Ambundo, huyu jamaa anajua sana!

WAKENYA wanaujua mziki wake, kwani Gor Mahia waliamua kumbeba kutoka Alliance ya Mwanza, kabla ya kuja kutemana naye kutokana na ishu ya janga la Corona.

Gor Mahia iliamua kusitishiana mkataba kutokana na Ligi Kuu ya Kenya kusimama na kujikuta wakiingia matatani ya kutakiwa kumlipa malimbikizo ya mshahara na posho zake nyingine kutokana na agizo la Fifa naye kurejea nyumbani Tanzania na kujiunga na Dodoma Jiji.

Namzungumzia winga mahiri Dickson Ambundo anayevitoa mate vigogo wa Ligi Kuu Bara, huku kukiwa na tetesi kwamba huenda msimu ujao akaibukia Yanga kama mambo yataenda yalivyo.

Mbali na kunukia Yanga, lakini kocha wa Simba, Didier Gomes naye aliwahi kukaririwa akivutiwa na soka tamu la winga huyo aliyewahi kukipiga Mbao FC kabla ya kutengeneza jina kubwa akiwa na Alliance aliyepanda nao Ligi Kuu kabla ya kuitema na kwenda Kenya na chama lake hilo kushuka.

Ambundo ni mmoja ya mawinga mahiri wazawa wanaosumbua kwenye Ligi Kuu Bara akiwa sambamba na Ayoub Lyanga anayekipiga Azam.

Ni winga anayejituma uwanjani, ana chenga na maudhi na mwenye pua zinazojua kunusa nyavu vilipo, ndio maana katika msimu wake wa kwanza wa kucheza Ligi Kuu alimaliza na mabao 12 kiasi cha Wakenya kuvutiwa naye na kumsajili.


MBAO YAMCHOREA RAMANI

Msimu wa 2016-2017 ndio ulikuwa mwaka wake wa kwanza alioanza kucheza soka la ushindani baada ya kupanda na Mbao.

Akiwa na timu hiyo alicheza kwa kiwango kizuri lakini baada ya kuona mambo hayaendi aliamua kugeukia katika klabu ya Alliance ili kuendeleza soka lake.

Ambundo aliondoka Mbao na kwenda Alliance ambayo ilikuwa imepanda Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2017-2018.


AKIWASHA ALLIANCE

Ambundo akiwa na Alliance alikuwa katika kiwango kikubwa baada ya kuifungia timu hiyo mabao 12 katika msimu wake wa kwanza tu.

Ambundo anasifika kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga chenga pamoja na spidi kubwa ya kupeleka mashambulizi langoni mwa adui.

Kasi yake na utulivu wa mpira mguuni ndio silaha kubwa anayoitumia pindi anapokuwa uwanjani akitimiza majukumu yake.


WAKENYA WAMBEBA, ATUPIA MOJA CAF

Baada ya kung’ara akiwa na Alliance, matajiri wa Kenya, Gor Mahia walimsajili mchezaji huyo mwaka 2019 na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akiwa na timu hiyo kwenye mashindano yake yote, aliifungia bao moja Gor katika Ligi ya Mabingwa Afrika na baadaye aliondoka kutokana na kutolipwa stahiki zake.

Ambundo aliamua kuingia makubaliano ya kuondoka na Gor Mahia baada ya kutomaliziwa sehemu ya pesa za usajili wake pamoja na mishahara ambayo alikuwa anaidai timu hiyo.


AJIBANA MWAKA DODOMA

Baada ya kumalizana na Gor Mahia, Ambundo msimu huu alijiunga na Dodoma Jiji na kusaini mkataba wa mwaka moja tu wa kuitumikia timu hiyo.

Katika mkataba wake mpaka sasa tangu aanze kuutumikia amebakiza miezi miwili, mkataba wake unamalizika mwezi wa nane.

Licha ya kutoka nchini Kenya baada ya kuwa na misuko suko na Gor Mahia, Ambundo ameendelea kuwa katika kiwango kizuri katika timu ya Dodoma Jiji.


ANAASISTI NA KUFUNGA

Winga huyu mpaka sasa akiwa na Dodoma Jiji hajaacha kuonyesha kile ambacho kipo kwenye miguu yake baada ya kuifungia timu hiyo mabao matatu(3).

Licha ya kufunga Ambundo pia ametoa pasi za mabao saba (7) katika kuhakikisha washambuliaji wa timu yake wanafunga mabao muhimu ya kuibeba Dodoma Jiji.

Ambundo amekuwa miongoni mwa mawinga wazawa wanaofanya vizuri katika Ligi akikimbizana na Idd Seleman ‘Nado’ na Ayoub Lyanga wote wa Azam FC.