EXCLUSIVE: Idd Pazi father aliyebeba mazito moyoni

 “MOYO wa mtu ni kichaka.” Ndivyo anavyosema kipa na kocha wa zamani wa makipa wa Simba, Idd Pazi  ‘Father’ ambaye kwa sasa anaishi wilayani hapa akipatiwa matibabu.

Pazi aliyefahamika kama Tanzania One wa kwanza nchini, jina lililoanza kutumika kwake mwaka 1983 akiwa mchezaji wa Simba yupo Uvinza, Kigoma zaidi ya mwaka mmoja akitibiwa baada ya kuchukuliwa na ndugu zake kwani yeye makazi yake yalikuwa jijini Dar es Salaam.

Mwanaspoti ambalo lilifika nyumbani kwa ndugu zake lilizungumza na Pazi ambaye anasema anaumwa kwa kipindi kirefu, ingawa kwa sasa anaona ana nafuu kubwa ukilinganisha na awali, lakini kwa mtu mgeni ama anayemuona kwa mara ya kwanza bado unaona afya yake haijaimarika sawasawa.

“Mwanangu wanasema moyo wa mtu ni kichaka, ndivyo ilivyo kwangu, moyo wangu umebeba mambo mengi sana yenye maumivu, wakati mwingine najikuta machozi yakinitoka tu. Ila naamini Mungu, ipo siku nitakuwa sawa na kuendelea na shughuli zangu,” anasema Pazi aliyewahi kuzidakika Majimaji, Plisner na kucheza soka la kulipwa Sudan na akuongeza;

“Nimeumwa sana kwa muda mrefu lakini sasa naendelea vizuri, maana ilikuwa inakatisha tamaa, nilikuwa nasimuliwa tu kuwa nilifikia hatua ya kuchanganyikiwa kabisa, nawaza hivi kweli ni mimi lakini bado namshukuru Mungu kwa hapa nilipofikia.

“Sipendi kukukumbuka mengi niliyopita maana yalikuwa ni maumivu makali sana kikubwa napaswa kuwa na shukrani kwa Mungu hadi hapa naamini nitarejea kufanya shughuli zangu, natamani sana kurudi kupambania mpira kwa maana ya kufundisha vijana ama kuwashauri,” anasema Pazi na kuongeza:

“Nimetumia gharama kubwa kuokoa maisha yangu kama nilivyosema hapo awali ilifikia hatua napoteza kumbukumbu, hivyo bado napambana kujiweka sawa.”

Hata hivyo, Pazi ambaye ni baba mzazi wa mshambuliaji Zahoro Pazi hakusita kuelezea machache katika soka alipokuwa akicheza na sasa hasa kwa makipa nafasi aliyokuwa akiicheza kwenye timu kadhaa alizopita.


KASEJA NA MANULA

Father aliyeanza kucheza soka miaka ya 1970 akiwa kama mshambuliaji kabla ya kuhamia kwenye ukipa, anasema Juma Kaseja ni kipa anayependa kukosolewa na kufundishwa kama ilivyo kwa Ivo Mapunda na kwamba walikuwa bora, huku akimtaka Aishi Manula kuishi maisha ya watangulizi wake ili awe bora zaidi.

“Makipa wazuri wapo wachache siku hizi, akikaa mmoja basi ndio huyohuyo anaangaliwa zaidi tofauti na miaka yetu timu nyingi zilikuwa na makipa wazuri na ushindani ulikuwepo.

“Baada ya sisi kuondoka walikuwepo wengine achana na kina Mwameja wenye ubora wao, bali nazungumzia hawa vijana kama kina Kaseja, Ivo wamekuja na kina Manula, Beno Kakolanya na wengine.

“Tatizo kubwa kwa sasa timu kukosa makipa wengi ni kwa vile siku hizi vijana wanajifanya wanajua kila kitu hata kama wanakosea, nakumbuka wakati Kaseja anadaka pamoja na kuwa kwenye ubora wake lakini alipenda sana kujishusha kutafuta maarifa mengine ya ziada kwa watangulizi wake.

“Nilivyorudi kutoka Oman, nilimkuta Kaseja akiwa kwenye changamoto kubwa ndani ya Simba, kwani alikuwa na tatizo la kudaka mipira ya mbali, alinifuata kunieleza na wakati huo Simba walinichukua basi nilikaa naye miezi mitatu tatizo likaisha.

“Mara nyingi alinifuata kule Ukonga akiwa na mipira yake anaomba tufanye mazoezi ya sisi tu wawili tu, niliona juhudi zake na kiu yake sikumkatisha tamaa tukafanya mazoezi, hivyo hivyo kwa Ivo naye alinitafuta na wakati mwingine wanakwambia wana shida ya kudaka mipira fulani basi tunafanyia kazi kabla ya mechi zao.

“Hakuna anayejua kila kitu ila wakati mwingine unapaswa kujifunza kutoka kwa mwenzako, kujifunza kitu kwa ni njema huwezi kuchekwa ama kudharauliwa pengine hujui, lakini ukijifanya unajua kila kitu, basi huwezi kubadilika makosa yako maana utamwamini yule tu anayekufundisha kwa wakati huo ilihali naye ni binadamu mwenye upungufu wake,” anasema Pazi aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kucheza soka Indonesia.


AMCHOMOA MSHERI YANGA

Pazi anasema ukiachana na makipa aliowazungumzia hapo juu basi Tanzania One anayemuona kwa miaka ijayo kama atapewa nafasi basi atakuwa kipa wa Yanga, Abutwalib Mshery.

“Tatizo ni Yanga imetoan Tanzania One mmoja tu, Sahau Kambi lakini kipa anayetaka kuwa Tanzania One anapaswa kuchezea Simba, namuona Msheri ndiye Tanzania One ajaye ila aondoke Yanga aende sehemu nyingine na baadaye anaweza kubahatika kuidakia Simba.

“Ni kipa mzuri lakini anakaa benchi, natamani kumuona akicheza, ana kipaji na uwezo mkubwa tu ila sasa huwezi kumkalisha benchi Djigui Diarra. Bado hajachelewa anaweza kuomba hata dirisha dogo kwenda kuichezea timu za KMC, Namungo, naamini ataibeba sana nchi baadaye.”


AVUNJA MKATABA WA LAKRED

Simba msimu huu ina makipa wanne, watatu ni wazawa na mgeni mmoja. Kuna Manula, Hussein Abel, Ally Salim na Ayoub Lakred raia wa Moroco. Pazi anawachambua makipa hao.

“Sikuona sababu ya Simba kuleta kipa wa kigeni kwa sasa tena kutoka Moroco, kuumwa kwa Manula sio kwamba haponi walitakiwa kuwaamini wazawa na wasingeruhusu Beno aondoke. Unaposajili kipa wa kigeni ina maana ndiye anayetakiwa kuwa kipa namba moja.

“Sasa Manula anapona na kila mtu anafahamu uwezo wake sasa utakalisha Manula nje ili Ayoub acheze? Kwa Simba ninayoifahamu siamini kama hicho kitu kinaweza kutokea pale Manula atakaporejea kikosini.

“Hebu angalia Yanga, walimleta Diarra tena mwenye uwezo mkubwa kila mtu anafahamu makipa wengine wote wazawa wamekubali kuanzia benchi, je, kwa Manula itakuwa hivyo? Usajili mwingine naweza kusema hauna sababu wakati mwingine.

“Ninachoweza kuwaambia Simba kama Ayoub hana uwezo kumzidi Manula basi wavunje mkataba wake haina haja kwasasa na kama uwezo wake ni mkubwa basi Manula aanzie benchi kama ilivyo kwa Metacha Mnata ambaye kakubaliana na hali hiyo pale Yanga, hivyo Manula naye akubali.

“Huyu Salim pamoja na kwamba amecheza mechi hizi za awali vizuri, bado anapaswa kujifunza zaidi aende timu ambayo atapata nafasi ya kudaka mara kwa mara ili aendelee kuiva vizuri mechi mbili ama tatu sio kipimo kizuri cha ubora wake, Salim amechelewa sana na umri unaenda.

“Kuhusu Abel ambaye amesajiliwa kuchukua nafasi ya Beno basi anapaswa kupambana vilivyo ili kumpa ushindani Manula kama alivyokuwa anafanya mtangulizi wake, awe jasiri na apambane kweli. Beno hakuwa na hofu juu ya Manula na ninaamini Manula alimhofia Beno pamoja na changamoto alizokuwa anakutana nazo ila ni kwavile Manula amejitengenezea ufalme.

“Namsihi Abel kwamba asife moyo hata Salim alikuwa hapati nafasi, ila ajitambue kuwa ameingia kwenye timu yenye ushindani mkali wa namba, asiwe mtu wa kujifungia atafute mazoezi binafsi kama ilivyokuwa kwa akina Kaseja, awatafute hao wamwongezee maarifa,” anasema Pazi.


KWA NINI TANZANIA ONE

Anasema alipewa jina hilo na watangazaji wa Redio Tanzania wakati huo baada ya kutoka kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika Nairobi Kenya. Anasimulia:

“Kwenye mashindano hayo ambayo yalishirikisha timu mbalimbali mwaka 1983 kuna kipa alikuwa anidakia AFC Leopards na Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars Mahmoud Abbas aliyeitrwa ‘Kenya One’, siku hiyo ilikuwa mechi ya timu ya Tanzania Bara na Kenya. Kwetu golini nilikuwepo mimi na kwao alisimama yeye, aisee alikuwa kipa kweli.

“Sasa kila akiokoa mpira watangazaji wa kule wanasema Kenya One, Kenya One na ikumbukwe niliitwa kwenye timu hiyo nikiwa nimefungiwa kwasababu Majimaji walidai nimesaini Simba nikiwa mchezaji wao.

“Hivyo nilikuwa sidaki mechi za ligi ndani ya Simba kwa kipindi hicho.

“Mwaka uliofuata kwa maana ya 1984 nilianza rasmi kudaka mechi za Ligi Kuu nakumbuka mwaka huo Simba ilitwaa ubingwa na haikupoteza mechi hivyo kila nikidaka watangazaji wakawa wananiita Tanzania One na ndipo jina hilo lilipoanzia na limekuwa hadi sasa.

“Na ndani ya Taifa Stars nilidaka tukiwa na makipa wenzangu Hamisi Kinye na Juma Mhina na mwaka 1985 nilisajiliwa Al Hilal ya Sudan nikiwa Mtanzania wa kwanza kuidakia timu hiyo.

“Kama nilivyosema Simba ina bahati ya kuwa na Tanzania One, nilipotoka akaja Mwameja, Kaseja na sasa Manula ila sielewi na sioni mwanga kwamba baada ya Manula nani atakuwa Tanzania One, maana wachezaji wa sasa hawatabiriki pia, kiukweli anapaswa kuandaliwa mwingine sasa Manula muda umeanza kumtupa na akubaliane na hilo ila sio Salim hawezi kuvaa hicho kiatu.”


SIMBA IENDE MALI, BURKINA FASO

“Nawashauri viongozi wa Simba, siku wakitaka kipa wa kigeni basi waende nchi za Magharibi kama Mali, Burkina Faso kuna makipa wazuri sana na sio hawa kutoka nchi za Kiarabu, mpira wa hapa wengi wanaushindwa,” anasema Pazi na kuongeza kwa kumtaja nyota wa zamani wa Yanga, Abubakar Salum  ‘Sure Boy’ ambaye ni baba mzazi wa Salum Abubakar aliyewahi kukipiga Azam FC na sasa Yanga kuwa ni kati ya wachezaji bora walioweka rekodi kwenye soka la Bongo.

“Hasa namkumbuka kwenye mechi ya fainali ya kombe la Afrika Mashariki na Kati, Yanga walicheza na Al Merrikh pale Uhuru (Shamba la Bibi), mwaka 1986 ingawa Yanga hawakutwaa ubingwa kwani walifungwa kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kutoka sare ya 2-2.

“Al Merrikh walianza kuifunga Yanga, lakini Yanga wakasawazisha dakika za nyongeza mabao lililofungwa na Sure Boy aliyetokea benchi, hivyo Yanga sasa inacheza na timu ambayo wana historia nayo kama ilivyo kwa Simba kucheza na Al Ahly mechi ijayo ya African Football League na pia Al Hilal kwa sababu nilichezea timu hiyo.

“Naziombea timu zote zinazocheza michuano ya CAF zipate matokeo mazuri na wasiwadharau wapinzani wao, mpira unabadilika na lolote linaweza kutokea. Mimi binafsi natamani ningekuwa nazishuhudia mechi hizo ila hali yangu ndiyo kama hivi, nakumbuka sana michezo,” anasema Pazi.