Wasanii wa hizi nyimbo, mnadaiwa video

Muktasari:

  • Sio  huo tu, unaukumbuka wimbo wa Mandojo na Domo Kaya 'Nikupe nini', ni wimbo mwingine wenye miaka zaidi ya 20 lakini huo pia kichupa chake kilitoka mwaka jana.

'CHUPA nyingine' una ukumbuka? Ni mmoja ya nyimbo za msanii wa Hip Hop, Mchizi Moxi uliokaa takriban miaka 20 ndio ukaja ukafanyiwa video.

Sio  huo tu, unaukumbuka wimbo wa Mandojo na Domo Kaya 'Nikupe nini', ni wimbo mwingine wenye miaka zaidi ya 20 lakini huo pia kichupa chake kilitoka mwaka jana.

Kuna huu 'Hili Gemu' wa Juma Nature, video yake ilitoka miaka mingi baadae na ikafanya vizuri. Pia japo wimbo wa 'Mzee wa Busara' ulitesa miaka hiyo, ulipikwa upya akishirikiana na Inspector Haroun Babu na kuachia video ambayo inasumbua mitandaoni.

Hizi ni baadhi ya nyimbo za kitambo ambazo kwa ubora wake kwenye mashairi, mashabiki walikuwa na hamu ya kuona zikifanyiwa video. Sasa zinabamba kwenye media ingawa zimechelewa, kikubwa zimeachiwa.

Hata hivyo, zipo nyimbo ambazo hadi leo hii, wasanii wanaotajwa ni wakubwa na wamefika mbali lakini wameshindwa kuzitendea haki kwa kutotoa video zao na mashabiki ni kama wanawadai na hata zikitoka sasa hivi zitagusa hisia zao.

Sababu kubwa kwa kipindi hicho inatajwa ni teknolojia, aina ya mashairi na utafutaji wa maeneo kuendana na wimbo.

Hata hivyo, wapo waliofanya kibishi na kusuuza roho za mashabiki ambao wakisikiliza nyimbo hizo wanatamani kuona matukio ya kwenye mashairi yangekuwepo kwenye video.

Sababu nyingine ni gharama za kufanya video na hii ilichangia nyimbo kuishia redioni na wengi wameona hakuna sababu ya kuzirudia kwa kutoa video na wanatoa kazi mpya.

Hawa hapa wasanii ambao nyimbo zao baadhi ni kama mashabiki wanatamani wangeona video zao kutokana na utunzi wa maishairi na ulivyogusa hisia za wengi.


JUMA NATURE-

Mmoja wa wasanii wa Hip Hop ambaye alitesa na vibao vyake vingi lakini kati ya hivyo zipo ambazo mashabiki wakizisikiliza bado wanajiuliza kwa nini Nature hakutoa video.

Nyimbo kama Inaniuma sana, Mtoto Iddi, Sonia, Kighettoghetto na Jinsi Kijana. Mashairi ya nyimbo hizi ni wazi yaliwafikirisha watu na kutengeneza picha kichwani ya kile kinachoimbwa.

Huyo Sonia, vipi maisha ya kigeto na kijana aliyesumbua watu Idi. Zaidi alivyoumizwa na mapenzi wimbo wa Inaniuma, tengeneza picha kichwani video yake Nature anavyolalamika. Ni wazi video zao zingebamba sana.

PROFESA JAY

Kaka mkubwa na Mbunge wa zamani wa Mikumi. 'Piga makofi'. Moja ya nyimbo zilizoamsha watu kwenye viti klabu. Nani angeusikia asisimame.

'Bongo Dar es Salaam' wenye simulizi zinazoonekana wazi ingawa tulinyimwa video yake. Achana na 'Chemsha Bongo' ambao tuliishia kuusikiliza tu bila ya kuona kichupa chake.

Zipo pia 'Niamini' aliyeurudia pia na Lady Jaydee 'Nimeamini'. 'Ndiyo Mzee', 'Kikao cha Dharura', simulizi za nyimbo hizi zinaleta picha ya matukio ambayo hata hivyo mengi ni ya kufikirika lakini vipi kama kungekuwa na video zake. Zingebamba.

DAZ NUNDAZ -

Kundi lililotesa sana miaka 20 iliyopita na katika nyimbo zao ni chache sana zina video na nyingine bado tuna tamani tuone video zake.

'Barua' na 'Kamanda', kweli hadi leo hazina video? Nani asingetamani kuuona mkasa wa bosi kwenye video?

Ingependeza sana ila Ferouz hakututendea haki. Tuna haki ya kuwadai. Hata hivyo, miaka imeenda na kundi hili halipo pamoja tena ila kama wangetoa video, hizo nyimbo zingetesa sana.

SOLO THANG -

Alitamba na video ya wimbo 'Homa ya Dunia' hata hivyo nyimbo zake nyingi ambazo ziliteka hisia hazina video; 'Simu yangu', 'Mambo ya Pwani', 'Kilio Changu', 'Vina Utata'.

Kama ilivyo kwa ufundi wake wa mashairi, ingependeza kuona video za nyimbo hizi ambazo zina simulizi za kuvutia kuona matukio yake.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

JAY MO -

Pata picha video ya 'Mvua na Jua', vipi ya 'Maisha ya Bording' na anavyomsaka demu kwenye 'Kama unataka demu' na 'Bishoo'.

Mo ni kichwa hasa kwenye utunzi ila kwenye video kwa hizi nyimbo tunamdai. Wengi walitamani kuona matukio yalioimbwa kwenye mashairi ingawa muda umepita tangu ziachiwe.

Mwana FA - Aliimba na Jay Mo wimbo wa 'Ingekuwa vipi', kuna 'Mabinti', simulizi zake zilitamba na wengi walitamani kuona katika video kile kilichoimbwa. Hata hivyo miaka imekimbia kweli na hilo halijafanyika.

Mandojo na Domo Kaya - wakali wa voko Bongo. Inauma sana nyimbo za 'Wanoknok', 'Niaje', hazina video. Mashabiki wengi walisubiri kuona video zao lakini haikuwa hivyo ila kihisia wanaona wangetendewa haki kwa uwepo wao.

MCHIZI MOX-

'Demu Wangu' ni wimbo alioimba akijibizana na marehemu Albert Mangwea 'Ngweir'. Kwenye mashairi ya wimbo huo wanamgombea demu na ni moja ya simulizi tamu ambazo wengi walitamani kuziona kwenye video.

MANGWAIR-

'Gheto Langu' lilivyosimuliwa lilitamanisha sana kuona ukweli ya yaliyopo. Hata hivyo, Marehemu Mangwair hakutoa video yake na imebaki historia kwa mkali huyu wa mistari.

Pia wimbo wa 'Sikiliza' aliomshirikisha Mwana FA ni moja ya nyimbo zenye simulizi ambazo zilitakiwa kuwa kwenye video hasa kwa namna alivyowaongelea wanawake. Aendelee kupumzika kwa Amani peponi.

DULLY SYKES-

'Salome', 'Nyambizi' 'Julietha' na 'Leah'. Wengi waliishia kusikia zikitetemesha spika za redio lakini video zake hazikuwepo. Simulizi ya wimbo kama Salome na Nyambizi, zilivutia na hapa Dully alitunyima uhondo wa video. Kama vipi irudiwe.

Kwa nyimbo za miaka ya karibuni. Hapa ndipo mashabiki wengi wanaumia kuona hawajatendewa haki kwa nyimbo nyingi kutokufanyiwa video.

Kwa ukuaji wa teknolojia, hakuna ubishi hawa kuwadai video ni haki na wenyewe wanajua hawakutenda haki ila ilibidi iwe hivyo.

Zaidi kinachowasukuma ni vita ya tuzo za video kali na nyimbo kali ya mwaka zimewafanya mastaa wengi kuwekeza kazi zao kwa kutoa video kali wakimwaga fedha nyingi.

Hata hivyo, kuna nyimbo kali kipindi hiki pamoja na mashairi matamu lakini zimekosa video.

DIAMOND PLATNUMZ -

Mkali wa video kali na zinazofanya poa YouTube licha ya kutokuwa na muda mrefu zaidi ndiye anaongoza kwa kuwa na nyimbo nyingi.

'Lala Salama' ina miaka tisa tangu itoke na haijapishana sana na 'Ukimwona', moja ya tungo matata sana za Diamond na zilimpaisha kisanii zikitoa ujumbe mtamu wa mapenzi na 'Ukimwona mbali na kusikilizwa na watu zaidi ya Milioni 6 lakini hauna video.

'Nawaza', 'Loyal', 'Gimme', 'Yataniua' na Far Away aliomshirikisha Vanessa Mdee ni baadhi ya nyimbo ambazo video zake zilisubiriwa kwa hamu bila kutoka


HARMONIZE -

'Wapo', 'Utanikumbuka', My Way' na 'Mtaje' zimefanya vyema kwenye vituo mbalimbali vya redio na Youtube kwa sauti pekee bila video.

Ni wazi Harmonize hakushindwa kutoa video za nyimbo hizi labda tu ratiba zilibana kwani kwa kuzisikiliza tu zinahitaji vichupa kutokana na simulizi zake.

ALIKIBA -

'Mapenzi Yanarus Dunia' nani asiyeukumbuka huu wimbo ambao ni moja ya hit zake kali na zilizomtoa kimuziki kipindi anajitafuta kwenye gemu.

Kuna huu pia 'My Everything' wa mwaka 2012 na watu wanatamani kuona video yake kutokana na simulizi yake tamu

Zuchu - Hakuna asiyejua makali yake hasa kwenye vichupa na ana video nyingi kali lakini ya wimbo 'Hasara' imeacha maswali ya video yake iko wapi? Zuchu sijui analijua hilo.

Maua Sama - Shukuran imewapita wengi hivi hivi kwa kukosa kichupa. Kweli hapa Maua hajatenda haki kutokana na stori ya wimbo wake, zipo pia nyingine ambazo hazina video lakini ukiusikiliza Shukuran mwenyewe utadai video yake.


Nandy - Wimbo 'Dah' ameufanyia 'remix' na Alikiba na ndio uliotolewa video, lakini ule halisi alioimba mwenyewe hauna video na hilo limeacha maswali kwa mashabiki wake.

Yammi - Huyu dada anakuja juu kwa kasi na ni msanii wa Nandy. Nyimbo zake za 'Kiuno' na 'Tiririka' zinakimbiza sana Youtube kwenye sauti pekee lakini hazina video. Yammi, hapa unadaiwa video uwatendee haki mashabiki zako.

Orodha ni ndefu, lakini hao ni wachache tu ambao nyimbo zao zilipendwa sana lakini zikakosa video. Pia wasanii wa zamani na wa sasa wanatofautiana mambo mengi ikiwamo teknolojia na kwa sasa ni rahisi kutoa video kuliko enzi hizo muziki wa Bongo Flava ukianza kushika kazi.