Prime
Fadlu akikomaa na haya, ataitesa RS Berkane

Muktasari:
- Ila leo sio mahala pake kulizungumzia tuangalie kinachoenda kutokea uwanjani. Kuna hadithi inayotia matumaini bila kujali ni Amaan au Lupaso.
FAINALI ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na Berkane kuchezwa Zanzibar badala ya kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuna mahali hatuko sawa. Kuna mambo yasiyohitaji siasa bali vitendo.
Ila leo sio mahala pake kulizungumzia tuangalie kinachoenda kutokea uwanjani. Kuna hadithi inayotia matumaini bila kujali ni Amaan au Lupaso.
Turudi katika mechi ya fainali ya pili Amaan Zanzibar. Habari za mchezo kupelekwa Unguja zimezima hadithi tamu ya msimu 2024/2025 kwa Simba. Matokeo yake mjadala sasa umekua ni uwanja unapokwenda kuchezwa mechi hiyo badala ya safari nzuri ya Simba ilipopita hadi kufika hapo walipo dakika hii. Kuna hadithi inayotia matumaini bila kujali ni Amaan au Lupaso.
Kutoka kutengeneza timu hadi kushindania vikombe vyote wanavyoshiriki msimu huu.

Ni jambo linalotokea mara chache. Kila wanaposhiriki kuna kitu wanakiwania na wako siriasi katika kusaka matokeo na kombe. Katika Ligi Kuu Bara wako nafasi ya pili na bado wana nafasi ya kuubeba ubingwa huo kwavile bado msimu haujamalizika.
Kombe la Shirikisho la TFF wako nusu fainali na Shirikisho Afrika wanasubiri nusu fainali ya pili kuamua bingwa wa michuano. Ni kombe jingine hilo liko mikononi mwao.
Hadithi ya Simba katika michuano ya Shirikisho la Soka Afrika(CAF) kwa takribani misimu saba ni ya kuvutia hasa mechi za nyumbani Benjamini Mkapa, ndio maana nawaelewa walipoamua kupambana mchezo upigwe kwa Lupaso.

Msimu huu Simba wamecheza mechi tano za CAF, Benjamin Mkapa na kushinda zote, huku wakifunga jumla ya mabao kumi ikijumlisha na mechi ya nusu fainali iliyochezwa Amaan walipata ushindi wa bao moja dhidi ya Stelenbosch. Kuna hadithi inayotia matumaini bila kujali ni Amaan au Lupaso.
Tuwatazame Simba kimbinu kwa nini wamekua na hadithi nzuri wanapokua nyumbani. Kwanza Kocha Fadlu Davids amekua muumini wa mfumo wa 1-4-2-3-1 kama muundo wa timu ndani ya kiwanja. Ipi faida wanayoipata kiwanjani kwa kujipanga hivyo?
Kwanza unaipa timu unyumbufu wa maumbo kutoka 1-4-2-3-1 kwenda 1–2-4-2-2 au 1-2-4-1-3 na mengine mengi kulingana na wapi mpira upo. Kwa kuwa timu nyingi huzuia kuanzia eneo la katika ya kiwanja zinapokuwa ugenini hutoa nafasi kwa Moussa Camara na mabeki wake wa kati kuanza kujenga mashambulizi kuanzia nyuma tena kukiwa hakuna shinikizo. Humruhusu Ngoma ambae ndiye mhimili wa Simba kwenye kujenga shambulizi kutoka nyuma.

Wakati timu inaanza huruhusu walinzi wapembeni kuungana na mstari wa viungo hivyo kufanya vizuri kwa kuwapa uhuru washambuliaji wa pembeni kuwa na uhuru wa kutembeza mpira bila hofu. Sambamba na kutunza mapana ya kiwanja na mara nyingi wamekua wakipokea mpira kati ya viungo na mabeki wa timu pinzani kitu ambacho kimekua kikimpa Mpanzu au Kibu nafasi ya kupokea mpira na kuwageukia mabeki wa timu pinzani na ndipo uhatari wa Simba ulipo.
Kilichotokea mechi ya kwanza kwa iliyopigwa Morocco kwa dakika za kwanza ni kwamba waliweka shinikizo kuanzia juu, hivyo kulazimisha muundo wa timu muda wote kuwa 1-4-4-1-1 au 1-4-4-2 kuwafanya washambuliaji wa pembeni kuwa kwenye mstari mmoja na viungo wa kuzuia. Hii ilikuwa swali gumu sana kwa Simba ambalo sitarajii kabisa kuliona likiulizwa Amaan kulingana na historia ya Berkane wakiwa ugenini.

Matumaini ni makubwa kwa Simba kuirudisha mechi upande wao kwa kujilinda wasiruhusu kufungwa huku wakitumia nafasi wanazo tengeneza kwani Berkane msimu huu wa michuano hii iliyojizolea umaarufu mkubwa wamekua timu imara kwenye nyakati zote za mchezo. Wako makini kila sekunde wanayokuwa mchezoni, haswa katika mechi hizi za mwisho ambazo wanaliona kombe liko mezani sambamba na kitita cha dola. Na ni timu kubwa yenye wachezaji wanaojua umuhimu wa mechi kama hizi.
Wana utaratibu mzuri wa kujilinda ikiwa timu iliyoruhusu magoli machache kuanzia hatua ya makundi hadi fainali wameruhusu wavu wao kutikiswa mara mbili. Kitu chanya kwa Simba ni kwamba mabao hayo wameruhusu ugenini dhidi ya Stellenbosch na CS Constantine.

Upande wangu, Simba siwadai ila wanapaswa kumalizia hii hadithi nzuri kwa kubeba ubingwa ili kuifanya hadithi iwe tamu kwa atakayesimuliwa msimu wa 2024/2025 kwa Simba ya Tanzania n a Afrika Mashariki ilibeba Kombe la Shirikisho.