Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dabi ya makipa

LEO Jumapili, Watani wa Jadi, Simba na Yanga watashuka Benjamin Mkapa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na Wekundu wa Msimbazi watakuwa wenyeji wa mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka.

Ni mchezo ambao unatawaliwa na tambo kutoka pande zote mbili japokuwa hautabiriki, dakika 90 ndio huamua matokeo.

Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 18 sawa na Yanga, lakini ikiwa kileleni kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa.

Mastaa wengi wamepita kwenye dabi hii ambayo ni kubwa Afrika na baadhi yao wamefunguka kuhusu mchezo huo wa 111. Wanasema mchezo huo hautabiriki  na hata upande mmoja ukiwa dhjaifu si wa kuubeza kwani lolote linaweza kutokea na tayari huko nyuma mambo hayo yalishatokea.


WASIKIE WENYEWE

Ngoma ngumu...

Kipa wa Namungo, Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyewahi kuzichezea Simba na Yanga, anasema: “Mechi za dabi hazizoeleki ndiyo maana zina maumivu makali kwa timu inayopoteza, natarajia mchezo wa leo utakuwa mgumu.”


Ubora hautabiri Dabi...

Wakati akisema hivyo, staa wa zamani wa Simba na Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amesema haichukulii poa mechi hiyo, kulingana na timu hizo kutotegemea ubora wa vikosi vyao. Anasema kwa uzoefu alionao, hajawahi kuona dabi nyepesi na inayoweza kutabirika zaidi ya kusubiri dakika 90 za nani anaondoka kifua mbele.

“Yanga inafanya vizuri kwenye ligi na Simba inafanya vizuri, pamoja na hayo huwezi kutabiri dabi itakuaje, timu itakayokuwa na hamasa nzuri ndiyo itakayowafurahisha mashabiki wake.

 “Sikumbuki msimu gani, ila Simba haikuwa na kiwango kizuri, kipindi hicho ilimrejesha Madaraka Selemani aliyekuwa amestaafu, sasa hiyo ikawa inatupa jeuri Yanga, ajabu Selemani ndiye aliyetufunga.”


Siyo dabi ya kuvunja rekodi...

Abdallah Kibadeni aliyeitumikia Simba kama mchezaji na kocha, anasema anatarajia kuona burudani na mchezo mgumu utakaokuwa na mabao machache. “Sioni kama ni dabi itakayozalisha hat-trick ya kuvunja rekodi yangu ya mwaka 1977, kiufundi itakuwa mechi ya kushangaza na mpira utapigwa mwingi,” anasema.


Dabi ni ngumu

Kwa upande wa winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe anasema dabi ina machungu na furaha baada ya dakika 90.

“Mechi ya mzunguko wa kwanza ina uchungu mwingi, timu inayofungwa italazimika kusubiri mzunguko wa pili kulipa kisasi, ikiacha mashabiki wakae kinyonge mtaani, dabi hii ni ngumu hakuna timu inayoweza kutembea kifua mbele kushinda kirahisi,”anasema.


Makipa wamebeba dabi

Kocha wa makipa wa zamani wa Simba, Idd Pazi anasema ubora wa makipa wa klabu hizo, Djigui Diarra na Ally Salim ambaye ameibeba Simba kwenye mechi mbili za hivi karibuni utawapa wakati mgumu washambuliaji kucheka na nyavu.

“Salim na Diarra waitazame mechi hiyo kwa jicho la tatu, atakayeruhusu nyavu zake kutikishwa atajitia doa mbele ya mashabiki wake, pamoja na hayo yote natarajia itakuwa mechi ngumu yenye kutoa burudani nzuri,” anasema.


Atakayeamka vizuri...

Aliyekuwa beki wa kati wa Yanga, William Mtendawema anasema ni mechi ya kukamiana, kila timu itapambania furaha ya mashabiki wake. “Siyo mechi ya kutabiri hata kidogo, atakayeamka vizuri ndiye atakayecheka, mechi nyingi zilizopita wachezaji wanakamiana, hiyo inatokana na presha ya mashabiki, ukizungumzia ufundi timu zote zipo vizuri,” anasema.


Kuna watu watashangazwaa

Aliyekuwa beki wa kushoto wa Simba, Kasongo Athumani Mgaya anasema namna inavyochukuliwa timu hiyo na mashabiki wa Yanga, anawapa tahadhari ya kutotembea na matokeo. “Simba siyo mbaya, ila upepo kwa wafungaji ndiyo changamoto, ninachokiona kwenye dabi, mashabiki wa Yanga watashangazwa kuona pasi za maana, ila kuhusu matokeo dakika 90 zitaamua nani zaidi.”


Hawa wana nafasi

Beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua anaipa nafasi timu hiyo kuondoka na pointi tatu, akitaja sababu ni aina ya kikosi bora ilichonacho. “Yanga ipo imara kila sehemu, nimeangalia aina ya mabao wanayofunga wachezaji siyo ya kubahatisha ndiyo maana nasema ina nafasi ya kushinda, ingawa dabi haitabiriki.”


Kutakuwa na bato

Nyota wa zamani wa Simba, Yusuph Mgwao anasema dabi inaweza kukupa umaarufu au kukupoteza.Anasema wachezaji wengi walitamani zaidi kukaa benchi kuhofia kutofanya vizuri.

“Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Simba, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ anasema itakuwa mechi nzuri yenye ushindani lakini ametoa angalizo kwa waamuzi kutoiharibu.”

Kama waamuzi wakichezesha vizuri kwa haki basi hata wachezaji wataonyesha ubora wao na watu wanaona burudani nzuri.

“Burudani katika mchezo huo italetwa na viungo na washambuliaji wa timu zote mbili  na ndio itakuwa kupimo cha kuangalia umri wa mabeki.

“Itakuwa vita ya mabeki dhidi ya mastraika.”