Exclusive... HADHARA Fundi wa danadana anayeteseka kwa maradhi

Muktasari:
- Huko ni mbali sana, Kibongo Bongo jina la Hadhara Charles la mwanadada mwenye kipaji cha kuchezea mpira 'FreeStyle', licha ya kutembea nchini 10 Afrika, lakini maisha yake ni duni.
UMAARUFU sio utajiri na hakuna uhusiano kabisa, ukitaka kuamini hilo aliyekua Rais wa Uruguay, Jose Mujica alijulikana kama rais maskini zaidi duniani, licha ya kushika nyadhifa za juu za uongozi.
Huko ni mbali sana, Kibongo Bongo jina la Hadhara Charles la mwanadada mwenye kipaji cha kuchezea mpira 'FreeStyle', licha ya kutembea nchini 10 Afrika, lakini maisha yake ni duni.
Ukiachana na ugumu wa maisha yake, mwanadada huyo anasumbuliwa na ugonjwa ambao hajui afanye nini ili kuweza kupona, pia kapitia mikasa mbalimbali, iliyomfanya awe na presha ya kushuka.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti juzi jijini Dar es Salaam, mwanadada huyo mkali wa kupiga danadana kwa kutumia viungo tofauti vya mwili, anafunguka mambo mengi, ikiwemo kumkumbusha Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba bado anamtegemea katika ahadi aliyompa akiamini inaweza ikamvusha kutoka sehemu moja hadi nyingine.
"Najua mheshimiwa ana mambo mengi, lakini aliniahidi atanisaidia, naamini kupitia chombo chenu cha Habari cha Mwananchi Communications Ltd (MCL), ataona hilo," anasema Hadhara kwa sauti ya huzuni.

MGONJWA NA HATMA YAKE
Anasumbuliwa na ugonjwa wa kupoteza fahamu, wakati mwingine anajing'ata ulimi na kutoka damu masikioni, hivyo anahitaji msaada ili kurejea katika hali aliyokuwa nayo awali na kumfanya apige mishemishe kutafuta riziki na kuwapa mashabiki burudani.
Katikati ya mahojiano, alianza kujisikia vibaya, akaomba msaada wa kuitiwa dada zake ili wamshike kichwani kwa ajili ya kumsemea maneno na kabla hawajafika, ghafla akaanza kutoa povu mdomoni, ndugu zake wakawahi kumsaidia.
Mahojiano hayo yalifanyika nje ya nyumba ya ndugu zake (nyumbani kwa babu yao iliyopo Tandale).
"Mwandishi najisikia vibaya, acha kufanya mahojiano, niitie dada yangu anishike kichwani, ondoka haraka, sihitaji mtu yeyote, ondoka," kisha wakatokea dada zake wawili wakamshika kichwa na kumsemea maneno baadae wakawa wanamvuta kumwingiza ndani.
Mahojiano hayo yakasimama takribani nusu saa, ili kujua hali ya mgongwa inaendeleaje, akarejea katika hali ya kawaida, huku uso wake ukiwa umechoka, kisha akasema; "Nasumbuka sana, sijui hatma ya hali yangu itakuwa ni ipi."
Anaulizwa unapokuwa unasafiri, inapokutokea hali hiyo, unakuaje? Anajibu "Kwanza nimeanza kusumbuliwa tangu nikiwa mdogo, kuna wakati nikawa naumwa mara chache sana, imekuja kuzidi baada ya kufariki dunia kwa mume wangu mwaka jana.
"Kuna safari ya nje, niliwahi kupoteza fahamu, nilioenda nao wakanisaidia ingawa iliwashitua sana, kuna wakati nililazwa Muhimbili nikiwa nasumbuliwa na miguu, ila madaktari wakasema hawaoni ugonjwa nina msongo wa mawazo.
"Nilishauriwa na madaktari niache kuchezea mipira ili nikipumzishe kichwa changu, ndiyo maana natamani nipate msaada ili niweze kufanya shughuli nyingine."
Dada zake waliomsaidia wakati tukiwa kwenye mahojiano, walikataa kuzungumza lolote wala kurekodiwa video wakisema taratibu zao za kiimani haziwaruhusu kama wanawake, ila walisema kama ni mtihani alionao ndugu yao ni huo ulioonekana katika mahojiano na huwa zaidi ya hapo.

HATAKIWI KUKAA HUKU
Anasema mama yake mzazi, Asia Humoud (hakuwepo wakati wa mahojiano hayo), huwa anamwambia hapaswi kwenda ufukweni, kukaa sehemu palipo na moto, ama kuchota maji kwenye visima, lengo ni kuokoa maisha yake, pindi ikitokea amedondoka hasa kama hakuna mtu wa kumsaidia.
"Kuna wakati mwingine nikiwa mwenye huko Chanika ninakoishi, nikianguka naweza nikaa muda mrefu hadi fahamu zitakaponirejea, kuna wakati najing'ata ulimi unatoka damu, ama damu kutoka masikioni," anasema aliyeanza kupiga danadana tangu akiwa shuleni na uwezo wa kuzipiga hata 3,000 bila kupumzika.
DOKTA SHITA
Daktari maarufu na Mwandishi wa Spoti Dokta wa Mwanaspoti anayeliandikia pia Mwananchi, Shita Samwel anasema zipo sababu nyingi zinazochagiza kutokea kwa hali hiyo ikiwemo upungufu wa damu wowote yenye oksijeni katika ubongo, ndiyo sababu ya haraka mtu kupoteza fahamu.
Alipoulizwa ugonjwa huo una tiba alijibu; "Kupoteza fahamu sio ugonjwa kamili bali ni dalili za uwepo wa ugonjwa au hitilafu kwa hiyo kupoteza fahamu kutategemea na kubainika kwa chanzo."

TUKIO GUMU
Japo amesamehe, ila tukio ambalo hatakaa alisahau katika maisha yake, aligombana na ndugu yake mmoja, wakapigana baada ya kumshinda, akawaita wengine wawili wakawa watatu wakamwagia ndoo kubwa ya maji ya moto.
"Wawili walinishika mikono, mmoja akawa ananimwagia maji ya moto niliungua sana, pamoja na hayo yote, nilisamehe. Hakuna binadamu asiyekosea na wote ni wa Mungu hakuna sababu ya kuishi kwa visasi," anasema. (Tukio hili Mwanaspoti liliwahi kuliripoti miaka kadhaa iliyopita, sambamba na picha zake.)
TRUMP AACHA ALAMA
Miaka sita iliyopita, alikwenda kufanya shoo Malawi, katika mji wa Lilongwe, akachukuliwa video, iliyopostiwa na mkaka mmoja, ikiwa imeandikwa maneno haya 'Talent is a Very Opportunity'.
Anasimulia video hiyo, aliiona Rais aliyepita wa Marekani, Donald Trump akaiposti katika Twitter yake, akaandika maneno yaliyosomeka hivi 'Amazing' na ilitazamwa na watu milioni tisa katika mtandao huo.
"Baada ya hapo walikuja wawakilishi wa Rais huyo Mstaafu, Trump waliniambia wameagizwa nipewe Sh5 milioni, nikaenda moja kwa moja kwenda kuanza ujenzi wa kiwanja changu ambacho kilikuwa Chanika," anasema Hadhara na kuongeza;
"Ukiachana na pesa, pia waliniambia wanataka kuingia udhamini na mimi wa miaka 10 kupitia kampuni ya Nike, walipitia wizarani, ila kilichoendelea sijui, sijawaona hadi leo."

Anaulizwa kuhusu nyumba yake kama imeisha au la, naye akajibu; "Bado ndiyo maana naomba msaada sio wa kunipa pesa, wanisaidie vifaa vya ujenzi, umri unaenda kwa sasa nina miaka 36, naumwa miguu katika nyayo na vidole vya miguuni, itafikia hatua nitashindwa kucheza kabisa, ndiyo maana natamani nimalizie nyumbani yangu, ili nipate sehemu ya kuishi na watoto wangu.
"Nina watoto wawili, mmoja wa kiume ana miaka 19 pia kapata mtoto, hivyo nina mjukuu, ndiyo maana natamani ifikie hatua niachane na kazi hiyo ili nifanye hata biashara nitulie. Kupitia hiki kipaji cha kuchezea mpira, kinaendesha maisha yangu, maana nilianza nikiwa mdogo, hivyo sina kazi nyingine zaidi ya hiyo."
HARMONIZE, ALIKIBA
Msanii wa Bongo Fleva, Rajab Abdul 'Harmonize' alimchangia madirisha na Hadhara anasimulia; "Nilikutana na Harmonize Zanzibar, nadhani ilikuwa ni michuano ya Kombe la Mapinduzi, akaniona akasema tushindane kuchezea mipira, nikamshinda ndipo akaniambia nitaje zawadi ninayoitaka, nikamwambia anilipie madirisha na alifanya hivyo, namshukuru kwa moyo wake wa upendo."
Mbali na Harmonize kumchangia madirisha, lakini anamtaja mkali mwingine wa muziki nchini, sanii mwingine wa Bongo Fleva, Ali Kiba jinsi alivyokuwa anamshauri kufanya vitu vya kimaendeleo, anapokuwa anapata pesa.
"Ndio maana pesa ambazo nilikuwa nafanya shoo mtaani, ama nikialikwa ndani na nje, nilikuwa nawekeza katika nyumba," anasema.

DK JAKAYA KIKWETE
Anasema Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete amekuwa msaada mkubwa katika maisha yake kwa kumshika mkono, pindi anapokumbana na magumu.
"Nakumbuka mwaka jana, mdogo wangu alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), tulikuwa tunadaiwa Sh700,000 akatulipia baada ya kumpigia simu nimekwama," anasema Hadhara na kuongeza;
"Jambo lingine alilonishauri, aliniambia kitu gani nimefanya kupitia kipaji changu, nilimwelezea najenga, alisema nisije nikathubutu kuuza nyumba hiyo, pia aliwahi kunikaribisha nyumbani kwake, ndiyo maana nasema namwona kama baba yangu."
MTOTO WA MUSEVENI
Anasema mtoto wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye ni Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amekuwa akiandaa sherehe anazokuwa anamwalika, ili kuonyesha kipaji chake.
"Japo ni muda mrefu kwa sasa sijaonana naye, ila kipindi cha nyuma, alikuwa ananialika mara kwa mara kwenda Uganda kukiwa na sherehe, pia namshukuru sana, maana pesa ambayo nilikuwa naipata nalea watoto wangu," anasema.
Kuhusu watoto, Hadhara anafichua kwa nini anawalea mwenyewe; "Mzazi mwenzangu alifariki dunia, hilo pia linachangia niwe na msongo wa mawazo."
Baada ya kuulizwa kama anasumbuliwa na wanaume kutokana na kujulikana kwake, mwanadada huyo kwanza anacheka kisha kujibu kwa upole;
"Wanaume hawawezi kunisogelea, kwani wengi wao wanataka kulelewa, ndiyo maana niliumia sana baada ya kumpoteza baba watoto wangu, nilikuwa natafuta naye, kutokana na kazi zangu nimezungukwa na wanaume."
Anaongeza kwa kusema; "Nikimaliza kazi zangu, navaa kama mwanamke, ukinikuta nimepiga gauni, nimepaka na wanja, huwezi amini, ndiyo maana nasuka, navaa hereni pia ni mama."
Kitu kinachomuumiza anasimulia ni jinsi wanawake wenzake mtaani wanavyomchukulia kama mwendawazimu, anataka wafahamu kile ni kipaji chake na anafanya kazi ya kuwatafutia watoto wake chakula na yeye kuishi.
"Nashangaa kuona wanaume wananiunga mkono, ila wanawake ndio wanaonidharau zaidi mtaani, nikiwa nacheza huwa nachafuka, basi wananiona kama chizi."

STAA MASKINI
Kitaa kwao, wamemtunga jina kama Ronaldo a.k.a CR7 Mwanamke Staa Maskini, naye anakubaliana nalo, kulingana na mazingira anayoyapitia.
"Hawajakosea ninafahamiana na watu mbalimbali wakubwa ndani na nje, lakini maisha yangu ni ya chini, ingawa kuna kejeli wanazifanya zinaniumiza moyo. Wapo watu wanaoniita mwalimu wa mpira wa Aziz Ki, lakini hilo sikubaliani nalo, mimi fundi wa kuchezea mpira, Aziz KI wa Yanga anafunga na anajua kuupiga kwelikweli uwanjani, hivyo sistahili sifa hiyo".
Anasimulia jinsi mwanamitindo, Hamisa Mobeto alivyomkutanisha na Stephane Aziz Ki, lakini akaishia kumpungia mkono, kutokana na kushindwa kuelewana lugha.
"Hamisa alinipeleka kwa Aziz Ki, lakini nikaishia kumpungia mkono, kwani lugha ambayo anazungumza (Kifaransa) nikawa simwelewi," anasema, huku akicheka.
KAIZUNGUKA AFRIKA
Kupitia kipaji chake, amekwenda kupiga shoo katika nchi mbalimbali, anazitaja Gabon, Cameroon, Ethiopia, Afrika Kusini, Nigeria, Tunisia, Malawi, Kenya, Msumbiji, Botswana na Uganda.
"Kuna kipindi nilialikwa na mastaa wa soka kama Nwanko Kanu, Samweli Etoo, Patrick Mboma, kitu ambacho sikuwahi kukiwaza kabisa katika maisha yangu na walishangazwa na kipaji nilichonacho.
ANA TUZO YA AFRIKA
Aliwahi kumaliza mshindi wa tatu, tuzo za watu wenye vipaji vya kuchezea mipira inayojulikana kama 'FreeStyle ' ilifanyika Nigeria.
"Nina tuzo ambayo niliiwakilisha Tanzania katika mashindano makubwa ya Afrika, ndiyo maana namwomba Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mpenda michezo, atuunge mkono watu kama sisi."
Anasema ikitokea mashindano hayo yakafanyika kwa mwaka huu, haoni kama anaweza akashiriki, kutokana na hali ya afya anavyojisikia.
HADHARA NI NANI?
Licha ya kutopenda kuweka umri wake hadharani, lakini Hadhara ni mtoto wa kwanza katika familia yenye ndugu watatu akiwamo wadogo zake, Halwie na Amina na anasema alisoma Shule ya Msingi Bwiwingu, iliyopo Chalinze, Pwani na kuhitimu mwaka 2004 na kujitosa kwenye mishemishe za maisha na kusaka maisha ikiwamo kutumikia kipaji chake cha soka kabla ya kujaliwa watoto alionao Hamoud na Faith.
Timu aliyowahi kuichezea ni Home Boys (Cossovo) ya kwao Chalinze enzi za chandimu na alikuwa akicheza na wavulana, kisha kuendelea kujifua kupiga danadana kwa ustadi hadi kutoboa na kujipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.