Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CHAN 2009 (7) : Tatizo letu kubwa ni kwamba hatujifunzi

IMEICHUKUA Tanzania miaka 11 kurejea tena katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan). Kila nikitazama nyuma, naona kwamba tungetakiwa kushiriki walau mara mbili zaidi.

Kwanini? Kwa sababu mbili kubwa. Mosi ni kwamba nadhani baada ya kushiriki katika mashindano ya kwanza ya mwaka 2009, tungekuwa na uchu zaidi wa kushiriki tena na tena. Nchi zote za mpira barani Afrika huhakikisha zinakwenda Chan.

Sababu ya pili ni binafsi zaidi kwangu. Nadhani kwamba kuna wakati tulikuwa na kikosi kizuri zaidi kuliko kile tulichokuwa nacho wakati wa Marcio Maximo.


NINA MIFANO KADHAA

Golini, Juma Kaseja alikuwa bora wakati Maximo akiwa kocha. Hata hivyo, ninaamini alikuwa katika ubora zaidi kati ya mwaka 2010 hadi 2014. Kila mchezaji ana wakati ambao ana kiwango cha juu zaidi na nadhani Kaseja alikuwa bora zaidi wakati huo.

Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani walikomaa zaidi baada ya Maximo kuondoka. Kina Athumani Iddi, Haruna Moshi ‘Boban’, Saimon Msuva, Shomari Kapombe, Mrisho Ngassa, John Bocco na wengine walikuwa na uwezo wa kucheza kwenye kikosi chochote cha Stars kwa miaka 10 iliyopita.

Tatizo ni kwamba makosa yetu- karibu mara zote; ni yaleyale. Kwa sababu tulienda na raia wa Brazil; mwaka 2009, ni muhimu nikaeleza kuhusu mapungufu yetu kwa kuangalia walau Wabrazili wanafanya nini.


NIDHAMU WACHEZAJI

Wabrazili wanajua umuhimu wa nidhamu kwa wachezaji. Hata hivyo, wanajua pia kwamba kuna vitu huwezi kumfundisha mtu mzima.

Mchezaji ambaye amezaliwa na kukulia kwenye ‘magheto’ huwezi kumfunza tabia njema akiwa mtu mzima. Unachotakiwa kufanya ni kuelekeza akili yake katika mchezo na kutumia kipaji chake inavyostahili.

Wengi wa wachezaji wa Kitanzania ambao wanaonekana hawana nidhamu, ndiyo haohao ambao wamecheza mpira kwa muda mrefu na wengine wanaweza kucheza hadi leo.

Walikuwa na matatizo yao lakini mapenzi yao kwa soka yalikuwa makubwa sana.

Kuna waliohitaji msaada wa kisaikolojia ili waweze kujumuika na wenzao vizuri na kuna wanaohitaji kuachwa tu wafanye mambo yao.

Kuna mchezaji mmoja mashuhuri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambaye niliwahi kushuhudia akifuatwa hotelini kwenda kucheza mpira. Hakuwa na wenzake na alikuwa kwenye starehe zake.

Katika mechi hiyo niliyomshuhudia akiwa amefuatwa kutoka hotelini, ilimchukua dakika nane tu kupachika bao la kwanza na nusu saa baadaye akacheka na nyavu tena, bonge la mchezaji.

Hiyo si tabia nzuri na ameshindwa kucheza U;aya kwa sababu hiyo lakini kaipa DRC mataji ya kutosha na k;abu yake ya TP Mazembe imefaidika sana na kipaji chake. Wanachofanya ni kuishi na mchezaji kwa namna alivyo.

Nasikitika kwamba Stars haikufaidika sana na vipaji vya wachezaji kama Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Moshi ‘Boban’, Ramadhani Chomboh na wengine kwa sababu pengine tulitaka wafiti kwenye tabia zetu badala ya sisi kuwakubali kama walivyo.

Ukiambiwa vituko vya kina Maradona, Ronaido de Lima, Ronaldinho, Romario, Paul Gascoigne ‘Gazza’, Paolo Rossi, Wayne Rooney na wengine kwenye kuishi nao ungeona kabisa wasingeweza kutoboa kwenye mfumo wetu wa kusaka wachezaji.


MAKOCHA

Umewahi kujiuliza ni kwa vipi Stars iliamua kuwa na Charles Boniface Mkwassa, Salum Mayanga, Kim Paulsen, Emmanuel Amunike na hata kwa Etienne Ndayiragije? Nini hasa ilikuwa falsafa ya kuwa nao?

Ukiangalia mechi za Stars wakati wa makocha hao, utaona kabisa zote ni timu ambazo hazifanani kabisa kimfumo. Sasa unajiuliza, ni nini falsafa yetu kama nchi linapokuja suala la kucheza soka?

Akiondoka Ndayiragije ni hili ni swali la kufikirika tu; ni kocha gani mzawa anaweza kupewa kazi hiyo na Watanzania wakakubali na kumheshimu? Kama hakuna mzawa wa namna hiyo, tunawezaje kupiga hatua katika soka kama hatuna walimu wetu wenyewe?

Imekuaje nchi ndogo kama Burundi jirani zetu, waweze kutoa makocha wenye viwango vya kuja kufundisha hapa kwetu ilhali sisi tukiwa hatuna makocha wa namna hiyo? Tuna watu wengi zaidi, wasomi wengi zaidi na uchumi mkubwa zaidi kuliko Burundi. Tunazidiwa kwenye nini?

Kama nilivyoandika katika mojawapo ya makala zangu za awali katika mfululizo huu, hakuna taifa lililopiga hatua katika soka duniani kwa kutumia makocha wa kigeni. Nchi zote zimeendelea kwa kutumia makocha wake wenyewe.

DRC itapiga hatua kwa sababu ina kina Ibenge na Mwinyi Zahera. Zambia kwa sababu ya kina Patrick Phiri na George Lwandamina. Misri itazidi kusumbua kwa sababu ina kina Hassan Shehata. Afrika Kusini nayo sasa imeanza kutengeneza makocha wa kiwango cha juu.

Ili tuendelee kisoka, tunahitaji kutengeneza kundi la makocha wazuri 100 walau kwa kuanzia, ambao wana uwezo wa kufundisha wachezaji wa rika mbalimbali na pengine makocha 20 wa kiwango cha juu kabisa kwa ajil ya vilabu vyetu na timu za taifa.

Hakuna namna nyingine ya kufanya maajabu zaidi ya hiyo. Tatizo letu ni kwamba nasi tunajifanya kama Chelsea ya England kwa kazi ya kufukuza na kuajiri makocha wapya kila kukicha.

Tunasahau kwamba wenzetu wanafanya hivyo kwa sababu wanajidai kwa vile wana wachezaji wengi wazuri.

Kwenye jambo hili la makocha kuna taasisi mbili ambazo zina wajibu wa kuja na majibu; Serikali na TFF.

Hakuna mwingine mwenye jukumu na uwezo wa kutekeleza hili zaidi ya wawili hawa.


Imeandikwa na Ezekiel Kamwaga