Chan hatua ya makundi soka limepigwa kinoma

Muktasari:
Kwenye michuano hiyo hatua ya makundi yamefungwa jumla ya mabao 46 huku kinara akiwa ni Morocco na Guinea wakifunaga sita kila moja
RASMI nyasi za viwanja vya Ahmadou Ahidjou, Japoma, Reunification na Limbe Omnisports vyote vya Cameroon kuanzia jana vilianza kuwaka moto ambapo michezo ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Chan ilianza kuchezwa.
Timu nane kati ya 16 zilizoshiriki michuano hiyo ndizo zilifuzu hatua hiyo ya robo fainali huku nyingine nane zikiaga mashindano, robo fainali hizo zilianza jana Jumamosi.
Wenyeji Cameroon, DR Congo, Congo, Mali, Rwanda Zambia, Morocco, Morocco na Guinea ndizo zilizofuzu robo fainali huku Tanzania, Zimbabwe, Niger, Libya, Namibia, Burkina Faso na Uganda zikiishia hatua ya makundi na kuaga michuano hiyo.
Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa hatua ya makundi ilivyokuwa kwa kujumuisha matukio na mambo mbalimbali yaliyotokea kwenye hatua hiyo ambayo pia timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ ilishiriki.
MAKUNDI
Katika michuano ya Chan mwaka huu kulikuwa na makundi manne na kila kundi lilikuwa na jumla ya timu nne, kundi A lilikuwa na timu za Cameroon, Zimbabwe, Mali na Burkina Faso, kundi B lilikuwa na timu za Congo, DR Congo, Libya na Niger, kundi C lilikuwa na timu za Morocco, Rwanda, Togo na Uganda, huku kundi D likiwa na timu za Tanzania, Guinea, Zambia na Namibia na kutoka kila kundi zimefuzu timu mbili kwenda robo fainali na mbili zimeaga mashindano.
MECHI
Jumla ya mechi 24 zilipigwa kwenye hatua ya makundi ambapo hatua hiyo mechi 14 pekee ndizo zilimalizika kwa ushindi wakati mechi 10 zikimalizika kwa sare.
Katika hatua hiyo timu za Mali, DR Congo, Morroco, Guinea na Zambia ndizo zilipata ushindi mara mbili pekee huku nyingine zikishinda mara moja, kutoa sare na kupoteza.
Togo, Namibia, Zimbabwe, Niger na Libya ndizo timu zilizotia aibu kwenye michuano hiyo kwa kucheza mechi tatu kwa kila timu pasipo kuambulia ushindi hata mara moja.
Katika hatua hiyo ya makundi matokeo ya 1-0 ndiyo yalitawala kwani jumla ya mechi saba kati ya 24 zilizochezwa zilimalizika kwa ushindi wa bao 1-0.
MABAO
Jumla ya mabao 46 ndiyo yalifungwa kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo ambapo Morocco na Guinea ndizo ziliongoza kwa kufunga mabao mengi zikiwa zimefunga jumla ya bao sita kwa kila timu.
Mchezo kati ya Uganda na Morocco ndio mechi iliyokuwa na mabao mengi zaidi (7) kwenye hatua ya makundi kwani mechi hiyo ilimalizika kwa matokeo ya Uganda 2-5 Morocco.
Namibia imepata rekodi ya aibu ya kutofunga bao hata moja kwenye michuano hiyo hatua ya makundi ikiwa imefungwa mabao manne bila kufunga hata moja.
Uganda nao wameangukia pia kwenye michuano hiyo hususani kwenye hatua ya makundi waliyoishia kwa kuwa timu iliyofungwa mabao mengi ikiwa imeruhusu mabao saba.
Wenyeji Cameroon, Mali na Zambia ngome zao za ulinzi zilionekana kuwa imara zaidi kwani katika hatua hiyo ya makundi ndizo timu zilizoruhusu kufungwa bao chache zaidi ikiwa kila moja imefungwa bao moja pekee.
WAFUNGAJI
Mpaka hatua ya makundi inamalizika, mshambuliji wa Guinea Yakhouba Gnagna Barry ndiye alikuwa kinara wa mabao katika michuano hiyo akiwa na bao tatu. Mshambuliaji huyo pia anaichezea klabu ya Horoya ya Guinea.
Wachezaji Salomon Charles Banga (Cameroon), Masasi Obenza (DR Congo), Victor Kantabadouno (Guinea), Soufiane Rahimi (Morocco), Mossi Issa Moussa (Niger), Richard Nane (Togo) na Saidi Kyeyune (Uganda) ndio walifuata kwa ufungaji kila mmoja akiwa ameweka kambani mabao mawili.
Majina ya Watanzania Farid Mussa, Baraka Majogoro na Edward Charles Manyama nayo yatabaki kwenye vitabu vya wafungaji wa hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mwaka huu kila mmoja akiwa amefunga bao moja huku lile la Majogoro alilofunga dhidi ya Guinea likiingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya bao bora la hatua ya makundi.
Wengine wenye bao moja ni Claver Kiendrébéogo, Issiaka Ouedraogo, Issouf Sosso (Burkina Faso), Mapata Mouandza, Gautrand Ngouonimba (Congo), Kadima Kabangu, Chico Kubanza (DR Congo), Morlaye Sylla (Guinea), Moataz Al-Mehdi (Libya), Siaka Bagayoko, Demba Diallo, Issaka Samaké (Mali), Ayoub El Kaabi, Hamza El Moussaoui, Yahya Jabrane (Morocco), Olivier Niyonzima, Ernest Sugira, Jacques Tuyisenge (Rwanda),Bilali Akoro (Togo), Ibrahim Orit (Uganda), Emmanuel Chabula, Spencer Sautu, Collins Sikombe (Zambia) na Partson Jaure (Zimbabwe).
Wachezaji wawili wa Uganda Charles Lukwago na Paul Mbowa ndio wachezaji pekee waliojifunga bao kwenye michuano hiyo Lukwango alijifunga kwenye mchezo dhidi ya Morocco Mbowa akijifunga mechi na Togo.