Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wengi wamefanya ila Rayvanny kawazidi wote!

MWIMBAJI wa Bongofleva kutokea Next Level Music (NLM), Rayvanny kwa sasa ndiye msanii aliyefanya video nyingi zaidi na mpenzi wake, Fahyma maarufu kama Fahyvanny ambaye pia mzazi mwenziye wakijaliwa mtoto mmoja, Jaydan aliyezaliwa Aprili 2017.

Fahyma ni Mwanamitindo akiwa ameshinda tuzo mbalimbali za kimataifa kama Scream Awards (Nigeria), Starqt Awards (Afrika Kusini) na Swahili Fashion Week Awards zinazotolewa hapa nchini.

Huyu ndiye mrembo aliyetokea mara nyingi zaidi kwenye video za Rayvanny ikiwa ni mara nne, pia rekodi yake ya kipekee ni kwamba katika video ya wimbo, Kwetu (2016) iliyomtoa Rayvanny kimuiki, Fahyma alikuwepo na ndicho kipindi mapenzi yao yalianza.

Licha ya panda shuka, kuachana na kurudiana, tunaweza kusema Fahyma ni mwanamke nyuma ya mafanikio ya Rayvanny kwa kipindi cha miaka zaidi ya saba walichofanya kazi pamoja katika tasnia.
Katika video ya wimbo mpya wa Rayvanny, Forever iliyotoka hivi karibuni, Fahyma ametokea na kufanya vizuri kama kawaida yake, kwa ujumla video za Rayavnny alizonogeshwa na sura ya Fahyma ni; Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017) na Forever (2023).

Utakumbuka kipindi Rayvanny yupo na Paula alimtumia pia katika video ya wimbo wake, Wanaweweseka (2021) kutoka kwenye Extended Playlist (EP) yake, Flowers II, kwa hiyo hadi sasa Rayvanny amefanya video tano na warembo aliokuwa nao katika uhusiano.
Kwa muktadha huo, Rayvanny anazidi kuwaacha nyuma Mastaa wenzake Bongo kama Diamond Platnumz, Harmonize na Jux ambao nao wamewahi kufanya video zaidi ya mbili na wapenzi wao kama ifuatavyo;


1. Diamond (4) - Wema, Hamisa & Zari
Staa huyu wa WCB Wasafi karibia warembo wote ambao wamewahi kuwa nao katika uhusiano ameshafanya nao video za nyimbo zake, alianza na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ambaye alitokea kwenye video ya wimbo wake, Moyo Wangu (2011).
Hamisa Mobetto ambaye uhusiano wake na Diamond Platnumz ulikuwa wa siri sana hadi walipojaliwa mtoto, Dylan (2017), aliinogesha vizuri video ya ngoma ya Chibu, Salome (2016) akimshirikisha Rayvanny.
Kwa upande wake Zari The Bosslady kama alivyojaliwa watoto wawili na Diamond, Tiffah (2015) Nillan (2016), yeye ametokea video mbili za nyimbo za Diamond, Utanipenda (2015) na Iyena (2018) na ndiye mpenzi pekee wa Diamond aliyefanya naye video nyingi.


2. Harmonize (4) - Wolper, Sarah & Kajala
Kipindi penzi la Harmonize na Jacqueline Wolper lipo katika kilele cha mafanikio yake, walisafiri hadi Afrika Kusini kufanya video ya wimbo, Niambie (2017), huku Wolper akitokea na ndiye mpenzi wa kwanza wa Konde Boy kufanya hivyo.
Aliyekuwa mke wa Harmonize, Sarah kutokea Italia waliyedumu katika ndoa takribani mwaka mmoja (2019 - 2020), ametokea kwenye video za nyimbo mbili za Harmonize, My Boo Remix (2019) na Niteke (2019) kutoka kwenye EP yake, Afro Bongo.
Naye Kajala Masanja ambaye alivishwa hadi pete ya uchumba na Harmonize, ametokea kwenye video moja, Nitaubeba (2022) na muda mfupi baada ya video hiyo kuachiwa wakaachana. Briana kutokea Australia ndiye mrembo pekee aliyekuwa na uhusiano na Harmonize ambaye hakutokea kwenye video yeyote ya Konde Boy.


3. Jux (3) - Vanessa, Nayika & Huddah
Staa huyu wa RnB Bongo naye kila mrembo anayekuwa naye ni fursa kwake, kipindi yupo na Vanessa Mdee alimtumia katika video ya wimbo wake, Sisikii (2015), huku wakitoa nyimbo mbili za ushirikiano pamoja na video zake, Juu (2016) na Sumaku (2019).
Baada ya kuachana na Vee, Jux alizama kwenye penzi jipya na Nayika, mrembo kutokea Bangkok nchini Thailand ambaye alitokea kwenye video ya wimbo wake, Unaniweza (2020) na muda mfupi tu baada ya hapo wakaachana kwa madai ya umbali kati yao.
Na mwisho Jux akamvuta katika himaya yake, Huddah Monroe kutokea Kenya ambaye ameipamba vilivyo video ya ngoma yake, Simuachi (2022). Hata hivyo, Huddah alidai hajawahi kuwa na uhusiano na Jux bali ni kazi tu, huku Jux akisema Huddah ni mshirika wake kibiashara na ndio sababu ya ukaribu wao.
Ukiangalia kutoka kwa Diamond, Harmonize hadi Jux, utabaini wote tayari wameachana na wapenzi wao ambao walifanya nao video, ila Rayvanny licha ya kuwazidi idadi ya video alizofanya na wapenzi wake, bado yupo na mpenzi wake mmoja, Fahyma aliyefanya naye video nne kitu kinachomtofautisha na hawa wengine.

Hata hivyo, ikumbukwe Fahyma hajawahi kutokea kwenye video ya msanii mwingine tofauti na Rayvanny, ila kina Wema Sepetu, Jacqueline Wolper, Kajala Masanja, Ebitoke, Vanessa Mdee na Hamisa Mobetto wamewahi kutokea kwenye video nyingine tofauti na hizi za waliowahi kuwa wapenzi wao zilizotajwa kwenye makala haya.