Diamond hajapokea tuzo YouTube bahati mbaya

Muktasari:
- Kwa matokeo hayo, Diamond anakuwa mwanamuziki wa kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kupata tuzo hizo ikiwa ni ya tatu baada ya hapo awali kupokea Silver Creator Award (kwa wafuatiliaji 100,000) na Gold Creator Award (1,000,000).
HIVI karibuni Diamond Platnumz, mwanamuziki wa Bongofleva, akiwa huko Marekani alikabidhiwa tuzo (Diamond Creator Award) kufuatia kufikisha wafuatiliaji (subscribers) milioni 10 katika mtandao wa YouTube aliojiunga nao Juni 12, 2011.
Kwa matokeo hayo, Diamond anakuwa mwanamuziki wa kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kupata tuzo hizo ikiwa ni ya tatu baada ya hapo awali kupokea Silver Creator Award (kwa wafuatiliaji 100,000) na Gold Creator Award (1,000,000).
Hivyo, kwa sasa Diamond amebakiza tuzo moja kutoka YouTube, nayo ni Red Diamond Creator Award ambayo hutolewa kwa kufikisha wafuatiliaji milioni 100, na hadi kufikia Juni 2025, ni chaneli 14 pekee duniani zimefanikiwa kufikia namba hizo.
Utakumbuka Diamond alitoka kimuziki na wimbo wake, Kamwambie (2009) uliobeba jina la albamu yake ya kwanza, na kufanya vizuri kwa wimbo huo kulimsaidia kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2010.
Jina lake lilianza kuvuma Afrika baada ya kuachia kolabo na Davido kutokea Nigeria, My Number Remix (2013) ambayo iliwania tuzo za MTV MAMAs 2014 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana huku Diamond akiwania Msanii Bora wa Kiume.
Kuanzia hapo Diamond alianza kutanua himaya yake kimataifa, na moja ya njia alizotumia ni kuwekeza katika dijitali hasa upande wa YouTube, mtandao ambao mashabiki wengi Afrika Mashariki wanautumia zaidi kusikiliza muziki.
Na kweli ilimlipa hadi kuja kuweka rekodi kama mwanamuziki anayetazamwa zaidi (most viewed) YouTube ukanda wa kusini mwa Sahara ingawa alikuja kushushwa hadi nafasi ya pili ambapo kazi zake zimeshatazamwa zaidi ya mara bilioni 3.
Ikumbukwe Agosti 2023, Burna Boy kutokea Nigeria alikwea hadi nafasi ya kwanza kama mwanamuziki aliyetazamwa zaidi YouTube ukanda wa kusini mwa Sahara akimpiku Diamond, mshindi wa MTV EMAs mara tatu.
Hiyo ni baada ya mshindi huyo wa Grammy 2021, kutazamwa mara bilioni 2.241 YouTube na kumpiku Diamond aliyekuwa na bilioni 2.240, ila licha ya kupoteza rekodi hiyo, Diamond ameendelea kusalia kuwa kinara ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hadi sasa Burna Boy bado anaongoza akiwa ametazamwa mara bilioni 3.3, Diamond bilioni 3.0, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Wizkid mwenye bilioni 2.3, kisha Rema bilioni 2.1, Davido bilioni 1.9, Ckay bilioni 1.6 na Mr. Flavour bilioni 1.4.
Hata hivyo, bado Diamond, Mkurugenzi Mtendaji wa WCB Wasafi anaendelea kuongoza kwa wafuatiliaji (subscribers) YouTube, huku Burna Boy aliyejiunga na mtandao huo Januari 13, 2018 akiwa na milioni 5.4.
Orodha kamili ya wanaoongoza kwa wafutiliaji (subscribers) wengi YouTube upande wa Sahara ni kama ifuatavyo, Diamond - milioni 10, Rayvanny - milioni 5.7, Burna Boy - milioni 5.4, Harmonize - milioni 5.1 na Fally Ipupa - milioni 5.0.
Wengine ni Rema - milioni 4.9, Tyla - milioni 4.8, Davido - milioni 4.5, Ckay - milioni 4.2, na Zuchu - milioni 3.9, ambaye kwa namba hizo anaongoza Afrika Mashariki kwa upande wa mwanamuziki wa kike.
Ukitazama orodha hiyo, wasanii wote wa Bongofleva walioingia ni kutokea WCB Wasafi ambapo Diamond amewatoa kupitia lebo hiyo, hivyo tunaweza kusema amewarithisha namba zake kwa sehemu kubwa.
Hivyo Diamond kupokea tuzo kutoka YouTube sio kwa bahati mbaya, bali ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wake na amekipigania kwa miaka mingi huku akifungua fursa kwa wengine chini ya WCB Wasafi.
Diamond anapata heshima hiyo kutokana na nyimbo zake kufanya vizuri, mathalani ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki mwenye video nyingi zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube.
Anazo tano zenye namba hizo ambazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Nana (2015) na Jeje (2020) ambao ni wimbo wake wa kwanza solo kufanya hivyo.
Na wote wanaomfuatia Diamond wana video moja moja, video ya Harmonize iliyofanya hivyo ni Kwangwaru (2018), Zuchu ni Sukari (2021), Jux ni Enjoy (2023) na Rayvanny ni Number One (2020).
Akiwa na miaka zaidi ya 15 katika muziki, Diamond ameshinda tuzo 22 za TMA kati ya 2010 hadi 2024, huku akishirikiana na wasanii wengine wa kimataifa kama P-Square, Ne-Yo, Koffi Olomide, Tiwa Savage, Rick Ross, Fally Ipupa, Alicia Keys, Jason Derulo n.k.
Rekodi yake nyingine kubwa Afrika ni kushinda tuzo tatu za MTV EMAs sawa na Tyla wa Afrika Kusini, hawa ndio wanaongoza Afrika ingawa Tyla alishinda zote kwa msimu mmoja huku Diamond akishinda kwa misimu miwili tofauti.
Ikumbukwe Tyla ni mwafika wa kwanza kushinda kipengele cha Best R&B ndani ya MTV EMAs, huku akiwa mwanamke wa pili duniani asiyetokea Marekani kufanya hivyo baada ya Rihanna.