Dua Said asimulia balaa la usajili wa Wawa Simba

Muktasari:
- Hata hivyo, licha ya mafanikio yao uwanjani, baadhi ya mastaa wa soka wa zamani wamejikuta wakikumbwa na matatizo makubwa kutokana na maisha ya starehe, matumizi ya pombe, dawa za kulevya na mizunguko isiyofaa.
STAREHE na maisha ya kifahari ni baadhi ya mambo yanayohusishwa na wachezaji wa soka maarufu duniani.
Hata hivyo, licha ya mafanikio yao uwanjani, baadhi ya mastaa wa soka wa zamani wamejikuta wakikumbwa na matatizo makubwa kutokana na maisha ya starehe, matumizi ya pombe, dawa za kulevya na mizunguko isiyofaa.
Ingawa wakiwa uwanjani walikuwa ni shujaa na walioonyesha ustadi mkubwa, maisha binafsi baada ya kustaafu yamekuwa na changamoto kubwa.
Starehe zinazowezekana kwa wachezaji hao pamoja na shinikizo la umaarufu vimechangia kushindwa kudumisha maisha bora ya kifedha na kiakili, huku wengine wakiishi maisha ya dhiki na machungu.
Wachezaji wengi wa zamani licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kiufundi, walishindwa kudhibiti vyema hali zao za kifedha na kijamii kutokana na kujitosa kwenye starehe ambazo zilikuwa na madhara makubwa.
Yote haya unayapata katika gazeti hili lililofunga safari kwenda kwa staa wa zamani wa Simba, Dua Said, ambaye aliichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa.
Huku akiweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyeifunga Yanga mara nyingi, Dua anasimulia mikasa ya usajili, wakati wa uongozi wa Hans Pope yeye akiwa mjumbe wa kamati hiyo na kutaja sababu za mastaa wengi wa zamani kudumbukia katika dimbwi la umasikini.
KILICHO WA CHAKAZA MASTAA WA ZAMANI
Moja kati ya kilio kikubwa cha wachezaji wa zamani kuwa na hali mbaya za kimaisha, japokuwa sio wote, Dua anasema sababu kuu ni starehe.
"Huo ni mfumo wa maisha ambao mtu amejipangia na inatoka ndani ya damu ya mtu kwa sababu kuna vitu vinaweza kukuweka sehemu mbaya ya maisha.
"Starehe siku zote katika maisha huwa zinaharibu na ni kitu ambacho unaweza ukaamua wewe mwenyewe kuacha kwa sababu hakuna anayekushawishi kuvuta au kunywa, hivyo ni wewe mwenyewe na malengo yako," anasema na kuongeza:
"Kipindi unacheza ndani ya timu lazima uwe na malengo kuwa ndani ya miaka kadhaa unataka kujenga au vipi na familia yako iishi vipi baada ya wewe kumaliza soka. Kumshirikisha Mungu (ni muhimu) mimi mpaka sasa sijui ladha ya pombe, sigara au chochote kisichofaa. Ulaji wangu sio wa mafuta mengi ili niwe na nguvu za kufanya majukumu yangu."

BALAA USAJILI WA WAWA
Dua anasema kuwa aliwahi kuwa kwenye kamati ya usajili ya Simba iliyokuwa ikiongozwa na hayati Hans Pope.
Mchezaji huyo mkongwe anasema moja kati ya mambo ambayo yaliijenga Simba kuwa na mastaa wenye uwezo mkubwa wa kuipambania timu ni kamati bora ya usajili yenye uwezo mkubwa wa kujua soka na mapenzi ya dhati na timu, jambo ambalo kwa sasa ni nadra kuliona.
"Nakumbuka usajili uliokuwa mgumu zaidi, kwani katika kamati hiyo mimi ndiye nilikuwa mchezaji wa zamani na wengine wakiwa na akili kubwa ya mpira.
"Sitasahau tulivyopata shida kwa mchezaji mmoja hivi, alitakiwa asajiliwe na baadhi ya viongozi hawakumtaka. Kwa hiyo mwenyekiti Hans (Pope) akanichagua niende Uwanja wa Mkapa nikamtazame," anasema Dua.
"Kweli nikaenda na nikamuona ufundi wake na hapo niliporudi kwenye kamati nikawapa taarifa kuwa mchezaji yuko vizuri.
Mchezaji mwenyewe alikuwa ni Pascal Wawa. Kwa hiyo alisajiliwa na alicheza Simba miaka minne kwa mafanikio, hivyo naelewa sana umafia wa usajili ulivyo."
WANAKWAMA WAPI?
Nyota huyo wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi anasema kuna tofauti ya usajili wa sasa na zamani, kwani kuna viongozi wa klabu wanajali maslahi binafsi ndio maana wanabeba wachezaji wanaoshangaza uwanjani.
Anasema: "Zamani sisi tulikuwa tunafanikiwa kwa sababu tunakaa jopo. Hawa wachezaji wanaoweka vitu mtandaoni huwa wanachukua yale mazuri tu mara kafunga goli au kapiga pasi na kisigino.
"Kwa hiyo pale kuna vitu huwa tunavitazama kutoka kwa mchezaji ndio maana mbinu yetu ni kwenda kumuangalia uwanjani ili kumjua zaidi.
"Kuna watu wanasajili kwa mapenzi yao na sio kwa manufaa ya timu tofauti na sisi tulikuwa tunafanya kwa moyo mmoja. Ndio maana tulipata watu wa kueleweka sio wa kuchekesha".
HASARA ZA MPIRA KUWA BIASHARA
Kadri muda unavyozidi kwenda soka linazidi kuwa biashara na kazi ambayo vijana wengi wanaitazama ili kuwanufaisha zaidi tofauti na zamani.
Winga huyo wa zamani anasema kuwa mpira ni biashara na una faida na hasara zake ukiwasaidia vijana wengi kupata mafanikio mapema kimaisha.
"Sasa hivi ni biashara ndio maana hushangai mchezaji kutoka Yanga kwenda Simba, enzi zetu ilikuwa vita kwa sababu ile sio kazi ni mapenzi ya mtu kuchezea timu fulani," anasema.
"Mchezaji anaweza kupata majeraha kabla hata hajastaafu, kwa hiyo kama hakuwa na akili, basi kazi imeishia hapo lazima atapata wakati mgumu maishani. Vijana waache starehe watumie fursa hii ya mpira kuwa biashara vizuri."
MRITHI WAKE SIMBA
Wapo wachezaji ambao mbinu zao wakiwa uwanjani zinaweza kufanana na baadhi ya mastaa wa zamani, na hapa winga huyo wa zamani anazungumzia kuhusu staa aliyerithi mikoba yake Msimbazi.
"Kufananisha anatakiwa aseme mtu mwingine sio mimi kwa sababu kuna utofauti wa enzi zetu na zamani tulicheza kwa mapenzi tu sasa ni biashara," anasema mchezaji huyo.
"Ilikuwa ngumu kutoka kwenda timu nyingine au mkataba wake umeisha, hivyo ni ngumu kumpata mrithi wa moja kwa moja.
"Wakati nacheza nilikuwa mtu wa kujituma sana mpaka wenzangu walikuwa wakisikia nimeumia wanaona mchezo haunogi. Ila kwa Simba na muona Kibu Denis au Elie Mpanzu ndio kidogo naona wamechukua viatu vyangu."

AKATAA UKOCHA
Dua anasema akilini hajawahi kuwaza wala kutamani kufanya kazi ya ukocha kwani haoni kama atatimiza malengo akiwa huko.
"Wengi wanapenda kusomea ukocha hata mimi pia nilifanya hivyo. Lakini, sitaki kutumia elimu hiyo kwa sababu sio kazi ya kudumu," anasema Dua.
"Hizi timu kila siku zinafukuza makocha, hivyo huwezi kuweka malengo. Mpira sio kazi ya muda mfupi kama wengi wanavyosema kwani unaweza kutoka kucheza na ukafanya mengine ya ndani ya soka.
"Mimi sikutaka kuendelea kudumu ndani ya soka tena, labda niwe mdau tu ambao nitahusika katika mambo nitakayohitajika kama hivi kuwapa hadithi za zamani."
SIMBA YAMOTO
Kikosi cha Simba msimu huu kimeanza na moto katika mashindano ya ndani na kimataifa ambapo Dua anasema moja kati ya vitu vikubwa vilivyokijenga ni falsafa ya kocha Fadlu Davids ambaye amekuwa Msimbazi tangu mwanzo wa msimu.
"Simba sasa imejipata idara zote. Kocha ameongeza kutoa nafasi kwa mastaa ambao walikuwa hawachezi na sasa wanacheza.
"Mtu kama Edwin Balua alikuwa hachezi sana, lakini kuna kipindi anakuwa anacheza hivyo kocha yeyote anakuja na misimamo yake," anasema mkongwe huyo na kuongeza:
"Ndio maana timu yoyote inayoshiriki michuano mikubwa kama kocha akiondolewa katikati, basi ujue kuna anguko litatokea, mfano mzuri Yanga imemuondoa mwalimu sasa haijakaa sawa."
SIMBA NA MASTAA WA ZAMANI
Akizungumzia wachezaji wa zamani, winga huyo wa mkongwe pale Simba anasema wapo wengi, lakini hawapo karibu na timu labda kwa kuwa soka limekua kulinganisha na wakati wao.
Anasema: "Kipindi hiki wapo wanaoshirikiana na klabu na sisi wengine tupo kama mashabiki tu - hatuwezi kusema tumetolewa moja kwa moja. Mtu kama Matola (Selemani) yupo na Simba na wengine wengi, lakini hata mimi niliwahi kupita katika kamati ya usajili kuanzia 2014-2019 kabla ya Mohammed Dewji hajawa bosi."
WACHEZAJI WANAFELI HAPA
Mkongwe huyo pia anangumzia suala linalozungumzwa sana juu ya mastaa kuuza mechi na hapa anasema kilichowabeba wakati wao ni mapenzi na timu sio pesa.
"Kuna baadhi yao (wachezaji) wanaipenda Simba na wengine wapo kibiashara zaidi, mchezaji anaona amesaini zake miaka miwili kuitumikia timu, acheze akimaliza aende zake.
"Wapo wanaopenda timu na unawaona kabisa wanajituma na kuumia kama watapoteza na wapo wachache kama Kapombe, Tshabalala na wengine (wanaumia sana wakipoteza)."
ALIWAPOTEZEA YANGA
Ni kawaida kwa mchezaji kuchezea Simba na Yanga, lakini zamani ilikuwa ngumu kutokea hilo japokuwa viongozi waliwafuata kama wanaamini mtu anafanya vizuri.
Dua anasema: "Wakati niko Small Simba ya Zanzibar nilitafutwa na Yanga wakitaka kunisajili, basi nilikuwa na mechi timu ya Taifa nikawaomba nimalize halafu tutaongea.
"Basi walipokuja wakaniambia mbona tunasikia una ofa Uarabuni nikawaambia waniache kama wana wasiwasi. Baadaye waliporudi kuhitaji mazungumzo nilikataa, ndipo dili likaishia hapo."
ALIVYOTUA SIMBA
Dua ambaye alijitengenezea jina zaidi akiwa Simba anasema, "kuna kocha wa Small Simba aliniagiza kwa mdhamini Azim Dewji pesa nikamchukulie kama laki tano. Nilivyofika tu bosi akaniambia alikuwa ananitafuta na anataka nijiunge na timu kubwa, nikamwambia kule nilikokuwa kuna fomu za usajili zinakuja sasa itakuwa ngumu," anasema.
"(Dewji) akasema hakuna shida ataongea na kocha. Kipindi hicho siko kipesa wala sina wazo la kucheza huku. Kwa hiyo makubaliano yakaisha siku hiyohiyo.
"Wakati huo Edibily Lunyamila anatakiwa Simba kwa hiyo Azim akawapiga wachezaji baadhi kuwauliza kati yetu amchukue nani, basi nikapitishwa na kupewa milioni moja na laki tano kama pesa ya usajili... nikaanza kazi na hiyo hela nikaitumia kuoa kwanza."
BAADA YA SOKA
Kuhusu maisha yake ya sasa, mchezaji huyo wa zamani anasema anajihusisha na kilimo pamoja na ujasiriamali kama sehemu ya shughuli za kujiingizia kipato.
"Mimi ni mkulima na pia ni mjasiriamali wa biashara ndogondogo ambazo zinayafanya maisha yasonge. Ila napenda ufugaji kwa hiyo nina mifugo kidogo," anasema.
"Mfumo wa maisha ya kutokumtegemea mtu umenifanya niingie kwenye ujasiriamali. Maisha ni mazuri baada ya mpira, naongea na ndugu na jamaa kwani wapo ambao hawapati nafasi hii na walivuma wakati huo."

TANO BORA SIMBA
Mchezaji huyo wa enzi hizo anawataja baadhi ya nyota wanaomkosha Msimbazi akisema kama angekuwa kocha basi hawa wasingekosekana kikosini:
"Kwanza nitaanza na kipa Camara (Moussa), beki Shomari Kapombe, Mohammed Hussein 'TShabalala' bila kumsahau Kagoma (Yusuf) na Elie Mpanzu hao ndio mastaa wanaonivutia sana.
"Mpanzu namuona kuwa bora kutokana na aina yake ya uchezaji na alichokionyesha, itoshe kusema namuona mbali katika michezo ijayo. Ana pasi zenye matokeo ambazo ni ngumu kufanya hivyo bila ujuzi."