DAKIKA ZA JIOOONI: Azam inavyotoka kwenye ramani

Muktasari:
- Kwa hesabu hizo unaona ugumu uliopo kwa Azam kushinda vita ya kumaliza katika nafasi ya pili kama msimu uliopita ambao iliibwaga Simba na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikotolewa katika hatua ya awali.
AZAM FC inaendelea kupigania heshima yake, ambapo tumaini kubwa lililobaki sasa ni kumaliza katika nafasi ya tatu, ingawa kimahesabu bado inaweza kumaliza ya pili baada ya kuukosa rasmi ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Azam ilienguliwa rasmi katika mbio za ubingwa juzi baada ya kipigo cha 2-1 kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Yanga, ambayo imejiimarisha kileleni ikiwa na pointi 67 baada ya mechi 25. Azam imecheza mechi 26 na ina pointi 51, ikishinda zote nne zilizobaki itafikisha pointi 63.
Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa imecheza mechi 22, ina pointi 57 hivyo ikishinda mechi mbili tu kati ya nane ilizobaki nazo itakuwa imeshaifikia Azam.
Kwa hesabu hizo unaona ugumu uliopo kwa Azam kushinda vita ya kumaliza katika nafasi ya pili kama msimu uliopita ambao iliibwaga Simba na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikotolewa katika hatua ya awali.

MSIMU ULIOPITA
Msimu uliopita Azam, ambayo historia inatukumbusha imewahi kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja msimu wa 2013-14, ilimaliza nafasi ya pili ikilingana pointi na Simba zote zikiwa na pointi 69, huku juu yao walikuwapo mabingwa mara tatu mfululizo, Yanga, waliomaliza na pointi 80.
Azam kumaliza ya pili 2023-24 ilitokana na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ambapo ilikuwa na mabao 63 ya kufunga dhidi ya ya 21 ya kufungwa na kuwafanya kukaa juu ya Simba kwa tofauti ya mabao +42.
Simba ilimaliza na mabao ya kufunga 59 dhidi ya 25 ya kufungwa na kuwafanya wekundu hao kumaliza na tofauti ya mabao +34, jambo lililoifanya timu hiyo kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika ambako imetinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia yake na itacheza na Stellenbosch ya Afrika Kusini Aprili 20 Kwa Mkapa Dar es Salaam na kurudiana Aprili 27 kule Cape Town.

MSIMU HUU
Kiujumla, Azam ilikuwa na msimu mzuri uliopita hasa kwa kushinda vita ya kufuzu Ligi ya Mabingwa ambayo ilikuwa haijashiriki kwa miaka 10, huku pia staa wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akichuana katika vita binafsi ya hadi mwisho wa msimu ya kuwania Kiatu cha Dhahabu cha ufungaji bora wa ligi, ambacho kilienda Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyefunga mabao 21 huku staa huyo wa Azam akimaliza na mabao 19.
Msimu huu kibao kimegeuka. Azam baada ya kutolewa mapema katika Ligi ya Mabingwa kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1 na APR ya Rwanda, na kuchakazwa na Yanga kwa kipigo cha mabao 4-1 katika fainali ya Ngao ya Jamii, ikaanza ligi kwa matokeo yasiyoridhisha ikitoka suluhu mbili mfululizo dhidi ya JKT Tanzania (0-0) na Pamba Jiji (0-0).
Ikazinduka kwa kuipa kipigo kizito KMC cha mabao 4-0 na kisha kuilaza Coastal Union 1-0 kabla ya kurudi katika matokeo mabovu ilipolala 2-0 dhidi ya Simba na kiisha kutoka suluhu nyingine na Mashujaa (0-0).
Huu haukuwa mwanzo mzuri kwa timu ambayo imetoka kuiwakilisha nchi na inayojaribu kushinda ubingwa wa ligi kwa mara ya pili katika historia yake.
Mwendo mzuri uliofuata wa kushinda mechi saba mfululizo ikiwamo kuwalaza mapema mabingwa Yanga kwa bao 1-0 la Djibril Sillah Novemba 2, 2024 uliamsha matumaini, lakini mfululizo huo wa ushindi ulizimwa na Tabora United kwa kipigo cha 2-1 ugenini.
Kufikia sasa, baada ya vipigo vitano na sare sita katika mechi 26, Azam imeondolewa katika mbio za ubingwa na ina matumaini finyu ya kumaliza katika nafasi ya pili.
Na hata nafasi ya tatu italazimika kuipigania kwa jasho kwa sababu imetofautiana kwa pointi moja tu na Singida Black Stars iliyo katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 50. Azam ina pointi 51.

MECHI ZIJAZO ZITAAMUA
Azam imeshapotea katika ramani ya ubingwa na bila ya shaka ramani ya kufuzu Ligi ya Mabingwa na sasa inapaswa kujishikilia isipoteze japo fursa ya kumaliza katika nafasi ya tatu.
Imebakiza mechi nne, moja ni dhidi ya Kagera Sugar ambayo raundi ya awali iliifunga kwa taabu bao 1-0 nyumbani Azam Complex na sasa itaenda ugenini Kaitaba, kisha itaivaa Dodoma Jiji (Azam Complex), halafu ina mtihani wa nyumbani dhidi ya nyuki wa Tabora United ambao waliilaza Azam 2-1 kule Tabora na itamalizia ugenini dhidi ya Fountain Gate.
Wapinzani wao katika kuwania kumaliza nafasi ya tatu, Singida Black Stars wana mechi nne pia za kumalizia msimu dhidi ya Tabora United (nyumbani), Simba (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani) na Tanzania Prisons (nyumbani).

AZAM BINGWA 2013/14
Azam ile ya kibabe iliyotwaa ubingwa wao wa pekee wa Ligi Kuu katika historia yao msimu wa 2013/14, ilimaliza ligi bila ya kupoteza (26PL, 18W, 8D, 0L) na kuwa moja ya timu tatu tu zilizowahi kufanya hivyo katika historia ya ligi hiyo pamoja na Yanga msimu wa 2021-22 (30PL, 22 Wins, 8D 0L) na Simba 2009-10 (22PL, 20W, 2D, 0L).
Azam ilipotwaa ubingwa nafasi ya pili walikuwa Yanga na pointi 56.

MSIKIE POPAT
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, anakiri timu yao kuyumba msimu huu, akisema wako kwenye eneo la kufanya tathimini ya kina kujua mambo yaliyowaangusha.
Popat anasema Azam, haistahili kuwa kwenye kiwango ambacho walikionyesha msimu huu na kwamba lazima kutakuwa na sababu za msingi zilizowafikisha hatua hii ingawa wataendelea kutafuta matokeo mazuri kwenye mechi zilizosalia.
“Kiwango cha timu yetu ni kweli kuna maeneo tunaonyesha tumeshuka. Msimu uliopita tulimaliza nafasi ya pili, msimu huu tulipaswa kwenda juu zaidi au kubaki palepale,” anasema Popat.
“Kitu kinachotuumiza huu ndio msimu ambao tuliwapoteza wachezaji wawili pekee Kipre Junior tuliyemuuza Algeria ambaye ndio unaweza kusema lilikuwa jambo zito lakini pia Dube (Prince) ambaye naye aliondoka hapa kwetu muda mrefu kabla hata msimu kumalizika.
“Tunahitaji kufanya tathimini kubwa ya ndani na tupo kwenye mchakato huo tukimaliza tutajua mambo yote yaliyotukwamisha mpaka kufikia hapa.”
MSIKIE KOCHA
Kocha Rachid Taoussi amekiri kwamba timu iko katika nafasi ambayo ipo nje ya malengo akisisitiza kikosi hicho kilipaswa kuwa kwenye kuwania ubingwa.
“Siwezi kusema nina furaha na eneo ambalo tupo kwenye ligi, mimi ni kocha ninayetaka kuona sehemu ninayofanya kazi tunaishi kwa malengo makubwa bahati mbaya kidogo kuna maeneo hatujafanya vizuri,” anasema.
“Kama unataka kushndana na timu kongwe kama Yanga na Simba basi unatakiwa katika ubora wa juu wakati wote.
“Bahati mbaya Nilikuta timu imeshatolewa kwenye mashindano ya Afrika lakini hivi karibuni tena tukapata mshtuko wa kupoteza nafasi ya kuchukua ubingwa wa Kombe la FA hii haikuwa nzuri kwetu.
“Changamoto kubwa nyingine tumekuwa tukikumbana na hali ya kupata majeruhi wa mara kwa mara tena kati ya wale ambao ni wachezaji wetu bora, hili lilikuwa linatuweka kwenye wakati mgumu kujua namna ya kujipanga.”
“Kama mnavyoona ligi ya hapa Tanzania ni ligi ngumu sana sio rahisi kuona timu inashinda.
“Nataka kwanza tumalize salama msimu huu lakini kuna mambo mengi tunatakiwa kuyafanyia kazi ili kuhakikisha makossa ambayo tumeyafanya au yametutokea msimu huu hayajirudii huko mbele, narudia Azam ni timu kubwa tena inawezekana kubwa zaidi ya klabu zote za hapa, lakini ni lazima tuishi kwa akili kubwa ya kupigania hadhi ya klabu hii.”