MAYELE: Mwamba aliyeweka heshima Afrika

Muktasari:
- Sio kubeba ubingwa huo wa kwanza katika maisha yake ya soka, lakini mwamba amemaliza kinara wa mabao katika michuano hiyo kama alivyofanya 2022-2023 alipokuwa Yanga na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika alipokosa taji, ila alimaliza kinara wa mabao.
NAMBA haziongopi. Ndio, straika wa zamani wa AS Vita ya DR Congo na Yanga anayekipiga kwa sasa Pyramids ya Misri, Fiston Mayele amethibitisha kuwa mwamba, baada ya juzi usiku kuandika rekodi ya kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Sio kubeba ubingwa huo wa kwanza katika maisha yake ya soka, lakini mwamba amemaliza kinara wa mabao katika michuano hiyo kama alivyofanya 2022-2023 alipokuwa Yanga na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika alipokosa taji, ila alimaliza kinara wa mabao.
Kuibeba Pyramids akiipa taji la kwanza la michuano ya Afrika tangu kuasisiwa 2008, kumemfanya Mayele kuendelea kuthibitisha kuwa mmoja wa washambuliaji bora zaidi Afrika kwa sasa ndani ya misimu mitatu mfululizo ya mashindano ya ndani hadi kimataifa.
Mayele ambaye ametumika misimu miwili Pyramids na kabla ya kutua aliitumikia Yanga kwa misimu miwili ambayo alicheza kwa ubora na kuipa mataji na sasa anasumbua Misri, ligi namba moja kwa ubora Afrika.

Akiisaidia Pyramids kutwaa taji ameibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa akipachika mabao sita kambani huku akiwa nayo jumla tisa - matatu akifunga hatua ya awali. Ubingwa alioutwaa ilikuwa ni fainali yake ya pili kucheza kwenye mashindano ya CAF baada ya 2022/23 akiwa Yanga alipoibuka mfungaji bora akiingia kambani mara saba.
Kimataifa Mayele amecheza mechi 13 zenye dakika 1088 akifunga mabao tisa kati ya hayo matatu alifunga hatua ya awali na sita ndiyo yaliyompa tuzo ya ufungaji bora Ligi ya Mabingwa Afrika.

ANACHOKIFANYA
Katika msimu wa kwanza 2023-2024 akiwa na Pyramids, Mayele maarufu kama ‘Mzee wa Kutetema’ alicheza mechi 43 za mashindano yote na kufunga mabao 21 akiasisti tano.
Licha ya ugeni wa ligi hiyo msimu wa kwanza namba zilionekana kumbeba akicheza mechi 32 ambazo alitumika kwa dakika 2365, akafunga mabao 17 na kutoa asisti nne.
Michuano ya kimataifa alicheza mechi saba akifunga bao moja na asisti moja akitumika kwa dakika 549 na alicheza mechi tatu michuano ya Kombe la Misri akifunga mabao mawili dakika 241 na michuano ya Egyptian Super Cup alicheza mechi moja akitumika dakika zote 90 hakufunga wala kutoa asisti.
Ubora aliouonyesha msimu wa kwanza ulijenga imani kwa benchi la ufundi kuendelea kumuamini na kumpa nafasi.
Msimu huu amecheza mechi 38, akafunga mabao 18, asisti mbili na akitumika kwa dakika 3018. Mayele amecheza mechi za ligi 17, amefunga mabao sita na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao. Egyptian Super Cup msimu huu amecheza mechi moja akitumika kwa dakika 90, hakufunga wala kuasisti na michuano ya Kombe la Misri amecheza dakika 64 akifunga bao moja.

YANGA
Mayele aliitumikia Yanga kwa misimu miwili tangu 2021/2022 akitokea AS Vita ya DR Congo, akawa mhimili mkubwa wa safu ya ushambuliaji katika michuano ligi na mashindano ya CAF
Katika msimu wa kwanza, staa huyo aliyesifika kwa staili ya kushangilia kwa kutetema alishika namba mbili kwa vinara wa upachikaji mabao Ligi Kuu akifunga 16 nyuma ya George Mpole aliyeifungia Geita Gold mabao 17. Hakuishia hapo, alifunga mabao mawili katika Kombe la Shirikisho (FA na msimu huohuo alifunga bao moja kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
Ikumbukwe pia kabla ya kudondokea katika Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga ilianzia kwenye Ligi ya Mabingwa na huko Mayele alifunga mabao saba akitupia hat-trick mbili dhidi ya Zalan ya Sudan na moja dhidi ya Al Hilal katika sare ya mabao 1-1 kwa Mkapa kabla ya kutolewa kwa bao 1-0 ugenini, Omdurman, Sudan.
Pia aliitungua Simba mabao mawili katika Ngao ya Jamii msimu huo mechi iliyomalizika kwa Yanga kushinda 2-1 na pia kwenye FA ambako Yanga iliitwaa taji hilo akifunga mawili.
Kiufupi msimu huo Mayele alifunga jumla ya mabao 35 kwenye Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika, FA na Ngao ya Jamii.
Kwa maana hiyo katika misimu miwili ambayo alicheza Yanga alifunga jumla ya mabao 54.
Baada ya mafanikio Yanga nyota huyo alitimkia Pyramids ambako ameiwezesha kucheza fainali ya Kombe la Dunia 2029.

MSIKIE MWE-NYEWE
Akizungumza jana na kituo cha redio cha EFM, Mayele alitaja siri ya mafanikio kuwa ni kujiamini huku akidai ataendelea kufanya hivyo na hatarajii kuporomoka. Pia alisema kuwa alipokuwa anasaini mkataba na Pyramids aliomba apewe miaka miwili aonyeshe uwezo wake na ndicho kinachotokea sasa.
“Siri kubwa ni kujiamini. Najiamini kwenye kazi ninayoifanya. Katika maisha kwenye kila jambo unatakiwa kujiamini,” alisema.
“Mwaka wa kwanza nimechukua Egypt Cup lakini pia kwenye ligi tumekosa ubingwa kwa pointi mbili tu, kuna vitu vinaendelea huenda tukapata ni mafanikio makubwa kwangu na jana (juzi) nimekuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Ni furaha kubwa kwangu kwa sababu tumetwaa Ligi ya Mabingwa sio rahisi timu hii niliyopo tulikuwa tunapewa nafasi ndogo tumepambana sasa ni mabingwa. Namshukuru Mungu,”
“Kila mtu amejitoa kwa jasho na damu kuhakikisha tunafikia hapa, nina wengi wa kuwashukuru familia na meneja wangu Yasmin ...kubwa zaidi naweza kusema nina furaha sana.”