Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Elly Sasii anatabasamu, hana hofu anakunywa juisi

JICHO Pict

Muktasari:

  • Anatushangaa sisi ambao tunamshangaa yeye akiwa yuko mahala fulani sasa hivi akiwa na glasi yake ya mvinyo akiwa hana hofu. Katika akili alijua kwamba kitafanyika hiki, kisha kitatokea kile, halafu kitakuwa hivi. Sisi ndio ambao tulikuwa tumemsahau na akili yake.

MDOGO wangu Elly Sasii hana hofu. Anatushangaa sisi ambao tunamshangaa. Anatushangaa sisi ambao tunamsifia mwamuzi wa pambano la pili la Singida Black Stars dhidi ya Simba, Ahmed Arajiga ambaye alichezesha vizuri pambano la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho pale mkoani Manyara.

Anatushangaa sisi ambao tunamshangaa yeye akiwa yuko mahala fulani sasa hivi akiwa na glasi yake ya mvinyo akiwa hana hofu. Katika akili alijua kwamba kitafanyika hiki, kisha kitatokea kile, halafu kitakuwa hivi. Sisi ndio ambao tulikuwa tumemsahau na akili yake.

Ndani ya siku tano tu, mambo yamekuwa mengi. Sasii alichezesha pambano la Ligi Kuu kati ya Simba na Singida Black Stars, akavurunda. Halafu likaja pambano la Simba dhidi ya Singida Black Stars tena pale Manyara, Arajiga akachezesha vizuri.

Pambano la kwanza Sasii alilivuruga kiajabu tu. Aliwanyima Singida penalti mbili za halali. Kila mwanadamu ambaye alikuwa anatazama pambano lile alishangaa.

JICH 01

Binafsi huwa nina tabia ya makusudi ya kuchati na waamuzi wachache ninaowachagua kuhusu uamuzi wao uwanjani. Siwezi kuwataja kwa sababu kwao ni kinyume cha maadili. Wapo wanaonifafanulia kuhusu uamuzi wao. Wengine wanakiri kukosea.

Kamanda wangu Sasii aliamua kunifungia ukurasa wake ili nisiwe namuona. Kifupi watoto wa mjini huwa wanasema aliamua ‘kuniblock’ baada ya kushindwa kujibu maswali yangu kadhaa. Hakuwahi kuwa na majibu kama ambavyo hawezi kuwa na majibu ya pambano ambalo alivurunda.

Hili pambano la Ligi Kuu, Sasii alilivurunda kiutata kama ambavyo amewahi kuvurunda mechi nyingi za ligi hiyo kwa staili kama hiyo. Kulikuwa na kitu moyoni ambacho hatuwezi kukithibitisha moja kwa moja, lakini ni wazi kwamba alikuwa ameharibu utamu wa mchezo.

JICH 02

Mwisho wa siku nadhani alifahamu kwamba ligi yetu ilikuwa inaelekea ukingoni. Unapovurunda mechi kama ile iwe kwa namna yoyote kinachofuata kwa mwamuzi wa Kitanzania ni kufungiwa kwa miezi mitatu tu. Kisha mambo yanaendelea kama kawaida. Tumeshuhudia kwa wengine kadhaa.

Kesho tutakua Juni 2 na kama akifungiwa, Sasii atakuwa huru Septemba Mosi. Kwa sababu ligi yetu imechelewa kumalizika na hadi mwishoni mwa mwezi huu, itakuwa inachezwa ina maana tutarajie msimu ujao utaanza Septemba Mosi. Ina maana Elly Sasii atakuwa anatumikia kifungo chake wakati wa likizo.

Kifungo hakitakuwa na athari yoyote kwake. Msimu ujao atakuwapo uwanjani kama kawaida. Ni kama ambavyo amewahi kutumikia adhabu hii mara kadhaa na alirudi uwanjani kuendelea kuyafanya madudu ambayo aliyafanya katikati ya wiki.

JICH 03

Mambo ya aina hii yamewahi kufanywa na waamuzi ambao hawana mipango ya muda mrefu katika maisha yao ya soka. Walijua kwamba wao huwa hawasafiri kwenda kuchezesha mechi za kimataifa kama ilivyo kwa Arajiga. Hawana cha kupoteza. Labda ndio maana walifanya waliyofanya kwa makusudi.

Arajiga anafahamu kwamba ujinga wowote ambao anaweza kuufanya basi atapoteza zile safari zake za kwenda kucheza mpira ndani ya Afrika kwa sasa. Ni kitu cha kawaida kusikia Arajiga anacheza pambano la Botswana dhidi ya Algeria. Hauwezi kuwasikia baadhi ya waamuzi wakifanya hivyo na nina pengine hata wao wenyewe wamekata tamaa ya kufanya hivyo, ndio maana wanatufanyia wanachokifanya. Wanavurunda kwa makusudi mechi za Ligi Kuu na kuadhibiwa kishkaji na mambo kuisha.

Madhara yake nini? Kitu cha kwanza kabisa ni kuugeuza mpira wetu kuwa kichekesho. Ni kweli kwamba waamuzi huwa wanakosea, hata huko Ulaya huwa wanakosea lakini muda mwingi huwa wanakosea katika namna ambayo wanatuachia ubishi.

JICH 04

Huwa wanakosea katika namna ambavyo wakati mwingine wanalazimika kusaidiwa na VAR. Mfano ni kwamba hata Arajiga mwenyewe alikosea kutompa kadi nyekundu Ellie Mpanzu katika pambano la juzi. Hata hivyo, wote tulikubaliana kwamba Arajiga alipaswa kupata msaada wa VAR ili amtoe nje Mpanzu. Hata hivyo, kwa sasa katika michuano yetu ya ndani hatutumii teknolojia hiyo.

Sasii alifanya makosa katika kitu ambacho hatukuhitaji kutumia VAR. Hata Simba wenyewe waliweka ushabiki kando na kukiri kwamba Singida walistahili penalti zao. Wasingeweza kulisema hili hadharani, lakini katika vikao vya kahawa walikuwa wanalisema hili.

Madhara mengine ni yapi? Kuna kampuni ambazo zimewekeza pesa nyingi katika kudhamini mpira wetu, lakini wanaweza kukosa imani na namna ambavyo unaendeshwa. Tunakosa weledi ambao unaweza kupelekea baadhi ya kampuni kuamua kujiondoa na vichekesho vyetu.

Na tukiachana na hilo hata kampuni la kubashiri nazo zitagundua kwamba mpira wetu ni wa maigizo. Wataacha kuziweka mechi zetu katika majukwaa yao, lakini uwezekano wa wao kujiondoa pia katika udhamini wao wa timu mbalimbali nchini.

JICH 05

Hapo hapo tukumbuke namna ambavyo tunazidi kuwafanya mashabiki wa soka nchini kulipenda zaidi soka la Ulaya. Tayari tunajua kwamba mashabiki wengi hawaendi katika viwanja vya soka kwa sababu mbalimbali ikiwamo utaratibu mbovu wa kuingia uwanjani.

Lakini mashabiki wanapenda soka la Ulaya kwa sababu hawajui kinachoweza kutokea uwanjani. Huku kwetu mechi zinatabirika, hasa zile za wakubwa kwa sababu tunajua kuna kina marefa wanakuja na matokeo yao mfukoni.

Na mwisho wa siku adhabu ambazo zinatolewa kwao, zinawafanya watabasamu na wasiwe na hofu. Fikiria madhara makubwa ambayo Sasii ameyasababisha, lakini adhabu yake ni kufungiwa kwa miezi mitatu tu. Kwanini awe na hofu?!

Kama angekuwa ni mwamuzi ambaye anateuliwa na CAF au FIFA kuchezesha mechi zao angeweza kuwa na hofu. Angekuwa na hofu ya kukosa kufunga mkanda wa kiti cha ndege pamoja na kupokea dola zake kutoka kwa wakubwa.

Kwa sasa hawezi kuwa na hofu. Anajua kwamba yeye ni mwamuzi wa hapahapa ndani. Anasikiliza hizi kelele zetu kwa sasa anaishia kutabasamu na kunyanyua glasi yake ya mvinyo. Alichotaka kimekuwa na Septemba mwaka huu huu atakuwa uwanjani akichezesha pambano la Ligi Kuu.