Ahoua kaiacha miguu izungumze zaidi

Muktasari:
- Kipa anapimwa kwa kuzuia nyavu zake zisitikiswe akitumia mikono. Ili kumpata kipa bora, clean sheet zinahusika.
KATIKA timu, tathmini ya mchezaji hufanyika kulingana na nafasi yake. Kila nafasi kuna cha kuangalia ili kufahamu mchezaji husika amefanya nini.
Kipa anapimwa kwa kuzuia nyavu zake zisitikiswe akitumia mikono. Ili kumpata kipa bora, clean sheet zinahusika.
Ukija kwa mabeki, nao wana kazi ya kuzuia mpira usiingie golini kwao wakitumia miguu na beki mzuri ni yule mwenye uwezo wa kucheza mipira ya juu na chini.
Hali kadhalika kiungo mkabaji kazi yake kwanza kusaidia ulinzi, kisha kuiunganisha timu kutoka nyuma kwenda mbele.

Viungo washambuliaji wana kazi mbili, kutengeneza mabao na kufunga huku washambuliaji kazi yao kubwa ni kufunga, suala la kutengeneza nafasi ni jambo la pili.
Ukiangalia katika kikosi cha Simba, unakutana na nyota Jean Charles Ahoua ambaye msimu uliopita alikuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Ahoua kwa nafasi ya kiungo mshambuliaji anayocheza anaonekana kuifanya kazi yake inavyotakiwa. Ana uwezo wa kufunga, kuchezesha timu na kutengeneza nafasi kwa wachezaji wenzake kitu ambacho hadi sasa amekionyesha ikiwa ni mapema sana kwani hata hajamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi.

Kiungo huyo ambaye ni kati ya wachezaji wapya 15 waliosajiliwa na Simba kipindi cha dirisha kubwa msimu huu kabla ya dirisha dogo kuongeza Ellie Mpanzu, namba zake hadi sasa zinamfanya kumuweka kwenye daraja la waliofanikiwa.
Ingawa wapo wanaosema uchezaji wake unategemea zaidi timu kuwa bora ndiyo afanye vizuri, lakini mwenyewe ameamua kutowajibu kwa kufungua mdomo zaidi ya kuiacha miguu yake izungumze. Ukweli, namba zinambeba.
Kabla hatujaenda mbali, Ahoua ndiye mchezaji aliyecheza kwa dakika nyingi Ligi Kuu Bara msimu huu kati ya nyota wapya waliosajiliwa na Simba nyuma ya kipa Moussa Camara.
Wakati Camara akicheza mechi zote 13 kwa dakika 1170, Ahoua amecheza dakika 832 katika mechi 12 alikosekana mechi moja dhidi ya Tanzania Prisons.

Hiyo inadhihirisha Ahoua ni miongoni mwa wachezaji muhimu wa kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha, Fadlu Davids aliyeshinda Tuzo ya Kocha Bora mwezi Agosti sambamba na Ahoua aliyebeba ile ya Mchezaji Bora mwezi huo.
LIGI KUU BARA
Katika Ligi Kuu Bara, Ahoua anashika nafasi ya pili kwa wachezaji wenye asisti nyingi nyuma ya Feisal Salum 'Fei Toto' mwenye saba wakati yeye anazo nne.
Pia mabao yake sita yanamfanya kumfikia Seleman Mwalimu wa Fountain Gate ambaye awali alikuwa kinara wa ufungaji kabla ya kupitwa na Elvis Rupia anayecheza Singida Black Stars akifunga saba.
Ndani ya kikosi cha Simba, Ahoua amehusika kwenye mabao 10 kati ya 28 yaliyofungwa na timu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 34 ikishuka dimbani mara 13.

Kiungo huyo mabao yake sita ameyagawa katika maeneo matatu. Penalti amefunga mbili, faulo moja na yale ya kawaida matatu.
Ahoua alianza msimu vizuri kwani mwezi Agosti wakati ligi ikiwa ndio kwanza imeanza alibeba Tuzo ya Mchezaji Bora mwezi huo.
KIMATAIFA
Ahoua amecheza mechi zote tano za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kuanzia hatua ya mtoano hadi sasa makundi.
Ukiangalia katika mechi hizo, mchango wa Ahoua unaonekana kwani amefunga bao moja na kutoa asisti mbili tangu hatua ya makundi ianze.
Alifunga bao moja kwa penalti wakati Simba ikishinda 1-0 dhidi ya Bravos, kisha akatoa asisti dhidi ya CS Constantine na Mohamed Hussein 'Tshabalala' alifunga Simba ikichapwa 2-1 ugenini.
Kiungo huyo pia alitoa asisti katika bao la kusawazisha dhidi ya CS Sfaxien lililofungwa na Kibu Denis, siku ambayo Simba ilishinda 2-1 nyumbani.
Ahoua aliyezaliwa mwaka 2002, jijini Zikisso, Ivory Coast, anaitumikia Simba akitokea Stella Club d’Adjamé ya nchini huko.
Ikumbukwe wakati anashinda Tuzo ya Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita 2023/24, alifunga mabao 12 na asisti timu.

Ukiangalia takwimu zake hizo za msimu uliopita kama akiendelea na mwendo wake huu alioanza nao ni wazi atazivuka kwani amebakiwa na mabao sita na asisti tano.
MSIKIE MWENYEWE
Hivi karibuni, Ahoua aliliambia Mwanaspoti kitu cha kwanza anachokifanya uwanjani ni kuwatengenezea nafasi wenzake na ikitokea nafasi ya kufunga inabidi aitumie.
"Ninataka kutangulia kwanza kuwatengenezea nafasi washambuliaji kwa kutoa asisti lakini kama nitapata nafasi nitafunga kwa kuwa najua kufunga," alisema Ahoua.
TAKWIMU NYOTA WAPYA SIMBA
MOUSSA CAMARA
DAKIKA: 1170
MECHI: 13
CLEANSHEET: 10
KELVIN KIJILI
DAKIKA: 222
MECHI: 07
MABAO: 00
ASISTI: 00
VALENTINE NOUMA
MECHI: 365
MECHI: 06
MABAO: 00
ASISTI: 01
ABDULRAZACK HAMZA
DAKIKA: 620
MECHI: 08
MABAO: 00
ASISTI: 00
CHAMOU KARABOUE
DAKIKA: 642
MECHI: 08
MABAO: 00
ASISTI: 00
AWESU AWESU
DAKIKA: 544
MECHI: 12
MABAO: 02
ASISTI: 01
DEBORA FERNANDEZ MAVAMBO
DAKIKA: 774
MECHI: 11
MABAO: 01
ASISTI: 00
AUGUSTINE OKEJEPHA
DAKIKA: 510
MECHI: 10
MABAO: 00
ASISTI: 00
JOSHUA MUTALE
DAKIKA: 407
MECHI: 09
MABAO: 00
ASISTI: 00
OMARY OMARY
DAKIKA: 55
MECHI: 02
MABAO: 00
ASISTI: 00
YUSUPH KAGOMA
DAKIKA: 158
MECHI: 04
MABAO: 00
ASISTI: 00
JEAN CHARLES AHOUA
DAKIKA: 832
MECHI: 12
MABAO: 06
ASISTI: 04
VALENTINO MASHAKA
DAKIKA: 68
MECHI: 02
MABAO: 02
ASISTI: 00
STEVEN MUKWALA
DAKIKA: 509
MECHI: 13
MABAO: 04
ASISTI: 02
LEONEL ATEBA
DAKIKA: 667
MECHI: 09
MABAO: 05
ASISTI: 01
ELIE MPANZU
DAKIKA: 57
MECHI: 01
MABAO: 00
ASISTI: 00