mazoezi. Ni machache ya kiufundi ambayo kama yatakamilika basi timu itakuwa imara zaidi ya hapa.”
KOCHA: Goran Kopunovic
POINTI: 2
MABAO YA KUFUNGA: 3
MABAO YA KUFUNGWA: 3
CLEAN SHEET: 0
MATOKEO: Simba 2-2 Coastal na Simba 1-1 Polisi Moro
MSIMU: 2015-2016
KOCHA: Dylan Kerr
POINTI: 6
MABAO YA KUFUNGA: 3
MABAO YA KUFUNGWA: 0
CLEAN SHEET: 2
MATOKEO: African Sports 0-1 Simba na Mgambo JKT 0-2 Simba
MSIMU: 2016-2017
KOCHA: Joseph Omog
POINTI: 4
MABAO YA KUFUNGA: 3
MABAO YA KUFUNGWA: 1
CLEAN SHEET: 1
MATOKEO: Simba 3-1 Ndanda na JKT Ruvu 0-0 Simba
MSIMU: 2017-2018
KOCHA: Pierre Lechantre
POINTI: 4
MABAO YA KUFUNGA: 7
MABAO YA KUFUNGWA:0
CLEAN SHEET: 2
MATOKEO: Simba 7-0 Ruvu Shooting na Azam 0-0 Simba
MSIMU: 2018-2019
KOCHA: Patrick Aussems
POINTI: 6
MABAO YA KUFUNGA: 3
MABAO YA KUFUNGWA: 0
CLEAN SHEET: 2
MATOKEO: Simba 1-0 Tanzania Prisons na Simba 2-0 Mbeya City
MSIMU: 2019-2020
KOCHA: Patrick Aussems
POINTI: 6
MABAO YA KUFUNGA: 5
MABAO YA KUFUNGWA: 2
CLEAN SHEET: 0
MATOKEO: JKT Tanzania 1-3 Simba na Simba 2-1 Mtibwa Sugar
MSIMU: 2020-2021
KOCHA: Sven Vandenbroeck
POINTI: 4
MABAO YA KUFUNGA: 3
MABAO YA KUFUNGWA: 2
CLEAN SHEET: 0
MATOKEO: Ihefu 1-2 Simba na Mtibwa Sugar 1-1 Simba
MSIMU: 2021-2022
KOCHA: Didier Gomes
POINTI: 4
MABAO YA KUFUNGA: 1
MABAO YA KUFUNGWA: 0
CLEAN SHEET: 2
MATOKEO: Biashara United 0-0 Simba na Dodoma Jiji 0-1 Simba
MSIMU: 2022-2023
KOCHA: Zoran Maki
POINTI: 6
MABAO YA KUFUNGA: 5
MABAO YA KUFUNGWA:0
CLEAN SHEET: 2
MATOKEO: Simba 3-0 Geita Gold na Simba 2-0 Kagera Sugar
MSIMU: 2023-2024
KOCHA: Roberto Oliveira ‘Robertinho’
POINTI: 6
MABAO YA KUFUNGA: 6
MABAO YA KUFUNGWA: 2
CLEAN SHEET: 1
MATOKEO: Mtibwa Sugar 2-4 Simba na Simba 2-0 Dodoma Jiji
MSIMU: 2024-2025
KOCHA: Fadlu Davids
POINTI: 6
MABAO YA KUFUNGA: 7
MABAO YA KUFUNGWA: 0
CLEAN SHEET: 2
MATOKEO: Simba 3-0 Tabora United na Simba 4-0 Fountain Gate