AKILI ZA KIJIWENI: Wale Al Ahly wamefika fainali bwana

WANAKUAMBIA kila shetani na mbuyu wake aiseeh na kilichofanywa na Al Ahly msimu huu kinaweza kuthibitisha hilo.

Jamaa walianza kwa kusuasua sana katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu hadi kupelekea baadhi ya watu kuwatabiria kuwa hawatofika mbali kama ambavyo wamezoeleka kufanya.

Hata hivyo tunaoyafahamu vyema mashindano hayo na historia ya Al Ahly tuliwahonya waliokuwa wakiibeza na kuwataka waweke akiba ya maneno kwa sababu wale watu  sio wa kuwadharau pindi linapokuwa suala la Ligi ya Mabingwa mikononi mwao.

Wakati walipokuwa kwenye hatua ya makundi, kulikuwa na uwezekano wa Al Ahly kutupwa nje ya mashindano kwani walikuwa wanaomba Mungu kweli kutokana na nafasi finyu ya kusonga mbele ambayo walikuwa nayo.

Nafasi ya kutolewa ilikuwepo kama Al Hilal ya Sudan ingepata ushindi katika mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Mamelodi Sundowns lakini mwisho wa siku mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1.

Ni mechi ambayo Al Hilal walipata penalti wakakosa lakini pia Mamelodi Sundowns haikupanga kikosi chake kilichokamilika.
Baada ya kupenya mtego huo, Al Ahly wakawa binadamu wengine na sasa wanasubiria mechi mbili za fainali ambazo watacheza na Wydad Casablanca.

Jamaa ni kama wanayamiliki hayo mashindano aiseeh maana hata kama wakianza vibaya, ukiona wameingia robo fainali tu basi ujue utawakamata fainali ama watachukua kabisa kombe lenyewe.