ZIFF ya mwaka huu inaonyesha mwanga

Muktasari:
- Licha ya kuwa miongoni mwa matamasha makubwa ya filamu Afrika na kufanya vizuri kwenye maeneo mengi, lakini kwa miaka mingi nimegundua kitu kimoja ambacho nilikuwa nakitazama kama changamoto. Wasanii wa Tanzania kutovutiwa na tamasha hilo.
TAMASHA la kimataifa la filamu Zanzibar (ZIFF), ndiyo kongwe na kubwa la filamu Afrika Mashariki. Limekuwa likifanyika Zanzibar kwa miaka 28 sasa.
Licha ya kuwa miongoni mwa matamasha makubwa ya filamu Afrika na kufanya vizuri kwenye maeneo mengi, lakini kwa miaka mingi nimegundua kitu kimoja ambacho nilikuwa nakitazama kama changamoto. Wasanii wa Tanzania kutovutiwa na tamasha hilo.
Unakuta unasafiri kwenda Zenji unafika pale na kukuta orodha ndefu ya filamu kutoka kila kona ya dunia zinazoonyeshwa. Jumlisha wakufunzi kutoka maeneo mbalimbali duniani wanakuja kutoa mafunzo ya taaluma mbalimbali kwenye filamu.
Na bado pia kuna maprodyuza na kampuni za filamu zinakuja kutafuta wasanii wenye mawazo ya filamu na miradi ambayo ipo jikoni ili washirikiane kutengeneza kwenye ubora wa kimataifa, lakini ajabu ni kwamba hukuti wasanii wa Tanzania.
Mpaka nikawa najiuliza hawa wasanii wanashida gani? Kwanini hawaendi ZIFF licha ya fursa kama zote zilizojaa? Ni kwamba hawana muda? Hapana! Mbona kwenye matukio mengine tunawaona sana. Ni kwamba hawaoni faida? Sidhani! Mbona wasanii wachache wanaohudhuria ZIFF wanatoa ushuhuda wa mafanikio za tamasha hilo?
Sijawahi kujua shida ni nini inayofanya mwamko kuwa mdogo wa wasanii wa filamu wa Tanzania, lakini nachojua ni kwamba mwaka huu mambo yamekuwa tofauti. Wasanii wengi wamekwenda Zanzibar kuhudhuria tamasha hilo. Na sio wasanii tu, kazi zao pia zipo hapo na zinaonyeshwa. Ukumbi wa Ngome Kongwe umekuwa ukijaa kwa maonyesho ya filamu za Kitanzania.
Pengine huu ndiyo mwanzo wa ukurasa mpya wa tasnia ya filamu Tanzania. Pengine wasanii wetu wameanza kuelewa kuwa kazi ya sanaa siyo tu burudani kwa soko la ndani, bali pia bidhaa ya kiutamaduni inayoweza kusafiri na kuvuka mipaka.
Pia pengine tumekuwa tukiwalaumu wasanii wakati kumbe mfumo mzima ulikuwa hauwawezeshi. Vitu kama gharama za kuishi Zanzibar kwani wasanii wengi wa filamu Tanzania wanatokea Dar. Kwa hiyo kwenda Zenji kuna nauli, hoteli, chakula na mambo mengine. Pengine sasa wasanii wetu wana vibunda vinavyowawezesha kwenda Zenji kushiriki kwenye tamasha.
Kwa vyovyote vile kitu kimoja kipo wazi - ZIFF mwaka huu imekuwa fundisho. ZIFF siyo ya “watu wa nje”. Ni jukwaa la wasanii wa Afrika na Watanzania ni sehemu ya Afrika hiyohiyo. Tena kwa sababu jambo linafanyikiwa nyumbani, wasanii wa Tanzania ndo wanatakiwa kulichangamkia kuliko mtu yeyote.
Kipindi kama hiki, Ngoma Kongwe na Unguja kwa ujumla inatakiwa iwe imejaa wasanii wa filamu kama mawakala wa pesa mtandao, kila unapokatiza unakatana nao. Kinachoendelea mwaka huu ni mwanzo mzuri na dalili nzuri. Inaonyesha kwamba hatujachelewa. Inaonyesha kwamba hatujachelewa.