Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Club Africain walivyoifundisha Yanga kucheza ugenini

Club Africain walivyoifundisha Yanga kucheza ugenini

PENGINE mwamuzi alikuwa na huruma sana kwa wachezaji na benchi zima la ufundi la Club Africain wakati ikicheza mechi ya kwanza ya raundi ya mtoano ya Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi Jumatano.

Kama ni huruma, basi tabia hiyo inaweza kumchafulia rekodi yake ya uamuzi kwa kushindwa kuvichukulia hatua vitendo vya ajabu kutoka kwa wachezaji na benchi zima la ufundi.

Lakini si rahisi kwa huruma yake kupita kiasi na kumtibulia rekodi yake ya ubora katika uamuzi. Kwa hiyo ni dhahiri kila alichofanya kilikuwa ndani ya sheria na kanuni zinavyotaka.

Na kama ni hivyo, wachezaji na benchi zima la ufundi la Club Africain hawakufanya makosa makubwa yaliyostahili adhabu kubwa, zaidi ya zile kadi mbili za njano kwa mchezaji mmoja na mtu mmoja kutoka benchi la ufundi.

Na kama ni hivyo, basi Yanga na Watanzania kwa ujumla wamepata somo la kucheza ugenini dhidi ya timu ambayo unajua inaweza kupata matokeo mazuri nyumbani.

Wengi tunajua njia pekee ya kupoteza muda ni kuchelewa kurusha mpira, kuchelewa kupiga mpira wa adhabu, kipa kuchelewa kupiga mipira kutoka golini kwake, kipa kuchupa chini baada ya kudaka mpira usio na hatari yoyote au kipa kuchelewa kudaka mpira uliokuja golini kwake ambao hauna hatari.

Wachezaji na benchi zima la ufundi la Club Africain walikwenda mbali zaidi, walifanya vitendo vya kuchelewesha mpira lakini kubwa zaidi kucheza na saikolojia ya mwamuzi kutoka mwanzo wa mchezo hadi mwisho.

Muda wote, benchi la ufundi la Club Africain lilikuwa limesimama likikosoa kila uamuzi na kujaribu kumwelekeza mwamuzi sehemu moja ya uwanja kuashiria kuwa kuna tatizo. Na kwa kutaka kuwafanya watulie, refa alilazimika kwenda kwenye benchi hilo kila mara kujibishana nao au kutaka wasimzonge mwamuzi wa akiba ambaye alilazimika kufanya kazi mithili ya refa msaidizi.

Kila refa alipopuliza filimbi, tayari wachezaji wa Club Africain walimzonga kujaribu kutoa hoja na hivyo kumlazimisha mwamuzi azijibu, kumbe ilikuwa ni janja ya kutaka kumuondoa mchezoni na kupoteza muda.

Zaidi ya kumzonga refa kila mara kwa nia ya kupoteza muda, wachezaji wawili wa Club Africain walidiriki hata kwenda kumpongeza kipa Djigui Diarra kwa kudaka ‘mpira vizuri’. Ilikuwa ni baada ya shambulizi kali lililoishia kwa shuti kali ambalo Diarra alilidaka kirahisi. Wakati Diarra akitaka kuanzisha shambulizi kwa kumrushia mpira mchezaji wake kuanzisha shambulizi la kushtukiza, wachezaji wawili wa Club African wakamfuata haraka kwenda kumshika begani, kama ishara ya kufurahia kazi aliyofanya kuzuia shuti lile.

Hiyo ilikuwa ni mbinu ya kumzuia asianzishe haraka shambulizi la kushtukiza.

Na katika tukio la ajabu kabisa, mtu mmoja kutoka benchi la ufundi la Club Africain aliingia uwanjani wakati mpira ukiwa eneo jingine, akachukua mpira wa akiba uliokuwa karibu yake na kuupiga kuelekea uwanjani. Wengi walidhani mwamuzi angechukua hatua dhidi ya kitendo hicho, lakini akaishia kuzozana na benchi la ufundi, huku muda ukienda.

Kimpira, Club Africain ilitulia nyuma bila kuhangaika sana kwenda mbele. Ilipoteza mipira kirahisi katikati na mara moja wachezaji wote wakaharakisha kurudi nyuma kujipanga kuzuia shambulizi. Ilionekana dhahiri walijua Aziz Ki anafunga kwa mashuti ya mbali na hivyo kila alipojitengenezea nafasi upande wa kushoto, hawakumruhusu apate muda wa kujivuta na kupiga shuti.

Fiston Mayele aliwekwa kwenye ulinzi ambao haukumruhusu ageuke na mpira mara kwa mara na hivyo kuwa ngumu kwake kujaribu mashuti golini. Bernard Morrison na Tuisila Kisinda walizuiwa kukimbia na mpira pembeni kwa ajili ya kutoa krosi na hivyo kulazimika mara kadhaa kujaribu kuingia ndani ambako kulikuwa na msitu wa watu.

Mbele, Club Africain walimbakiza mshambuliaji mmoja, mrefu ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kujifanya ameumia kila mara alipogusana na wachezaji wa Yanga, akisababisha mashabiki kumpigia kelele refa kutaka amuonyeshe kadi ya njano. Mara kadhaa refa alienda kumuangalia na kukumbana na wachezaji na madaktari wa Club Africain ambao kuna nyakati waliingia uwanjani hata bila ya kuitwa na mwamuzi.

“Tulikuwa tunajua kuwa ni timu ambayo ikicheza ugenini inapenda kucheza nyuma sana, kupoteza muda, kukuingia kichwani wakufanye na wewe ukasirike, vitu kama hivyo. Lakini tukabaki kwenye mchezo, tukabaki concentrated na tukafanya kila jitihada,” alisema Kocha Cedric Kaze.

Benchi la ufundi la Yanga pia liligundua tatizo la kujaribu kupitisha mipira katikati baada ya Watunisia kufunga njia zote za pembeni.

“Wakati tunacheza tulitaka sana kupita katikati lakini unakutana na timu ambayo imejaza watu wengi mbele ya defende na mbele ya 18, sanasana hatukucheza sana kwa pembeni. Hiyo ndiyo ingetufanya tuufungue huu mchezo,” alisema Kaze.

Hii ni sare ya pili ya kutofungana ambayo Club African imeipata Tanzania mwaka huu baada ya kulazimisha matokeo hayo dhidi ya Kipanga kwenye Uwanja wa Amaan, lakini wakacharuka kwao na kushinda kwa mabao 7-0.

“Of course kuna vitu vidogovidogo hatukuzingatia, lakini kucheza na timu ambayo ina watu tisa nyuma na mmoja mbele ni vigumu, lakini tunajua kuwa mechi ya marudiano, nao watafunguka,” alisema Kaze.

“Naamini kuwa mchezo bado ni 50/50 na tunaamini kuwa tuna chances za kuqualify. Ni kweli tunaenda kucheza ugenini lakini tunaamini quality tunayo na jinsi tulivyomuona mpinzani kuna kitu cha kufanya kwenye dakika tisini zilizobaki.”

Watakapofunguka, watakuwa wakali zaidi na ni kawaida kwa timu za Kiarabu kushinda kwa mabao mengi nyumbani. Labda njia nzuri zaidi ni kulazimisha matokeo ya suluhu kama Watunisia hao walivyofanya dhidi ya Yanga na Kipanga. Na ili isitumie nguvu nyingi kuzuia, Yanga itahitaji kuwa na ujanja binafsi wa wachezaji kama Watunisia walivyofanya kuupoozesha mchezo na kucheza na akili ya refa wakati wote, huku benchi la ufundi likitumia mbinu za kumvuruga refa na kusaidia kupoteza muda.

Bila ya mbinu hizo za medani, Yanga inahitaji kuwa na kiwango cha juu sana kuweza kufunga mabao ya ugenini ambayo ni muhimu baada ya kutoruhusu bao nyumbani, kitu ambacho ni faida kwa mabingwa hao wa soka Tanzania.

Kaze amesema wamewaona wapinzani wao jinsi wanavyocheza na hivyo watakuwa katika nafasi nzuri ya kupata matokeo yenye faida kwao, lakini kama watakuwa hawajajifunza mbinu hizo binafsi za wachezaji na benchi la ufundi safari bado ni ndefu. Kwa Waarabu kuujua mpira pekee hakutoshi kuipa timu mafanikio, bali mbinu za kuvuruga wapinzani kimchezo na kisaikolojia.