Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usajili Van Der Schaaf atamani Barka arejee Uholanzi

Usajili Van Der Schaaf atamani Barka arejee Uholanzi

KOCHA wa zamani wa timu ya wanawake ya Ajax, Maarten van der Schaaf amejikuta akimkumbuka mchezaji kinda wa Kitanzania, Barka Mpanda na kusema anatamani kumwona kijana huyo akirejea tena Uholanzi kupigania ndoto zake.

Wakati Barka akiwa Amsterdam, Uholanzi kwenye kliniki ya Ajax kwa wiki tatu alipata nafasi ya kufanya mazoezi binafsi na kocha huyo.

Maarten alimposti Barka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram na kueleza kuwa amefurahia kupata nafasi ya kufanya mazoezi na kijana huyo wa Kitanzania ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kile ambacho alikuwa akikifanya.

Siku hizi dunia ni kama kijiji tu kutokana na utandawazi uliopo hivyo ilikuwa rahisi kusambaa kwa video ambazo zilikuwa zikionyesha vile ambavyo kijana huyo wa Kitanzania alikuwa akifanya makubwa kwenye kliniki hiyo iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana, 2021.

Gazeti hii lilitafuta mawasiliano na kocha huyo na kuongea naye mawili matatu kuhusiana na Barka ambaye alimtaja kuwa miongoni mwa makinda wenye vipaji vikubwa ambao amewahi kupata nafasi ya kufanya nao programu za mazoezi.

“Siwezi kuficha maana nilifurahishwa naye, nilipata muda wa kumsoma vizuri na kuona kile ambacho kipo ndani yake. Anatakiwa kuwa chini ya uangalizi ili kukilea kipaji chake na kumfanya afikie malengo, ana shauku ndani yake na msukumo mkubwa,”

“Ni jambo zuri kwa mtoto kuwa na msukumo maana utamfanya kufanya mara mbili ya mambo ambayo hufanywa na mchezaji wa kawaida, nilitamani kuendelea kuwa naye hapa tukifanya mazoezi pamoja lakini hilo halikuwa ndani ya uwezo wangu,

“Lakini naamini kuwa atarejea tena maana alifanya vizuri kwenye ile kliniki. Alichonacho ndani yake ni kitu kikubwa, ni mwepesi na mwenye kushika maelekezo kwa haraka, hilo ni jambo muhimu na kubwa kwa mtoto,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya wanawake ya Ajax, hakuishia hapo aliendelea kumzungumzia Barka kwa kusema ni vizuri kwa wazazi kutambua vipaji vya vijana wao maana hilo linaonekana kuwa tatizo kwa familia nyingi za Kiafrika.

“Ni rahisi kumtengeneza kijana angali akiwa mdogo na kumfanya afanye makubwa kwa miaka ya baadaye, inawezekana kuwa na Messi pamoja na Ronaldo kutoka Afrika na kuitikisa dunia kama walivyofanya wawili hao kwa zaidi ya miaka 10,” alisema.

Hivi karibuni Barka ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka 2021 kwenye ile kliniki ya vijana ambayo alienda kufanya Uholanzi kwenye klabu hiyo ya Ajax.

Kijana huyo wa Kitanzania amewazidi kete zaidi ya vijana 500 kutoka mataifa mbalimbali.

Ndani ya wiki tatu ambazo alikuwa Uholanzi, Barka alitwaa tuzo mbalimbali ikiwemo mjuzi bora wa wiki na mchezaji mwenye thamani zaidi ndani ya uwanja (MVP).

Kwa mujibu wa baba wa kijana huyo, Seif Mpanda, kurudi Uholanzi kwa kijana wake ni suala la muda hivyo mambo yakiwa tayari watawatangazia Watanzania hivyo amwataka kuwa na subira kipindi hiki ambacho mazungumzo yanaendelea.

“Tuna mawasiliano ya karibu na watu wa Ajax. Sipendi kusema vitu ambavyo vipo nusu nusu tusubiri kila kitu tutakiweka wazi,” alisema Mpanda.

Kipindi hiki ambacho yupo nchini, Barka amekuwa akifanya programu mbalimbali za mazoezi binafsi chini ya kocha Mjerumani, Martin Hammel.