Zuchu, Nandy kama kawaida

Muktasari:
- Mwanaspoti limewambamba live waimbaji hao nyota maeneo ya Sinza Africa Sana, wakiwa pamoja wanapiga stori vizuri tu na wanacheka, huku wakitaniana.
KAMA ulidhani kuna bifu lolote linaloendelea baina ya Faustina Mfinanga ‘Nandy’ na Zuhura Othman ‘Zuchu’ basi jua hakuna kitu kama hicho, kwani wawili hao wanapiga umbea kama kawaida.
Mwanaspoti limewambamba live waimbaji hao nyota maeneo ya Sinza Africa Sana, wakiwa pamoja wanapiga stori vizuri tu na wanacheka, huku wakitaniana.
Nandy alipoulizwa na Mwanaspoti kuhusu madai ya kutoiva na Zuchu alisema ni uzushi tu kwani yeye na Zuchu ni marafiki na huwa mara nyingi wanakuwa pamoja, ila watu ndio wanatengeneza maneno ya kuwa hawaelewani.
“Nimeyasikia sana hayo maneno ya kuwa mimi na Zuchu hatuelewani, au eti ametengenezwa kwa ajili ya kunishusha kimuziki. Lakini napenda kuwaambia kwamba sisi tunapendana sana na Zuchu ni mdogo wangu na ananiheshimu sana,” alisema Nandy.
Pia Nandy alifafanua ili kazi za sanaa nchini Tanzania ziweze kwenda vizuri, watu waache kuzusha maneno ya uongo kwa wasanii.
“Baadhi ya mashabiki wetu wanapaswa wabadilike tabia za kugombanisha wasanii, tabia hii itashusha sanaa zetu zisiendelee,” alisema Nandy.
Zuchu si msanii wa kwanza wa kike kupewa tuhuma za kutengenezwa ili kumshusha mwingine, Linah alidaiwa kuandaliwa kuchukua nafasi ya Lady Jaydee, eti Recho aliandaliwa kumshusha Ray C.