Amina Vikoba ndiye ‘Siwa wa Mzee Kikala’ kwenye Kombolela

Muktasari:
- Huyu ni Amina Ahmadi ‘Amina vikoba’. Na kama hujui, ni dada wa msanii wa singeli, Dulla Makabila na Mwanaspoti lilikutana naye Mtoni Kwa Aziz Ally, Temeke wanakoandaa tamthilia hiyo ya Kombolela na kupiga stori na Dakika 5 Na...
NI mmoja wa wasanii mahiri wa maigizo kwa sasa katika tasnia ya Bongo Movie. Ameigiza tamthilia mbalimbali na kujikusanyia mashabiki wengi huku ile ya Kombolela inayorushwa na Chaneli ya Sinema Zetu ya Azam Tv na amewafanya wengi kuzidi kuifuatilia kutokana na kipaji chake.
Huyu ni Amina Ahmadi ‘Amina vikoba’. Na kama hujui, ni dada wa msanii wa singeli, Dulla Makabila na Mwanaspoti lilikutana naye Mtoni Kwa Aziz Ally, Temeke wanakoandaa tamthilia hiyo ya Kombolela na kupiga stori na Dakika 5 Na... akifunguka kuhusu maisha yake ya sanaa na mambo mengine.
Amina Vikoba ni nani?
“Wengi wanadhani jina la Amina Vikoba limetokana na kuchezesha mchezo wa vikoba, ila siyo. Jina la Vikoba limetokana na filamu yangu ya kwanza niliyoitengeneza mwenyewe kwa hela yangu na ipo YouTube. Tangu hapo ndiyo jina vikoba likajulikana.”

Tamthilia iliyomtambulisha
“Nimecheza tamthilia nyingi ila ambayo imenitambulisha hadi leo wengi wananijua ni ‘Kombolela’ kuanzia msimu wa kwanza (season 1) na sasa inaendelea ya pili inayoandaliwa na Abdull Usanga.”
Uhalisia wa Kombolela na maisha yake ya kawaida
“Tofauti kabisa. Kwenye Kombolela nimecheza kama mwanamke niliyezalishwa nyumbani, mdada ambaye sina adabu. Hata hivyo, siyo kama yule ‘Siwa’ (jina analotumia) wa Kombolela (anacheka). Mimi ni mchangamfu na nina Adabu na heshima kwa kila mtu. Ile ni ‘script’ (mwongozo) tu na ilivyoandikwa ndivyo imenitaka kucheza hivyo. Wee, yule Siwa wa Kombolela ni habari nyingine hapana kabisa (anacheka).
Changamoto katika kazi
“Eee.. ni kubwa sana. Kwanza watu kudhani kile nachofanya kwenye tamthilia ya Kombolela ndivyo ulivyo. Yaani hadi watu huwa wananiogopa, wanajua niko vile na mdomo, kuchambua watu, daah! Ila niwaambie tu, Kombolela ndiyo kwanza imeanza na bado sana huko mbele kuna mazuri zaidi na zaidi, ikimuhusu Siwa wa mzee Kikala.”

Huwa unaongezea maneno ya kuongea mbali na ‘script’ (mwongozo)?
“Ndiyo, huwa naongeza ili kunogesha. Mwongozaji anasema kama utaongezea neno basi liendane na ‘script’ aliyoandika mwandishi, ili lisitoe maana ya tamthilia.”
Ni kweli ulifanya sherehe ya kupewa talaka baada ya kuachika?
“Hapana jamani, ile video ‘clip’ iliyokuwa inasambaa kwenye mitandao ilikuwa ni Dokta Kumbuka aliamua kuchagiza tukiwa tutafanya sherehe. Pale tulikuwa tunatoka kushuti tamthilia ya ‘Jua Kali’ akaamua kuongea vile kuwa nitafanya sherehe lakini hapana ningefanya ingeonekana haya mambo hayajifichi bana.”
Watu wanasema gari aina ya Range Rover Dulla amelikodi hajanunua ni kweli?
“Yataongeleka mengi tu na sio kila mtu atapenda maendeleo yako, gari amelinunua na kikubwa anatamba nalo, nampongeza kwa hilo sana amepiga hatua.”

Kuna watu wanakuita wifi Yuda kisa uhusiano wa Dulla
“Sisi mawifi huwa tunapata lawama sana kupitia kaka zetu. Siyo kwamba tunapenda kuhamahama kwa mawifi zetu, sasa utakuta kaka yako ameenda kwa huyu mara katoka kaenda kwa huyu, nasi tunaamua kuhama naye, sasa ulibakia sehemu si utaonekana mnafiki,” anasema Amina na kuongeza katika familia yao wako sita huku yeye ni wa pili na Dulla ni wa pili kutoka mwisho kuzaliwa.
Kuna ishu ya Zaylissa baada ya kuachika kwa Manara alikuja dukani kwako
“Hapana ile video ‘clip’ ni ya zamani kipindi Zaylissa aliolewa na Dulla alikuwa anakuja dukani, sasa watu waliposti baada ya kuachika kwa Manara na wanasema ni rafiki yangu, hapana sio kihivyo. Ila kama akirudiana na mdogo wangu, mie sawa tu si ndogo wangu Dulla atakuwa ameamua. Katika ma ex wa Dulla ninaowakubali ni yeye. Ana adabu na upendo.”

NDOA YA NGAPI HII?
“Nina ndoa tatu, ya kwanza nina mtoto mmoja, ya pili niliolewa na mkristo nikabadili dini nikazaa watoto wanne na ya tatu hii na nimerudi katika dini yangu ya Kiislamu.”
umeolewa mke wa pili?
“Hilo sijalijua. Mimi ninachojua niko peke yangu, kama lipo basi labda nyuma yangu.”
Nini matarajio yako kwenye sanaa yako?
“Mimi matarajio yangu ni kuwa na kazi zangu binafsi za kuigiza, nimeshaanza kuandaa kazi zangu na hivi karibuni nitaziweka YouTube, hivyo mashabiki zangu nawaomba sapoti yao pale nitakapoanza kutupia kazi zangu.”

Nje ya uigizaji
“Mimi ni mfanyabiashara na nina duka langu la vitu mchanganyiko, nauza nguo, pochi, vitambaa, vijora, viatu linaitwa Siwa mchanganyiko lipo Magomeni Popobawa.”
Hatasahau hiki
“Kufiwa na baba. Huwa namkumbuka sana kuna muda natenga muda nalia na kutamani kama angekuwa hai angeona watoto wake sisi tulivyokuwa sasa wengine waigizaji wengine wana magari ya kifahari kama ‘Range Rover’ na angeona wajukuu zake huwa nafikiria vitu vingi sana nabaki kumwombea dua tu. Ssasa tumebakia na mama.”
Leo ondoa utata Dulla ni timu gani Simba au Yanga?
“Yule haeleweki anaweza akiamka akawa Simba, jioni akawa Yanga, kwenye suala la mpira hayuko kihivyo sana yeye kazi yake kutunga nyimbo aingie studio tu.”
“Kipindi marehemu baba alikuwa anapenda sana Yanga na watoto wote tukawa Yanga hadi Dulla, ila sasa hivi amekuwa haeleweki timu gani Dulla.”