BAB' KUBWA 2024 ulikuwa mwaka wa mafanikio kisoka
Muktasari:
- Tangu mwanzo wa mwaka, tumeshuhudia hatua za kujivunia kutoka kwa Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa, rekodi za Taifa Stars, na maendeleo ya vijana kupitia timu kama Ngorongoro Heroes.
MWAKA 2024 umekuwa wa kihistoria kwa maendeleo ya soka Tanzania, ukionyesha ukuaji mkubwa wa mchezo huo kupitia mafanikio ya klabu na timu za taifa.
Tangu mwanzo wa mwaka, tumeshuhudia hatua za kujivunia kutoka kwa Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa, rekodi za Taifa Stars, na maendeleo ya vijana kupitia timu kama Ngorongoro Heroes.
Aidha, tukio kubwa la Tanzania kushirikiana na Kenya na Uganda kushinda tenda ya kuwa wenyeji wa mashindano ya Afcon 2027 inaendelea kudhihirisha kwamba soka la Tanzania limeingia katika enzi mpya ya mafanikio.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametoa pongezi kubwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha michezo, akisema msaada wake umekuwa msingi wa maendeleo haya.
Tukianza na mafanikio ya klabu, Simba na Yanga zilitengeneza historia ya kipekee kwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa pamoja. Huu ulikuwa ni ushahidi wa dhamira yao na uwekezaji wa muda mrefu wa klabu hizo, zikiiweka Tanzania kwenye ramani ya soka ya kimataifa.
Rais Wallace Karia amezipongeza klabu hizi kwa kuwa mabalozi wa nchi, akisema: “Mafanikio haya yanaimarisha jina la Tanzania katika soka la Afrika, lakini hayawezi kufanikishwa bila mazingira mazuri ambayo serikali imeyajenga.”
Mafanikio ya Taifa Stars kufuzu kwa mara ya nne kwenye michuano ya AFCON ni hatua nyingine muhimu mwaka huu. Timu hiyo imeonyesha ukuaji mkubwa, safari hii ikiongozwa na kocha mzawa, Hemed Suleiman ‘Morocco’.
SIMBA, YANGA KIMATAIFA
Kwa mara ya kwanza Machi mwaka huu, Simba na Yanga ziliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabigwa Afrika kwa pamoja ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.
Simba ilifuzu hatua hiyo, baada ya kuichapa Jwaneng Galaxy mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, huku Yanga ikifanikiwa kufuzu wiki moja nyuma kwa kuifumua CR Belouizdad mabao 4-0, kwenye uwanja huohuo.
Kufuzu kwa timu zote ilikuwa ni jambo la kujivunia kwa kila Mtanzania kwa kuwa ndiyo nchi pekee ambayo ilipeleka timu mbili robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo.
Timu hizo ziliweka rekodi ya kumaliza hatua ya makundi zikiwa zimefunga mabao mengi zaidi kuliko nyingine zote, baada ya kila moja kufunga mabao tisa zikifuatiwa na Belouizdad, Mamelodi Sundowns na Asec Mimosas ambazo kila moja ilifunga mabao saba, Esperance de Tunis ilifuzu ikiwa imefunga mabao sita sawa na TP Mazembe.
Rekodi nyingine ambayo iliwekwa na timu hizo mbili zikiwa ndiyo pekee ambazo zilishinda michezo miwili tu ya hatua ya makundi, lakini zikapenya kwenda robo fainali.
Simba ilishinda nyumbani dhidi ya Wydad Casablanca 2-0 na Jwaneng Galaxy mabao 6-0, huku Yanga ikishinda dhidi ya CR Belouazdad 4-0 na Medeama 3-0.
BAADA YA MIAKA 35
Mei mwaka huu, Wagosi wa Kaya, Coastal Union walijihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya CAF kwa kutoka suluhu na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, baada ya kufikisha pointi 42.
KMC ilikuwa na uwezo wa kuzifikia pointi hizo 42, lakini kipigo kutoka kwa Simba kilitibulia na kuiacha ibaki katika nafasi ya nne.
Matokeo ya KMC yakairahisishia Coastal kukata tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa ikiwa ni baada ya miaka 35.
Mara ya mwisho kwa Coastal kushiriki michuano ya kimataifa ilikuwa mwaka 1989 iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika na kuishia raundi ya kwanza. Michuano hiyo ilikuja kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004.
Coastal ilikuwa timu ya sita kukata tiketi ya CAF kwa kumaliza ligi katika nafasi ya nne baada ya KMC, Namungo, Biashara United, Geita Gold na Singida Fountain Gate, kupitia njia hiyo katika misimu iliyotangulia kutokana na Tanzania Bara kupewa nafasi ya timu nne katika michuano hiyo, mbili zikicheza Ligi ya Mabingwa na nyingine Kombe la Shirikisho.
TAIFA STARS YAFUZU AFCON
Novemba mwaka huu, Taifa Stars iliandika historia kwa kufuzu kucheza AFCON kwa mara ya nne baada ya kuifunga Guinea bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva dakika ya 61 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Stars ilifuzu kwa kumaliza nafasi ya pili ikiwa na alama 10 huku DR Congo ikiongoza kundi kwa alama 12 wakati Guinea alimaliza na alama 9 katika nafasi ya tatu.
Safari ya Tanzania kwenye AFCON ilianza mwaka 1980, ambapo Taifa Stars ilifuzu kwa mara ya kwanza chini ya kocha wa kigeni, Slawomir Wolk kutoka Poland. Licha ya kuwa mara ya kwanza, timu hiyo ilijitahidi kupambana, lakini ushindani wa kipindi hicho ulikuwa mgumu zaidi.
Miaka 39 ilipita kabla ya Taifa Stars kurejea kwenye mashindano haya ya kifahari mwaka 2019, safari hii chini ya Emmanuel Amunike kutoka Nigeria.
Mwaka 2023, chini ya Adel Amrouche wa Algeria, Taifa Stars ilirejea tena kwenye michuano ya AFCON. Hata hivyo, mafanikio ya mwaka huu yameweka historia, kwani hii ni mara ya kwanza kwa timu kufuzu chini ya mwongozo wa kocha mzawa. Hemed Suleiman ‘Morocco’.
“Tulikaa na kuamua kila mmoja kujitoa na kufanya vizuri katika michezo miwili iliyokuwa mbele yetu baada ya kupoteza dhidi ya DR Congo, tuliona kuwa bado tuna nafasi na kweli tuliweza kufanikisha hilo, haikuwa rahisi,” anasema kocha huyo mzawa.
TWIGA STARS YAPANGIWA VIGOGO
Timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ ilifahamu kundi na wapinzani wake katika fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (Wafcon) 2024 zitakazifanyika mwakani kuanzia Julai 5 hadi Julai 26 huko Morocco. Imewekwa kundi C na timu za Afrika Kusini, Ghana na Mali.
Hii ni mara ya pili kwa Twiga Stars kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake ambapo ya kwanza ilishiriki katika fainali za 2010 zilizofanyika Afrika Kusini na ilimaliza ikiwa imeshika mkia kwenye kundi lake ikitoka sare mechi moja na kupoteza mbili.
NGORONGORO WAMO
Oktoba mwaka huu, Tanzania ilikata tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Uganda katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) U20 kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Ngorongoro Heroes inayofundishwa na kocha mzoefu, Charles Boniface Mkwasa anayesaidiwa na Kally Ongala na Juma Kaseja, kocha wa makipa, kwani ililazimika kutoka nyuma baada ya beki Brian Toto Majub kuanza kuifungia Hippos katika dakika ya 46.
Winga wa KVZ ya Ligi Kuu ya Zanzibar, Sabri Dahary Kondo aliirejesha mchezoni Ngorongoro kwa bao lake zuri la kusawazisha katika dakika ya 73 ambalo lilisindikizwa nyavuni na kipa wa Hippos, Abdu Magada na dakika 90 zikamalika timu hizo zikiwa zimefungana 1-1.
Shujaa wa Tanzania alikuwa mshambuliaji wa JKU ya Ligi Kuu ya PBZ Zanzibar, Jammy Suleiman Simba aliyeifungia Ngorongoro Heroes bao la ushindi dakika ya 119 na kuamsha shangwe kubwa kwa mamia ya mashabiki waliojitokeza kwenye Uwanja wa KMC. Vijana hao walitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuifunga Kenya mabao 2-1.