AKILI ZA KIJIWENI: Milioni 4 za Fei Toto zingenitosha kula kuku

NIPO kijiweni na washkaji zangu ukaibuka mjadala wa malalamiko ya mama wa Fei Toto kuwa mwanaye kuna nyakati alikuwa anakula ugali na sukari na amechoka kuichezea Yanga.
Suala la kuchoka kuichezea Yanga halikuwa msingi mkubwa wa mjadala wetu kwani Fei Toto ni muajiriwa tu wa Yanga na haimaanishi kuwa angeichezea milele.

Kuna wakati angeondoka tu iwe kwa kuuzwa kwenda kwingine, kuachwa au kustaafu soka lakini kiuhalisia asingeichezea milele.
Wanangu wa kijiweni walikuwa wanafikiria suala la kijana kula ugali na sukari kuonyesha kuwa kile ambacho anakipata kwa sasa hakimtoshi

Ilibainika kuwa Yanga inamlipa Fei Toto mshahara wa takribani Sh 4 milioni kwa mwezi ambao ndio kijana anataka uongezwe.
Masela kijiweni kila mmoja anafikiria angekuwa analipwa kiasi hicho cha fedha na anafafanua namna ambayo ingemtosha kutumia kwa kula na matumizi mengine na ikabakia kupigia mishe nyingine.

Basi nami nikaona nichangie namna ambavyo ningeweza kuishi kwa kipato hicho cha mshahara pasipo kula ugali na sukari.
Nimewakumbusha washkaji kijiweni kuwa kuku mzima wa kienyeji anauzwa kwa Sh 25,000 na iwapo ukiamua yule kuku wa kienyeji kila siku, maana yake utatumia Sh 750,000 tu kwa mwezi mzima na hivyo utabakiwa na Sh 3,250,000 kutoka katika Sh 4 milioni unayolipwa mshahara.
Lakini ukiamua kula kuku wawili kwa kila siku, maana yake kwa mwezi utatumia Sh 1.5 milioni ya kununulia kuku wa kula tu na ugali wako huku ukibakiwa na Sh 2.5 milioni.
Kwenye suala la kula nisingeteseka na kufikia hatua ya kula ugali na sukari. Kwanini iwe hivyo na Sh 4 milioni ingenitosha kula vizuri na chenji ikabakia?

Ningeweza kuamua kununua unga kilo mia, mchele kilo mia, maharage kilo mia na nyama kilo mia na bado akiba nyingi ya fedha ingebakia mfukoni.
Mchele wa daraja la juu unaweza kuwa kilo Sh 5000. Maana yake nikinunua kilo mia nitatumia Sh 500,000 tu.
Nikinunua maharage kilo mia maana yake nitatumia Sh 400,000 tu na nikinunua nyama kilo mia maana yake nitatumia Sh 800,000 tu.

Ningeweza kununua mbuzi 10 pale Vingunguti nikafuga halafu nikawa na uhakika wa kitoweo endelevu cha kula na ugali wangu au wali badala ya sukari.

Kama kufuga ni tabu bado ningeweza kununua mbuzi mmoja kila siku nikachinja na kupata kitoweo na bado kuna kama Sh 1 milioni ingebakia mfukoni ambayo ningefanyia mambo mengine.
Samaki wa Sh 20,000 tu kwa siku wangenitosha kufanya kitoweo ambapo kwa mwezi ningetumia Sh 600,000 tu na bado ningebaki na Sh 3,400,000 ya kutesea mitaani.

Kiukweli Sh 4 milioni ni nyingi na inatosha kupata mboga ya kueleweka kwa ajili ya msosi, kijana wetu usikute alipenda tu kula ugali na sukari.