Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dakika za jioni hatimaye Wabrazili wametema bungo

PAZIA Pict

Muktasari:

  • Waingereza walikuwa taifa la kwanza kati ya mataifa makubwa kisoka kuamua kumng'ata jongoo kwa meno.

KIBURI, majivuno, dharau, kujisikia kuna siku vinafika mwisho. Ilianzia kwa Waingereza na sasa imefika Brazil. Imechukua miaka mingi kuchutama, lakini taifa kubwa kisoka Brazil limeamua kwenda na kocha kutoka Italia. Carlo Ancelotti 'Don Carlo' mvuta sigara kubwa, Cigar.

Waingereza walikuwa taifa la kwanza kati ya mataifa makubwa kisoka kuamua kumng'ata jongoo kwa meno. Januari ya 2001 wakati dunia ikiwa bado ina mning'inio wa kuingia katika karne nyingine Waingereza walikutana London na kumchagua Mswedeni, Sven-Goran Eriksson kuwa kocha wao wa timu ya taifa.

Kabla ya hapo mataifa yote makubwa yalikuwa hayajawahi kuteua kocha wa kigeni kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa. Wabrazil, Waingereza, Waitaliano, Waargentina, Wajerumani, Waholanzi na Wafaransa wote walikuwa hawajawahi kumuita mgeni awafundishe namna mpira unavyochezwa. Waingereza baada ya kuzurura kwa makocha wa ndani kwa muda mrefu walikuwa wamekiri kwamba kazi ilipaswa kutoka nje.

PAZ 01

Kulikuwa na kelele nyingi kutoka kwa Waingereza. Hawakukubali kirahisi. Kwamba Mswedeni awafundishe mpira? Haikuwaingia akilini. Wengi bado walikuwa na kiburi na majivuno ya Uingereza wao. Kingine kilichowauma ilikuwa pesa ambayo Eriksson alikuwa anaingiza kibindoni kwa kuifundisha The Three Lions. Kila siku walitengeneza kashfa mpya kwa Eriksson. Walichambua hata vimada wake.

Baadaye Waingereza walionekana kuzoea. Walikwenda kwa Fabio Capello ambaye alikuwa Muitaliano kama ilivyo kwa Don Carlo. Na hata sasa hivi wamekwenda kwa Mjerumani, Thomas Tuchel ambaye wanaamini anaweza kuwapa Kombe la Dunia mwakani pale Marekani, Canada au Mexico. Waingereza wameshazoea wanapokutana kwamba kitu cha msingi ni kutafuta kocha bora, na sio kazima awe ametoka Uingereza.

Nadhani wamekubaliana na ukweli huo hata wakichukulia mfano wa ligi yao wenyewe. Ni timu gani kubwa inafundishwa na kocha wa Kiingereza? Kuanzia Arsenal, Manchester United, Manchester City, Liverpool na Chelsea. Yuko wapi kocha wa Kiingereza katika timu hizo? Na si kwao tu, kuna kocha wao gani anayetamba katika ligi nyingine?

PAZ 02

Wana wachezaji hadi wanaotamba nje ya England kamakina Jude Bellingham, Harry Kane, Jordan Henderson, Tammy Abraham na wengineo, lakini yu wapi kocha wa Kiingereza ambaye anafanya hivyo? Hakuna. Labda ndio maana sasa hivi akichukuliwa kocha wa kigeni Waingereza wanaamua kukaa kimya. Hawana hoja za msingi za kukataa.

Na sasa Wabrazil wamefuata nyayo. Usichukulie kama kitu rahisi sana kwa sababu Wabrazil wana maringo yao. Wao ndio wamechukua Kombe la Dunia mara nyingi zaidi. Mara tano. Wao ndio walikuwa wanakwenda Ulaya na aina yao ya mpira ambayo iliwashinda wazungu wa Ulaya. Walikuwa wanakuja Ulaya na staili yao ya mpira inaitwa Samba. Waliumiliki mpira katika kiwango cha juu.

Wakati huo walikuwa wanatumia wachezaji wa ndani na walikuwa hawajaanza kucheza Ulaya. Walitwaa Kombe la Dunia pale Stockholm, Sweden mwaka 1958 wakiwa na kina Pele na wengineo. Wakarudi tena Ulaya kutwaa Kombe la Dunia katika ardhi ya Czech mwaka 1962 wakiwa na vipaji vyao kutoka ndani. Walisumbua mno.

PAZ 03

Mwaka 1970 wakaenda zao Mexico wakiwa na kina Pele, Vava, Mane Garincha, Tostao, Carlos Alberto na wengineo na wakacheza mpira mwingi na kutwaa kombe la tatu la dunia. Baada ya hapo walipigwa benchi kwa miaka 24 mpaka walipotwaa Kombe la Dunia pale Marekani mwaka 1994. Hapo katikati kabla ya kwenda Marekani walikuwa wamepunguza kiburi na wakaamua kwenda na wakati kwa kuanza kupeleka wachezaji nje ya Brazil.

Waligundua kwamba walikuwa wanachelewa kutwaa tena Kombe la Dunia kwa sababu mpira wa Ulaya ulikuwa umeongezeka ushindani na wao walikuwa bado wamejifungia ndani. Wakapeleka wachezaji wengi Ulaya kwa ajili ya kwenda sambamba na wazungu wa Ulaya. Labda ndio maana walitwaa Kombe la Dunia dhidi ya Italia pale Marekani.

Na sasa baada ya miaka mingi kupita tangu mpira kuanzishwa, Wabrazili wameamua kutema bungo kwa kocha. Wameamua kwenda na kocha Muitaliano. Labda kuna kitu wamekiona kutoka kwake. Labda wameamua kujikita na mpira wa Ulaya lakini hapa kuna mambo mawili ya kuzingatia kwa haraka haraka.

PAZ 04

Kwanza kabisa Brazil haina makocha wa kuishtua dunia kwa sasa. Hata huku Ulaya huwa hawatuletei makocha. Kocha wa mwisho ambaye walituletea alikuwa Luis Felipe Scolari. Mpira mkubwa upo Ulaya, kwanini wasituletee makocha bora kama wao ndio wataalamu wa mpira? Matokeo yake wanaotamba kwa sasa ni makocha kutoka Hispania, Uholanzi, Ujerumani na Italia.

Lakini hapo hapo ni wazi kwamba mpira wao umeparaganyika. Wabrazili sio wale tena. Wamepoteza mambo yote mawili. Wamepoteza samba lao na pia wamepoteza vipaji vya mchezaji mmoja mmoja tofauti na ilivyokuwa zamani. Leo Brazil imekuwa timu ya kawaida tu. Haishangazi kuona tangu wale wahuni kina Ronaldinho, Ronaldo de Lima, Rivaldo na Roberto Carlos walipotwaa ubingwa pale Yokohama mwaka 2002, hakuna Brazil nyingine iliyotwaa Kombe la Dunia.

Kama hawakutwaa Kombe la Dunia kwa miaka 24 kuanzia 1970 mpaka 1994, wakajipanga kwa kupeleka wachezaji Ulaya, inawezekana na sasa baada ya kukosa ubingwa kwa miaka 23 wameamua kujipanga kwa kuleta makocha wa kigeni kuwafundisha namna ambavyo mpira umebadilika kwa kiasi kikubwa.

PAZ 05

Hatujasikia malalamiko mengi kutoka kwa Wabrazili kuhusu hili. Labda kwa sababu taarifa zao zinatolewa kwa idhaa za Wareno ndio maana hatujasikia, lakini nadhani lazima watakuwapo wahifadhina ambao hawataafiki kuhusu wao kufundishwa mpira na Muitaliano wakati Brazil imetwaa Kombe la Dunia mara nyingi kuliko Italia.

Vinginevyo dunia ya mpira yenyewe imebadilika kwa ujumla. Wabrazil ilikuwa lazima wakubali matokeo. Tazama namna ambavyo mpira mzuri kwa sasa unachezwa na Wahispaniola na unafundishwa na Wahispaniola. Ule mpira ambao tuliuona ukichezwa na Wabrazil na ukatustaajabisha sasa hivi unachezwa na Wahispaniola na unachezwa kwa umaridadi zaidi.

Labda ndio maana wamepunguza kiburi na kuamua kukubali yaishe. Nani anafuata baada ya hapo? Wajerumani? Waitaliano? Wafaransa? Waholanzi? Waargentina? Hatujui. Nashindwa kutabiri kwa sababu hizi nchi zinajivunia kuwa na makocha wazuri. Wengine mpaka sasa hivi bado wapo tofauti na Brazil ambayo haina hata kocha mkubwa anayefundisha timu kubwa kwa sasa.

Hata hivyo, wakati utafika na wao wanaweza kubadilika kama Waingereza na Wabrazil walivyobadilika. Itachukua muda lakini inawezekana. Fikiria ni timu gani ya taifa kati ya hizo ambayo inaweza kumkataa Pep Guardiola? Sioni. Kama Wabrazil wamekwenda kwa Don Carlo ambaye amedhalilika majuzi akiwa na Real Madrid, watakataa vipi kwa kocha aliye katika fomu kama Guardiola?