Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morocco: Chimbo la mastaa Bara

MASTAA Pict

Muktasari:

Kwa misimu kadhaa sasa, kumekuwa na wimbi la nyota wa Ligi Kuu Bara kupata dili nje ya nchi na kuendelea kuipeperusha bendera ya Ligi hiyo na hata ile ya Wanawake.

NYOTA mbalimbali wa Ligi Kuu Bara na hata wale wa timu za Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) wameendelea kuteka soka nje ya mipaka ya nchi kutokana na viwango bora wanavyovionyesha, hali inayoonyesha wazi soka la Bongo limepiga hatua kubwa zinazovutia maskauti wengi kuvutika nao.

Kwa misimu kadhaa sasa, kumekuwa na wimbi la nyota wa Ligi Kuu Bara kupata dili nje ya nchi na kuendelea kuipeperusha bendera ya Ligi hiyo na hata ile ya Wanawake.

Lakini kuna chimbo moja limekuwa kimbilio la nyota wengi waliong’ara au kutamba katika soka nchini, hata kama baadhi yao wameenda na kurudi, ila haiondoi ukweli kwamba ni sehemu inayotolewa macho na maskauti kwa ajili ya kuja kufuata vipaji vya kwenda kucheza huko.

Chimbo hilo si jingine ni Morocco. Kwa muda mrefu sasa nyota kadhaa wanaotamba nchini katika Ligi hizo kubwa wamekuwa wakienda kukipiga huko, ambako kwa msimu huu, tayari tumeshuhudia wachezaji Selemani Mwalimu ‘Gomez’ na Stephane Aziz KI wamejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco.

Nyota hao waliokuwa wakikipiga Yanga na Fountain Gate sio wa kwanza kutoka Ligi Kuu Bara na kwenda nchini humo kucheza soka la kulipwa na hapa chini Mwanaspoti linaelezea mastaa wengine waliotoka hapa na kwenda katika nchi hiyo.

MASTA 01

SELEMAN MWALIMU ‘GOMEZ’

Mshambuliaji huyu ndiye wa kwanza kwa msimu huu kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco baada ya kuonyesha kiwango bora wakati akiwa na Fountain Gate, ambapo hadi anaondoka dirisha dogo la Januari mwaka huu, alikuwa amefunga mabao sita ya Ligi Kuu Bara.

Nyota huyu alijiunga na Fountain Gate akitokea Singida Black Stars iliyomsajili akitokea KVZ ya Zanzibar, ambako msimu uliopita ndiye aliyekuwa mfungaji bora kwa kufunga mabao 20 na kutoa asisti saba katika mechi 27, kati ya 30, alizocheza.

Tayari mchezaji huyo ameanza kuitumikia timu hiyo na juzi kati aliingia uwanjani kukabiliana na mabeki wa Sevilla ya Hispania katika pambano la kirafiki la kimataifa lililopigwa kwenye Uwanja wa Mohammed V, Casablanca Morocco. Katika mchezo huo Sevilla ilishinda bao 1-0 na Gomez aliingia dakika 10 za mwisho za mchezo huo.

MASTA 02

STEPHANE AZIZ KI

Aziz KI amekwenda Morocco akijiunga na Wydad Casablanca akimfuata Seleman Mwalimu ‘Gomez’ baada ya kuachana na Yanga aliyoitumikia kwa misimu mitatu, tangu ajiunge na kikosi hicho rasmi Julai 15, 2022, akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Nyota huyo ameondoka Yanga akiacha rekodi ya aina yake baada ya kufunga jumla ya mabao 54 na kuasisti mengine 32, katika mashindano yote.

Msimu uliopita alishinda tuzo ya mfungaji bora na MVP wa Ligi Kuu baada ya kuhusika katika mabao 29 katika mechi 30 za Ligi akifunga mabao 21 na kuasisti mengine manane.

Kwa misimu mitatu Aziz KI ametwaa makombe tisa akiwa na kikosi hicho yakiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara, mengine mawili ya Kombe la Shirikisho (FA), Ngao ya Jamii mbili, Kombe la Muungano, Toyota na Mapinduzi yote akichukua moja kila shindano.

Mbali na mataji hayo, pia Aziz KI ameondoka nchini akiwa amebeba tuzo mbili za maana kubwa, ikiwamo ya Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa msimu uliopita, hapo ni tofauti na za Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu Bara zinazoendelea kutolewa.

Katika kipindi cha misimu yake mitatu, Aziz KI amefunga jumla ya ‘hat-trick’ tano ambapo nne kati ya hizo ni za Ligi Kuu Bara na moja ni ya michuano ya Kombe la Shirikisho la (FA), aliyoifunga msimu huu walipoichapa Stand United mabao 8-1.

Tayari Aziz KI ameshatumika akitokea benchini katika kipindi cha pili cha mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya FC Porto ya Ureno iliyopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Mohammed V ambayo Wydad ilipoteza kwa bao 1-0.

MASTA 03

SIMON MSUVA

Ni miongoni mwa wachezaji wa awali kutoka Ligi Kuu Bara kwenda kucheza soka la kulipwa Morocco akifanya hivyo mwaka 2018 alipouzwa na Yanga.

Msuva ni kati ya wachezaji waliofanya vizuri wakiwa wanacheza nchini, ambapo anakumbukwa zaidi msimu wa 2014-2015, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi cha Yanga, alichokifungia jumla ya mabao 17 na kutwaa Kiatu cha Dhahabu.

Kama haitoshi, msimu wa 2016-2017, akaibuka tena mfungaji bora akiwa na Yanga baada ya kufunga mabao 14, sawa na nyota wa zamani wa Ruvu Shooting, Abrahaman Mussa, ambapo kuanzia hapo akapata neema ya kuhitajika na klabu mbalimbali za nje.

Baada ya hapo, nyota huyo akajiunga na Difaa El Jadida na Wydad Casablanca zinazoshiriki Ligi Kuu Morocco (Batola Pro), kabla ya kutimikia Al Qadsiah FC, Al-Najma SC zote za Saudi Arabia, JS Kabylie ya Algeria na Al-Talaba SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq.

MASTA 04

NICKSON KIBABAGE

Kibabage anayeichezea Yanga kwa sasa, aliwahi kucheza soka la kulipwa Morocco katika timu ya Difaa El Jadida kwa mkataba wa miaka miwili, ingawa mambo yalienda tofauti na yalivyokuwa matarajio ya wengi baada ya nyota huyo kurudi nchini.

Nyota huyo ambaye ni zao la akademi ya Mtibwa Sugar, amewahi kucheza timu mbalimbali, zikiwamo Fountain Gate, KMC FC na Singida Big Stars, huku akiwa ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja.

MASTA 05

MAKA EDWARD

Kwa sasa Maka ambaye anacheza katika kikosi cha maafande wa JKT Tanzania, aliwahi kwenda Morocco kujiunga na Athletico De Tetuan ya huko, ambayo ina uhusiano mkubwa na Atletico Madrid ya Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’.

Hata hivyo, kabla ya kwenda Morocco, kiungo huyo aliyewahi kusaini Simba na Yanga kwa wakati mmoja kabla ya timu hizo kuafikiana, alienda kucheza Latvia kisha kurejea kimya kimya nchini, huku akiichezea pia Toto Africans ya jijini Mwanza.

MASTA 06

SHAABAN CHILUNDA

Chilunda aliyewahi kucheza soka Hispania katika timu za CD Tenerife na Club Deportivo Izarra, ni miongoni wa wachezaji waliowahi kwenda Morocco na kujiunga na Moghreb Athletic de Tetouan, baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na Azam FC.

Kwa sasa nyota huyo anaichezea KMC FC aliyojiunga nayo katika dirisha dogo la Januari 2025, baada ya kutokuwa na timu tangu Julai 1, 2024 alipoachana na Simba, ambako hadi sasa amefunga mabao mawili ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho.

MASTA 07

CLATOUS CHAMA

Kiungo huyu aliyejizoelea umaarufu mkubwa nchini, kwa sasa anaichezea Yanga baada ya kumaliza mkataba wake na Simba aliyoitumikia kwa vipindi mbalimbali tangu alipojiunga nayo mwaka 2018, akitokea klabu ya Lusaka Dynamos ya kwao Zambia.

Kiwango kizuri alichokionyesha kilimuondoa Simba mwaka 2021 aliponasa dili la kujiunga na RS Berkane ya Morocco, ingawa mambo yalikuwa ni magumu kwake na kurejea 2022 na kukikutumikia kikosi hicho misimu miwili tu hadi alipojiunga na Yanga.

Msimu wa kwanza kwake katika Ligi Kuu Bara baada ya kurejea, alifunga mabao manne na msimu uliopita alifunga saba nyuma ya kiungo wa zamani Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyemaliza kinara ndani ya kikosi hicho kwa kufunga mabao 11.

MASTA 08

TUISILA KISINDA

Winga huyo aliyejizoelea umaarufu mkubwa hapa nchini, alijiunga na Yanga Agosti 17, 2020, akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo, ambapo alipata dili la kutua RS Berkane ya Morocco iliyoweka kiasi cha dola 300,000 sawa na Sh693 milioni.

Kiasi hicho cha fedha kinatajwa kilikuwa kikubwa kwa wakati huo kwa Yanga kukipata kwa mchezaji huyo, kwani Simon Msuva aliyeuzwa Difaa El Jadida ya Morroco pia kwa dola 80,000 sawa na Sh184 milioni, ndiye aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo.

Heritier Makambo anayeichezea Tabora United msimu huu, aliwahi pia kuichezea Yanga kwa nyakati tofauti, aliuzwa kwenda Horoya AC ya Guinea kwa dola 70,000, ambazo kwa wakati huo zilikuwa ni sawa na Sh190 milioni, kisha kurejea tena nchini.


WENGINE

Mbali na nyota wa kiume, katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), kuna mastaa kiadhaa walioenda kucheza soka la kulipwa Morocco, akiwamo Enekia Kassonga ‘Lunyamila’ ambaye baada ya kutamba na Alliance Girls na Ruvuma Queens alipata dili la kwenda nchini humo mwaka 2021 na kujiunga na Ausfaz Assa-Zag.

Miaka miwili baadaye alitimkia Ukraine kuitumikia Kryvbas Kryvyi Rih kisha kwenda Saudia kukupiga Eastern Flames na sasa yupo Mexico akiitumikia Zamatlan.

Diana Msewa ni mchezaji mwingine wa soka la wanawake aliyeenda Morocco akifuatana na Enekia kujiunga na Ausfaz Assa-Zag aliyekaa misimu miwili kisha kutimkia Uturuki akianzia kikosi cha Amed kisha Trabzonspor.

Mkongwe Mwanahamis Omar ‘Gaucho’ aliyewahi kutamba na Mlandizi Queens na Simba Queens, ni kati ya wachezaji wa kwanza wa kike kwenda kucheza Morocco akijiunga na Chabab Atlas kabla ya hivi karibuni kurejea Msimbazi.

Pia kuna beki Zuwena Aziz amewahi kupita klabu kadhaa zikiwamo Kigoma Sisters, Baobab Queens, Thika Queens ya Kenya, Lady Doves ya Uganda, aliwahi kwenda kujichimbia Morocco alipojiunga na klabu ya Najah FC ya Morocco kisha kurejea hivi karibuni kuitumikia Ceasiaa Queens kabla ya kujiunga na Tausi aliyonayo kwa sasa.