Aucho aeleza siri za mafanikio yake Yanga

Muktasari:
- Mchezaji huyo wa kimataifa ambaye aliwahi kuzichezea Red Star Belgrade ya Serbia, ameonyesha kwa vitendo kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, na zaidi ya yote, ni mfano wa nidhamu, uvumilivu, na mapenzi kwa soka. Katika mahojiano yetu na Khalid, tulipata nafasi ya kujua zaidi kuhusu safari yake ya kisoka, changamoto alizokutana nazo, na mbinu zinazomfanya kuwa bora.
KHALID Aucho ni jina linalojulikana vizuri katika medani ya soka la Tanzania na ukanda huu wa Afrika Mashariki, haswa kutokana na mchango wake katika klabu ya Yanga na timu yake ya taifa la Uganda.
Mchezaji huyo wa kimataifa ambaye aliwahi kuzichezea Red Star Belgrade ya Serbia, ameonyesha kwa vitendo kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, na zaidi ya yote, ni mfano wa nidhamu, uvumilivu, na mapenzi kwa soka. Katika mahojiano yetu na Khalid, tulipata nafasi ya kujua zaidi kuhusu safari yake ya kisoka, changamoto alizokutana nazo, na mbinu zinazomfanya kuwa bora.
Tangu alipojiunga na Yanga Agosti, 2021, Aucho ameonyesha kiwango cha juu, akifanya kazi kwa bidii ili kusaidia timu yake kutimiza malengo yake. Lakini siyo tu uwezo wake uwanjani unamfanya kuwa maarufu, pia anajulikana kwa utu wake na mtazamo wa kujitolea kwa kila kitu anachofanya, awe uwanjani au nje ya uwanja. Katika mahojiano haya, Aucho alijitokeza kama mchezaji anayejua kwamba mafanikio katika soka yanahitaji juhudi, nidhamu, na, zaidi ya yote, kuamini katika uwezo wake.
MSINGI WA MAFANIKIO
Katika suala la kuwa mchezaji bora, Aucho anaelezea jinsi anavyothamini sana umuhimu wa kupumzika na kujali mwili wake. “Kupumzika na kuutunza mwili wangu,” ndivyo alivyosema Khalid alipoulizwa ni mambo gani yanamfanya kuwa mchezaji bora. Aucho amekiri kuwa siri ya mafanikio yake inapatikana kwenye kujali kupumzika na kufanya mazoezi ya ziada.

UREJEO WAKE UWANJANI
Kipindi fulani Aucho alikumbana na majeraha ambayo yalimweka nje ya uwanja kwa wiki kadhaa, lakini alipoulizwa kuhusu kurudi kwake uwanjani, alionyesha furaha na kutokuwa na wasiwasi.
“Najisikia vizuri na furaha kuona kuwa nimerudi kwa nguvu,” anasema.
Anasema kuwa kurejea uwanjani baada ya kuumia inahitaji uvumilivu na kujiamini kwa hali ya juu, kwani wakati mwingine wachezaji huwa wanakutana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki na vyombo vya habari.
LIGI INAVYOZIDI KUKUA
Aucho anasisitiza kuwa ligi ya Tanzania inakuwa bora na yenye ushindani kila uchao. “Ushindani unakuwa mkubwa kila msimu,” anasema, akiongeza kwamba timu nyingi sasa zinajitahidi kuwa na wachezaji bora na kuendeleza mbinu za kisasa. Hii ni hali ambayo imewafanya wachezaji na mashabiki kushuhudia ushindani katika kila msimu.Aucho anaamini, mafanikio ya timu hayategemei tu vipaji vya wachezaji, bali pia nidhamu na umoja wa timu, jambo ambalo Yanga imekuwa ikilifanya kwa miaka mingi.

KUKUTANA NA CHAMA
Mwanzoni mwa msimu, Yanga ilipata saini ya Clatous Chama. Aucho anaeleza furaha yake ya kushirikiana uwanjani na mchezaji huyo ambaye alikuwa akivutiwa naye tangu akiwa kwa wapinzani wao, Simba.
“Yeye ni mchezaji mzuri na mtu mnyenyekevu,” anasema Khalid, akionyesha jinsi anavyothamini kiwango cha Chama kwenye timu.
Anapokuwa uwanjani, Aucho anasema anapenda kucheza na mchezaji anayefanya mambo kuwa rahisi, kwani huu ni mtindo ambao unarahisisha mchezo wa timu nzima.
Kwa Aucho, ushirikiano huu unaleta nguvu na kasi kubwa uwanjani, na ni moja ya sababu zinazowafanya Yanga kuwa na uwezo mkubwa wa kushindana na timu nyingine kubwa za ligi.

CHANGAMOTO MSIMU HUU
Pamoja na mafanikio, msimu huu ulianza kwa changamoto kubwa kwa Yanga, hasa katika michuano ya kimataifa.
Aucho anaeleza kuwa bado kuna nafasi ya kuboresha matokeo yao kufuatia kupoteza michezo miwili dhidi ya Al Hilal na MC Alger huku wakitoa sare dhidi ya TP Mazembe.
“Tunaendelea kupambana. Hatuwezi kukata tamaa mapema,” anasema.
Aucho anasema, ni muhimu kuwa na mtazamo wa kupambana hadi mwisho, na kwa kushirikiana kama timu, matokeo mazuri yanaweza kuja muda wowote.
Akiwa na matumaini makubwa, Aucho anaongeza kuwa “kama tutashinda michezo ijayo, tunaweza kusema tutakuwa katika nafasi ya kusonga mbele.”

SIMBA NA MBIO ZA UBINGWA
Aucho anakiri kuwa Simba ni timu nzuri na kwamba ushindani wao unazidi kuwa mkubwa.
Anasema kuwa Simba wameboresha mbinu zao za kisoka na wameongeza kasi, jambo ambalo linaongeza ugumu wa mbio za ubingwa. Hata hivyo, alisisitiza kwamba ushindani huo ni mzuri kwa soka la Tanzania. “Ushindani huu una faida kwa ligi ya Tanzania,” anasema staa huyo.
, akionyesha kwamba wakati Simba ni wapinzani wakubwa, wao pia wanachangia kuboresha ligi na kuiweka katika kiwango cha kimataifa.
Kwa Aucho, yeye huheshimu ushindani kutoka kwa Simba, lakini bado anajivunia mafanikio ya timu yake na kujitahidi kuonyesha kiwango cha juu kila wakati.
ALIVYOCHUKULIA KUKOSOLEWA
Kama mchezaji mkubwa, Aucho anapitia changamoto ya kukosolewa kutoka kwa mashabiki na vyombo vya habari. Aliweka wazi kwamba, tangu alivyokuwa mdogo nyumbani kwao Uganda, alikuwa akikutana na mashabiki waliokuwa wakimkosoa kwa kila alichofanya.
“Nimezoea hiyo hali. Katika nchi yangu ya Uganda, watu wanakukosoa kila wakati,” anasema Aucho. Anasema kuwa ni muhimu kuwa na mtazamo mzuri na kujua jinsi ya kukabiliana na watu wanaokosoa, kwani soka ni mchezo wa maoni na si kila mtu atakubaliana na wewe.
FAMILIA NDO KILA KITU
Aucho mwenye watoto wawili, aasisitiza kuwa aliweza kufika mbali zaidi kutokana na msukuo wa familia yake.
“Nikiwaza kuhusu watoto wangu, naona ni lazima niende kazini kila siku,” anasema Aucho.