Dah! African Sports ‘Wana Kimanumanu’

Muktasari:
- Mechi hiyo si tu pambano la pointi kwenye msimamo wa ligi, bali ni suala la fahari ya jiji, historia na utambulisho wa wapenda soka Tanga.
DABI ya Tanga ni miongoni mwa mechi za kusisimua zaidi katika soka la Tanzania ikiakisi ushindani wa jadi kati ya klabu mbili kongwe za mkoa huo, Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ na African Sports ‘Wana Kimanumanu’.
Mechi hiyo si tu pambano la pointi kwenye msimamo wa ligi, bali ni suala la fahari ya jiji, historia na utambulisho wa wapenda soka Tanga.
Kila timu huingia uwanjani ikiwa na ari ya kipekee ikiwakilisha sio tu mashabiki wake, bali mitaa, familia na kumbukumbu za enzi za soka la jadi. Uwanja wa Mkwakwani husheheni mashabiki waliovaa rangi za klabu hizo yaani nyekundu na nyeupe kwa Wagosi na bluu na nyeupe kwa Wanakimanumanu wakiwa na matarajio ya ushindi na huwa ni sehemu ya historia yao.
Dabi hiyo imejikita katika historia ndefu ya ushindani, vipaji vya nyumbani na hamasa ya mashabiki na kila mara inapochezwa Tanga husimama kushuhudia nani ataibuka kidedea kati ya Coastal na Sports.
Mwanaspoti lilifunga safari hadi Tanga ilipokuwa African Sports na kuzungumza na katibu wa timu hiyo, Seleman Ramadhan ‘Magesi’ aliyesimulia sababu zilizoiangusha klabu hiyo iliyoanzishwa Novemba 18, 1936. Twende pamoja.

MAANA YA ALAMA
Kumekuwapo na mazoea kuwa kila timu inakuwa na maana yake, hapa katibu wa African Sports, Magesi anaeleza upande wa timu hiyo inamaanisha nini.
“Hii ni ishara ya nanga, meli ikifika mwisho wa safari huwa kuna kitu kama chuma kinashushwa chini ya bahari ili kuzuia isiendelee kutembea majini.
“Kwa hiyo sisi tunajiita aabaharia kwa maana kwamba hakuna zaidi yetu, ndio sababu hakuna timu nyingine ambayo ina alama kama hii,” anasema.
KILICHOIANGUSHA
Magesi anasema timu hiyo ilipandishwa na watu na haohao ndio walioishusha na kwamba mpaka leo bado inaendelea kujitafuta bila mafanikio.
“Timu yetu ilikuwa na watu wengi wenye pesa zao. Zilikuwa zikija Simba, Yanga wakati huo zinafungwa tu hata kama kulikuwa kuna mambo yanahitajika ilikuwa rahisi kufanyika.
“African Sports imekosa wadhamini ambao wangeisaidia kufika mbali kwa sababu zamani (timu) zilikuwa zinaendeshwa kiujamaa ukilinganisha na sasa.
“Hata wachezaji tulionao hatuwalipi chochote, tulitafuta vipaji kutoka maeneo ya karibu na tukawaambia kuwa kwa sasa bado mambo hayajakaa sawa hivyo hatuwezi kuwaahidi mshahara,” anasema.
“Kusafiri tu mpaka tuombe mchango, muda mwingine wachezaji wanatangulia halafu hela ya kula na usafiri wa kurudi tunaitafuta huku mtaani.”

UONGOZI TATIZO
Kuhusu uongozi anasema kuna ishu muhimu.
“Kingine kilichotukwamisha ni kutokuwa na viongozi ndani ya miaka 10. Tuliopo sio wa kuchaguliwa ila ni ile unaambiwa kaimu nafasi ya katibu au mwenyekiti.
“Linapokuja suala la kutafuta wadhamini tunakwama kwa sababu sisi sio viongozi wa kuchaguliwa kabisa. Kwa hiyo mtu anaogopa kuweka pesa yake, kwani anaamini kesho anaweza kupata shida na asiwepo wa kumsaidia.”
ISHU YA UKARIBU
Kama ilivyo kwa watani wengine kuwa haiwezekani mashabiki wa timu moja kukaa upande wa mwingine au viongozi wake kutembeleana, lakini upande wao ni tofauti sababu za mfumo huo wa maisha ni nini?
“Sisi na Coastal Union uhasama wetu upo ndani ya uwanja tu na sio kwenye maisha ya kawaida. Tunafuatana na kusaidiana kama kuna shida upande wa wapinzani tunashirikiana nao.
“Hatuna utaratibu kama timu zingine kwamba mkiwa wapinzani basi nyie ni maadui wakubwa yaani mtu akivaa jezi upande fulani inachomwa moto.
“Uhasama upo ndani ya mechi baada ya hapo tunaendelea na udugu wetu, lakini sasa hivi kuna mikoa mingine hakuna jambo hilo jezi ya mpinzani kuuzwa dukani kwako na wakati ile ni biashara.
“Unaweza ukamkuta mtu wa Coastal Union yuko pamoja na wa African Sports tunakunywa kahawa vizuri tu na kubadilishana mawazo hata kwenye ofisi ya timu mojawapo.”

DABI ILIVYO
Dabi ni mchezo flani unaokuwa na mambo yake na hapa Magesi anaeleza aliyonayo: “Sasa kuna watu hawajawahi kuona hizi timu zikicheza, zamani ilikuwa kama sikukuu siku ya dabi yenyewe. Nakumbuka mimi nilikuwa mtoto kipindi hicho, uwanja ulijaa mpaka tukafunguliwa tukae pembezoni mwa uwanja. Kwa hiyo wachezaji unawaona kwa ukaribu, kutokana na wingi wa watu.
“Hizi barabara utaziona zimejaa watu kuanzia saa 4 asubuhi wakienda uwanja. Kwa hiyo ukichelewa imekula kwako huingii unazuiwa kabisa maana ndani kumejaa.
“Hii dabi ilikuwa kubwa kwelikweli watu walikuwa wanakuja kutoka maeneo ya mbali mpaka nje kipindi hicho... watu wako radhi kutoka Zambia kuja Tanga.”
DABI NJE NDANI
Unaambiwa kulikuwa na dabi ya nje ya uwanja na ndani pia ambapo mashabiki wa timu walikuwa wakifanya mambo kabla ya mchezo.
“Mambo hayo yalikuwa ya zamani. Wazee walikuwa wakiamini sana mambo ya ushirikina kwa hiyo walikuwa wakitambiana kabla ya mechi kuhusu mabao watakayofungana.”

UKARIBU NA YANGA
Dabi ya sasa inashikiliwa na Simba Yanga. Kwa hiyo, Coastal Union kwa sababu walivaa nyekundu na African Sports njano basi wakagawana udugu.
“Sababu iliyotukutanisha ilikuwa rangi yaani ilikuwa ukishabikia African Sports basi upo Yanga, ukiwa mpenzi wa Simba basi utakuwa Coastal.
“Wakati huo tulikuwa tukifika mjini, basi Yanga walikuwa kama wenyeji wetu wanaotupokea.Kwa hiyo tulikuwa ndugu hasa, japo ndani ya uwanja hatukuwa tunalegeza kamba.
“Kwa sasa ukaribu upo kidogo mfano tulivyokuwa tukienda Songea na Mbeya kuna kiongozi wa Yanga tulimpigia tulivyokwama akatusaidia 17 milioni tukakamilisha safari yetu.”
COASTAL IMEFANIKIWA
Akiwazungumzia wapinzani wao, Coastal anasema: “Wenzetu walifanikiwa kubaki Ligi Kuu japokuwa waliwahi kuanguka pia ila wakainuka tena. Kuna kipindi tulianguka miaka 22 bila kuinuka halafu 2015 tukapanda na tukashuka wote pamoja. Ikashuka Mgambo, African Sports na Coastal Union, lakini wakaja vizuri na wakarudi sisi tunasuasua ila mpira wa kuombaomba sio mzuri sababu hauna faida.”

KARIA, MNGUTO
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto na Rais wa TFF, Wallace Karia wote ni wanachama wa Coastal Union, lakini katibu huyo anasema wamekuwa msaada hata kwa African Sports.
“Karia ni shabiki wa Coastal, lakini katusaidia sana tunaweza kumpigia simu tuna shida na pesa na akatusaidia au akatupa mtu wa kutushika mkono.
“Ila kweli kabisa hajawahi kuipendelea Coastal Union mpaka tukahisi kuonewa, ila amekuwa kiongozi mwema kwa wote ambaye anatusaidia sana.”
MASHABIKI WATIMKA
Magesi anasema kushuka kwa timu hiyo kumepunguza mashabiki ambao walikuwa wakipenda sana soka, lakini hawakuwa wanapata wanachotaka.
“Unajua mpira ni burudani. Kwa hiyo anguko letu limetufanya tupoteze mashabiki wengi ambao sasa wanashabikia timu zingine ambazo zinawapa burudani.
“Timu ili iwe na mashabiki inatakiwa ifanye vizuri mfululizo hata vizazi vijavyo vinavutiwa na timu husika, wanachama wengi lakini huwezi kusema unawapata kila siku.”
SIMBA NA YANGA
Kiongozi huyo anasema mpaka sasa kuna utamaduni haujafutika pindi zinapochezwa Simba na Yanga, kwani mashabiki wa Tanga hujigawa. “Mpaka sasa mashabiki wa African Sports wanashabikia Yanga. Kwa hiyo ikifika muda wa mechi hizo kuchezwa hali huwa inabadilika kabisa.
“Bado sisi ni wapinzani hadi kwenye Dabi ya Kariakoo ni ngumu kwa mshabiki kindakindaki wa African Sports kuishabikia Simba, labda hawa watoto wa miaka ya 2000,” anasema.

UBINGWA ENZI ZILE
Akizungumzia utamu wa soka la miaka ile, anasema: “Wakati tunabeba ubingwa wazee walikuwa wakibeba kombe, walikuwa na ushirikiano ambao uliwawezesha kuchanga pesa kwa umoja.
“Tofauti na sasa kupata pesa za kuendesha timu ni mpaka tuchange huku na kule ndio maana tumepotea kwenye ramani. Lakini malengo yetu ni makubwa huenda tukarudisha ushindani wetu.”
COASTAL INAWAOGOPA
Ushindani wa timu hizo mbili umekuwa na ukali ambao unakumbukwa na wengi, na katibu huyo anasema mpaka sasa Coastal Union bado inawaogopa.
“Coastal Union mpaka sasa hivi inatuogopa, haitaki hata kusikia inapokuja habari ya kucheza na sisi hata mechi za kirafiki, wana sababu zao wenyewe.
“Sisi tunatakaga kucheza nao ila wao hawataki... naamini bado tuna ukali kuwazidi ndio maana wanatuombea tusipande kwa sababu tulipocheza nao tuliwashusha.”
ILIKOTOKEA
African Sports ilianzishwa 1936 na maskani yake ikiwa ni Barabara ya 12, Tanga, waasisi wake wakiwa hayati Mohammed Msuo, Mwajitu na Athumani Makalo. Pia kuna baadhi ya wachezaji walioipa jina Sports mwanzoni ni kama makipa Mohammed Yahya, Omar Mahadhi, mabeki Mweri Simba, Omar Zimbwe, Salim Kajembe, Muhaji Mwabuda na kiungo Amran Shiba. Mabingwa wa Muungano 1988, mwaka ambao Costasl ilibeba taji la Ligi Kuu Bara na Wanakimanumanu walitwaa taji hilo wakiwa chini ya kocha Syllersaid Mziray ‘Super Coach’ (sasa marehemu), aliyekuwa akisaidiwa na Muhaji Mwabuda.
Kikosi cha ubingwa kilikuwa kinaundwa na Salim Waziri, Bakari Tutu, Francis Mandoza, Hassan Banda, Mhando Mdevi, Raphael John, Abbas Mchemba, Twaha Omar, Victor Mkanwa, Mchunga Bakari na Juma Burhan.
Wachezaji wa akiba walikuwa Duncan Mwamba, Martin Mahimbo ‘Water Green’, Abdul Ahmed ‘Bosnia’, Hamza Maneno, Dadi Fares na wengineo.
Hata hivyo Sports ilishuka daraja 1991 na tangu hapo ilikuwa ikisota kurejea Ligi Kuu bila mafanikio hadi 2015-2016 iliporejea na kushuka msimu huohuo sambamba na Coastal Union na Mgambo JKT ikiwa ni rekodi ya Ligi Kuu kwa timu za mkoa mmoja kushuka kwa mpigo.
Baadhi ya makocha waliowahi kuinoa timu hiyo ni Charles Boniface Mkwasa, Freddy Felix ‘Minziro’ na Joseph Lazaro aliyewika Coastal Union na Yanga miaka ya 1990 na Kassim Mwabuda aliyechezea Mtibwa Sugar enzi zake.
Kikosi kilichoirejesha Sports Ligi Kuu 2015 kiliundwa na Yussuf Abdul, Halfan Twenye, Mussa Ajiran, Juma Shemvuni, Mwaita Ngereza, Sultan Juma, Ramadhani Hamidu, Ally Ramadhani na Ally Shiboli.Wengine ni James Mendi, Nyanda Kaziyoba, Tokala Nzau, Ayub Masoud, Ally Issa, Mussa Chambe, Ally Ahmed, Fadhili Kizenga, Evarstus Munjwahuki, Maulid Abbas, Nzara Ndaro, Rashid Ally, Hussein Issa, Zakaria Majaliwa, Issa Yassin, Paul Muna, Mohamed Rashid na Kassim Juma chini ya majkocha Joseph Lazaro na Mohammed Kampira.
MALENGO
Kuhusu malengo, kiongozi huyo anasema: “Kwa sasa tumeanza na uongozi kwanza kuhakikisha tunachagua na sio kuwateua kama ilivyokuwa awali. Hii itasaidia wadhamini kutuamini tena. Tukipata wadhamini tutarejea katika ligi kwa haraka, lakini wadau wa soka wasitusahau kwani bado tunahitaji uwepo wao na mchango ili kunogesha mashindano kama zamani.”