Dullah Mbabe simu tatu ndizo sababu ya kipigo ulaya

DHARAU, kejeli na matusi sasa imekuwa sehemu ya maisha ya bondia Abdallah Pazi maarufu zaidi kama Dullah Mbabe kutokana na magumu anayopitia katika mchezo wa ngumi za kulipwa.

Dullah Mbabe ameshushwa thamani tangu alivyochezea kichapo mbele ya Twaha Kiduku, kabla ya yule Mkongomani, Tshimanga Katompa kumtwanga hadi kumtoa udenda. Walirudiana mwaka jana jijini Arusha na kumfanya Mbabe kuwaambia viongozi wa ngumi nchini kwamba, hawampendi ndiyo maana hawakumlinda na kichapo tena.

Achana na hiyo, juzi ametoka kupigwa KO ya raundi ya nne nchini Uingereza na bondia Cullum Simpson, hali iliyosababisha kuwa gumzo katika vyombo vya habari kutokana na kipigo hicho.

Lakini hayo yakiendelea, dunia imesahau Dullah Mbabe ndiye aliyemaliza jina la Maneno Oswald ‘Mtambo wa Gongo’ baada ya kumchapa raundi ya tatu katika pambano la raundi sita.

Kisha mbele ya bondia mtata, Thomas Mashali (marehemu) akamchapa kwa pointi katika pambano raundi kumi ikiwa ni miezi michache tangu pambano lao la kwanza ambalo lilivunjika raundi tatu katika Ukumbi wa Friends Corner, Manzese, mwaka 2015.

Tanzania hakuna asiyemjua bondia Francis Cheka ‘SMG’, lakini hakuweza kufua dafu mbele ya Dullah Mbabe kutokana kukubali kipigo cha KO ya raundi ya sita katika pambano la raundi 12 ambalo lilikuwa la kuwania ubingwa wa mabara wa WBF.

Bondia huyo ni mmoja kati ya Watanzania wachache walioweka rekodi ya kushinda nje ya mipaka ya Tanzania, mwaka 2016 alifanikiwa kumtandika, Andrey Kalyuhnyy raia wa Urusi kwa KO ya raundi tatu katika pambano la raundi sita lililofanyika Shanghai nchini China.


Hiyo ilikuwa mwanzo tu wa Dullah Mbabe kuanza kufanya vizuri nje ya mipaka ya Tanzania kwani mwaka 2019, alifanikiwa kushinda ubingwa wa WBO Asia Pacific kwa TKO ya raundi ya tatu dhidi ya Mchina, Zulipikaer Maimatiali katika pambano lililofanyika TSSG Qingdao, China.

Mbabe mwenye rekodi ya kucheza mapambano 50 mpaka sasa ikiwa sawa na raundi 232, amefanikiwa kushinda 34, kati ya hayo 29 ni kwa KO, amepigwa mara 14, kati ya hizo ni mara tatu ndiyo ameonja kichapo cha KO, huku akitoka sare mara moja.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Dullah Mbabe ambaye anashika nafasi ya tatu katika mabondia 19 wa uzani wa super middle huku duniani akiwa wa 217 katika mabondia 1535, juu ya kile kilichompata Uingereza na kupelekea kuwa gumzo zito nchini.

Mbabe ameanza kwa kusimulia kuwa, baada ya kupata pambano hilo la nchini Uingereza alipigiwa simu za kutakiwa kuliuza.

“Unajua watu hawajui, ila lile pambano nilipigiwa simu nikitakiwa kwenda kuuza. Kwanza nilipigiwa na bondia mwenzangu hapa ndani na kuniambia kuna mtu yupo Ghana anataka namba yangu, nikamwambia mpe nitaongea naye.

“Jamaa wa Ghana alivyonipigia akaniambia kuna mtu yupo Uingereza anataka kuongea na mimi, mpaka hapo sikuwa najua lolote, nilivyokuwa naongea na jamaa wa Uingereza, ndiyo alianza kuniambia suala la kuachia pambano.

“Lakini baada ya kumgomea ndiyo akaniambia watanipa Dola 1,000 sawa na Sh2.5milioni kabla ya kupanda ulingoni na baada ya kushuka wanipe Dola 7000 (Sh18 milioni).


“Binafsi nilimkatalia kuuza kwa sababu huwa siuzi mapambano, mimi kama kupigwa bora nikapigwe ndani ya ulingo, lakini siyo kuuza, baada ya kuwagomea wakaniambia nisipotaka nitapigwa na nikitaka nitapigwa, meseji zao ninazo.”

SWALI: Baada ya kuona hivyo ulichukua hatua gani?

JIBU: “Sikuweza kufanya lolote maana hata kule walinifuata lakini sikubadili msimamo wangu na ukizingatia nilikuwa kwao, ikabidi tusubiri muda wa pambano na kwenda ukumbini kwa ajili ya kupigana.

“Sasa baada ya kufika kule nikiwa na wakala wangu, hatujui walituwekea kitu gani katika chumba cha kubadilishia nguo maana wote tulipitiwa na usingizi mzito kabla ya kuja kuamshwa muda mchache kabla ya pambano, ilibidi nikapigane bila ya kufanya mazoezi mepesi kabla ya kupanda ulingoni.

“Kilichotokea kila mtu aliona, nikawa nimepoteza kwa KO, lakini bahati mbaya ikawa gumzo na kila mmoja kusema lake.

SWALI: Ulipata ugumu gani baada ya vyombo vingi kuripoti kupigwa kwako kuliko hata safari yako wakati unaelekea Uingereza?

JIBU: “Unajua kwanza vyombo vya habari ni muhimu katika kila eneo maana bila ya wao sisi hatuwezi kuwepo ingawa ilinishangaza kuona na hakuna chombo chochote ambacho kilitaka kujua safari yangu licha ya kuweka wazi safari yangu yote ila baada ya kupoteza pambano kule ndiyo ikawa gumzo.

“Hii inatengeneza mazingira ya kuwa wanafurahia kuona mtu akipoteza pambano ingawa nashukuru watu wa karibu hawakunitupa mkono kutokana na kunifariji kwao.

SWALI: Bondia mwenzako, Hassan Mwakinyo alitoa ujumbe mrefu katika Instagram baada ya wewe kupoteza na mwisho wa ujumbe wake amekwambia uache mihadarati na makundi ya ajabu, halafu ufanye kazi. Ni kweli unatumia mihadarati na una makundi ya ajabu?

JIBU: “Kwanza neno mihadarati lina maana gani? (akafanuliwa na mwandishi kwamba ni dawa za kulevya) hilo moja, halafu jambo la pili sina vikundi vya ajabu, lakini jambo la tatu situmii kilevi cha aina yoyote, yaani siyo mtumiaji kwa sababu kama ni pombe naweza kukaa mpaka miaka miwili bila ya kutumia ingawa kuna siku naweza kunywa bia zangu mbili au moja.

“Lakini kuhusu sijui mirungi sijawahi kabisa kutumia ila bangi siwezi kukataa kwa sababu niliwahi kuvuta nikiwa darasa la pili wakati nipo kwetu nasoma ingawa sasa watu wengi wanajua mimi navuta bangi au wanajua mimi muhuni sana.

“Binafsi mimi siyo muhuni sana wala mvuta bangi, mimi ni mtu wa kawaida kabisa, ndiyo maana nina mashabiki wengi na wala hujawahi kusikia nina skendo ya kumkaba mtu.

“Unajua kila mtu anaongea lake ila kama kuna mtu ameshaniona labda natumia hiyo mihadarati kama bangi basi alete ushahidi ingawa Waswahili wanasema anapokufa nyani miti yote huteleza, hivyo waache waongee.

“Kwangu ngumi ndiyo mchezo ambao umebadilisha mambo mengi kwangu maana nilipotokea na nilipo ni maisha ya tofauti, najua kuna watu wananiongelea vibaya, lakini hawafiki hata robo ya maisha yangu.

“Nataka nikwambie kwamba ninauheshimu sana huu mchezo kwa sababu nimetoka katika kukata mkaa na kuuza, nimetengeza sana majiko pale Kijitonyama na hadi bodaboda nimeendesha, hivyo siwashangai.

“Hawajui tu ila kwanza sijapanga, ninaishi kwangu, watoto wangu wanasoma ‘English Medium’ na nina usafiri wangu naweza kwenda ninapotaka wakati wowote, kwa ufupi siwezi kuwazuia watu kuongea wanachotaka.

“Binafsi bado naamini mchezo wa ngumi ndiyo umenifanya wanijue, umesababisha niende Ulaya mara nyingi na ndiyo umenipa mafanikio makubwa ya kimaisha.”

SWALI: Mashabiki wanasema umeisha kutokana na kupigwa sana, hii ipoje?

JIBU: “Nadhani anayesema nimeisha basi ni vyema akaja yeye tupande ulingoni tupigane ili ahakikishe nilivyoisha.”

SWALI: Una mipango gani kwa sasa?

JIBU: “Nawakaribisha promota yeyote anayeweza kuleta kazi nitafanya kwa sababu ngumi ndiyo maisha yangu,” anasema.