Wataweza? Wanavyopambana kurithi nafasi ya Steven Kanumba

KWENYE sanaa ya muziki kuna vichwa viwili vinavyozungumzwa zaidi kutokana na aina ya muziki wanaofanya huku wakifanikiwa kujinyakulia mashabiki lukuki.
Mastaa hao ni Alikiba na Diamond na ushindani wao unafananishwa na mastaa mahiri wa soka, Christian Ronaldo na Lionel Messi
Wakati Messi akiitwa ‘mpira kipaji’, Ronaldo anaitwa ‘soka mazoezi’, huku kwenye Bongo Fleva yetu, hawa wana Kiba na Mondi sifa zao kubwa ni kuimba ‘Alikiba’ na upambanaji na ubirudishaji ‘Diamond’.
Ushindani pia ulikuwepo kwa wasanii wa maigizo ‘Filamu’, na wasanii Ray Kigosi na Steven Kanumba walikuwa na upinzani mkali na kusababisha soko la filamu kukua kwa kasi.
Hata hivyo, baada ya kifo cha Kanumba, upinzani nao ulikufa, Ray akabaki mwenyewe kabla ya kuibuka kwa mastaa wengine wanaofanya vizuri na kumpoteza mkongwe huyo.
Hawa hapa mastaa sita wa filamu za Bongo walioanzisha vita mpya ya nani mkali baada ya upinzani wa Ray na Kanumba.
GABO
Kwa sasa anafanya vizuri kwenye tamthilia ya Jua Kali akifiti kwenye kila eneo analopangwa kuigiza huku kwenye tasnia hiyo anatajwa ni mmoja wa waigizaji bora wa kiume kutokana na kazi zake zinazofanya vyema sokoni.
Filamu alizoshiriki ni Majanga, Safari, Fikra zangu ya Jerusalem Film ya Jb hizi zote zikiwa za watayarishaji wengine tofauti na filamu yake ya Kona ambayo aliitayarisha mwenyewe, na sasa amekuja na filamu yake ya Safari ya Gwalu inayoelimisha jamii ikiwa imeitayarisha mwenyewe.

ISARITO
Alianza kwa kucheza filamu za mapigano kabla kuingia kwenye tamthilia ya Jua kali na kuwa gumzo alipoigiza kipengele cha mapenzi huku yeye akionekana kusalitiwa na wanawake zake kila mara hadi kuambulia vichapo.
Isarito maarufu kwa jina la Luka wa Jua kali ni mmoja wa mastaa wanaofanya vizuri kwenye tasnia hiyo kwa upande wa wanaume kutokana na aina ya uigizaji wake.

GARABH
Ni maarufu kutokana na kazi yake ya ‘U-MC’ kwenye shughuli mbalimbali hasa harusi kunakompa ulaji zaidi.
Hata hivyo, kipaji nacho kinamwingizia pesa na anatamba kwenye tamthilia ya Jua Kali na Lamata ndiye aliyempa nafasi ya kuigiza na kufanya vizuri hadi kuibua hisia za mashabiki wengi wakimsifu anaweza.

QUICK ROCKA
Ni mkali wa muziki lakini ameamua kuibukia pia kwenye uigizaji akianzia kwenye tamthilia ya Kapuni iliyokuwa chini ya Lamata na kuamua kumnyoa rasta kutokana na kubaini kipaji kwake.
Staa huyo hajataka kumwangusha Lamata kwani alifanya vizuri kwenye Kapuni na sasa anaendelea kufanya hivyo kwenye tamthilia ya Jua kali inayoongozwa pia na Lamata.

RAMMY GALIS
Anafanya vizuri kwenye tamthilia ya Huba lakini kabla alikuwa bora akianza kuigiza na marehemu Steven Kanumba kwenye baadhi ya filamu zilizotamba sokoni.
Awali alifananishwa na Rammy na mwenyewe aliwahi kukiri ndiye aliyemshawishi kuingia kwenye sanaa hiyo na kuachana na kazi yake aliyokuwa ameajiriwa katika bandari kavu.
Alianza kuonekana kwenye fila mu ya ‘Love in Power’ ya Kanumba ingawa hakuwa kati ya waigizaji wakuu.
Filamu yake ya kwanza ilitoka Agosti mwaka 2012, baada ya kifo cha Kanumba kabla ya kuanza kujulikana zaidi hasa alipoanza kufanya kazi na Ray Kigosi.

BEN KINYAIYA
Ni msanii wa Bongo Flava na mtangazaji ambaye ameamua kuingia kwenye maigizo baada ya kipaji chake kugundulika na huko amekuwa akifanya vizuri kwenye tamthilia ya Huba ikiwa na mastaa kama JB.
Kabla ya kuingia kwenye filamu staa huyo ametamba na nyimbo kama ‘Dalila’, ‘Tumekuja Kuwashika’, zilizopo kwenye albamu yake ya kwanza na anayodai kuwa ni ya mwisho. iliyokuwa na
nyimbo 10.
