Harry Kane, Kate penzi la kidato kimoja!

Muktasari:
- Kate amekuwa upande wa Kane katika kila hatua ya safari yake ya soka, akimuunga mkono kwa kila hali hadi alipovunja rekodi na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya England na ya klabu ya Tottenham Hotspur.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England na Bayern Munich, Harry Kane ana historia ya mapenzi isiyo ya kawaida ukilinganisha na wanasoka wengi wa daraja lake, na historia hiyo inakamilishwa na Kate Goodland ambaye wamekuwa pamoja tangu wakiwa shuleni.
Kate amekuwa upande wa Kane katika kila hatua ya safari yake ya soka, akimuunga mkono kwa kila hali hadi alipovunja rekodi na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya England na ya klabu ya Tottenham Hotspur.
Walikutana kwa mara ya kwanza wakiwa na umri wa miaka minne wakisoma shule ya msingi ya Larkswood huko Chingford, mashariki mwa London, na baadaye walijiunga na shule ya Chingford Foundation na ndipo uhusiano wao wa kimapenzi ulipoanza.

Tangu wakiwa wadogo walikuwa na ukaribu na watu mashuhuri, mathalani waliwahi kupigwa picha pamoja na David Beckham mwaka 2005 wakiwa na umri wa miaka 11 na 12 kwenye uzinduzi wa akademia ya mpira wa miguu yake Beckham.
Katika mahojiano na Jarida la Esquire hapo Februari 2015, Kane alisema yupo katika uhusiano na Katie ambaye amemfahamu tangu utotoni, na walikuja kufunga ndoa miaka 10 baada ya uhusiano wao kuanza rasmi.
“Tulikwenda shuleni pamoja, kwa hiyo ameona maendeleo yangu yote ya soka. Bila shaka, anashangazwa na yote haya,” anasema Kane, mfungaji bora wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) mara mbili.

Mnamo Julai 2017, Kane kupitia mtandao wa X, zamani Twitter alitangza kumchumbia Kate ambaye ni mhitimu wa masomo ya sayansi ya michezo na ni mkufunzi wa mazoezi ya mwili huku akiwa na wafuasi zaidi ya 300,000 Instagram.
Wawili hao walichumbiana wakiwa mapumzikoni katika visiwa vya Bahamas ambako walifuatana na binti yao Ivy, na hapo ndipo Kane alipomvisha pete Kate ufukweni. Kane aliposti picha kwenye mitandao akiwa amepiga goti na kuandika; “Amesema ndiyo.”
Kufikia Juni 2019, walithibitisha kufunga ndoa ingawa waliamua kutofichua mahali harusi ilikofanyika, picha zilionekana za kuvutia mno – Harry akimkumbatia na kumbusu mkewe huku bahari ikionekana kwa mbali.
“Hatimaye nimeoa rafiki yangu wa dhati! Nakupenda.” aliandika Kane ambaye uhusiano wake na Kate ulianza rasmi wakiwa na umri wa miaka 16 katika shule ya Chingford.

Ikumbukwe wakati wanafunga ndoa, tayari walikuwa na mtoto mmoja, binti yao Ivy aliyezaliwa Januari 2017, kisha akafuatia binti yao wa pili, Vivienne aliyezaliwa Agosti 2018.
Mtoto wao wa kwanza wa kiume, Louis alizaliwa Desemba 2020, na mtoto wao wa pili wa kiume, Henry alizaliwa Agosti 2023 ikiwa ni muda mfupi baada ya Kane kusajiliwa na Bayern Munich ya Ujerumani kwa dau la Pauni104 milioni.
Kate alionekana akiwa na ujauzito wa mtoto wao huyo wa mwisho kwenye uwanja wa ndege wa Luton wakati wakisafiri kwenda Munich kukamilisha mkataba wa Kane ambaye baada ya kusaini alizungumza.
“Familia inatarajiwa kurudi Uingereza, kisha tutajipanga jinsi ya kulishughulikia hili suala la kujifungua. Bado hatujafanya uamuzi, nitaongea na mke wangu kuhusu hilo. Kuna mambo mengi ya kupanga. Watoto, shule, mahali pa kuishi – tunapaswa kuyasimamia yote hayo,” anasema.
Chanzo cha karibu na familia hiyo kiliuambia mtandao wa The Mail on Sunday kuwa Kane na mkewe wanamiliki ndege binafsi, jambo lilliorahisisha safari kutoka Ujerumani kurudi Uingereza.
“Kulikuwa na matukio mawili makubwa yaliyotokea kwa wakati mmoja – Kate alikuwa karibu kujifungua, huku Kane akifanya uhamisho wake mkubwa na wa fedha nyingi kwenda Bayern.”
“Hata hivyo, mambo yanaweza kubadilika, lakini kwa sasa, kutokana na ujauzito wake na kuna watoto wanaosoma shule London, Kate ameamua kubaki hapa nchini Uingereza,” chanzo hicho kilieleza wakati huo.
Utakumbuka uamuzi wa Kate kubaki nyumbani kwa muda, unaelekea kufanana na ule wa Victoria Beckham ambaye mwaka 2003 alimuacha mumewe David aende Hispania kuichezea Real Madrid akitokea Manchester United.
Kane alipohamia rasmi Ujerumani kujiunga na Bayern Munich, mwanzo waliishi hotelini na baadaye familia nzima ilihamia kwenye nyumba mpya huko Bavaria mwishoni mwa 2023, na tayari Kate alikuwa ameshajifungua.

“Nataka kuelewa tamaduni zao kadiri iwezekanavyo. Niko tayari kabisa kujifunza lugha yao,” anasema Kate wakati akieleza jinsi anatamani kuzoea maisha ya Ujerumani.
Akizungumza na gazeti la Evening Standard hapo Julai, 2024, Kane alisema kama bado angekuwa hana mpenzi ingekuwa vigumu kwake kumjua mtu sahihi au yule anayefuata fedha na umaarufu wake.
“Kwa hiyo ni bahati kuwa nina mchumba wa utotoni. Yeye kila wakati alitaka kufanya mambo yake. Alienda chuo kikuu na alijitahidi sana. Nina familia nzuri, wananifanya nisibweteke na wamefanya kazi kwa bidii ili kunifikisha hapa nilipo,” anasema Kane.
Ikumbukwe Kane mwenye umri wa miaka 31 kwa sasa, msimu uliomalizika alishinda taji lake la kwanza baada ya Bayern kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bundesliga, huku klabu yake zamani ya Tottenham aliyodumu nayo kwa miaka 14, akishida taji (Europa) baada ya miaka 17 ya ukame wa mataji.