Wasikie mastaa Bongo amapiano ikizidi kupeta

Muktasari:
- Kwa hiyo kupitia amapiano wasanii Bongo kazi zao zinapata mapokezi makubwa, Agosti wimbo wa Diamond, Komasava (2024) wenye mahadhi ya amapiano uliweka rekodi kwa kuwa wa kwanza Afrika Mashariki kuingia chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs.
KADIRI miaka inavyokwenda amapiano inazidi kupendwa Bongo, mathalani wimbo wa Jux, Enjoy (2023) akimshirikisha Diamond Platnumz, una rekodi kwa video yake kuwa ya kwanza Bongo kutazamwa zaidi mara milioni 100 YouTube chini ya mwaka mmoja na nusu tu.
Kwa hiyo kupitia amapiano wasanii Bongo kazi zao zinapata mapokezi makubwa, Agosti wimbo wa Diamond, Komasava (2024) wenye mahadhi ya amapiano uliweka rekodi kwa kuwa wa kwanza Afrika Mashariki kuingia chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs.
Hata hivyo, licha ya wasanii wengi wakubwa nchini kutoa nyimbo za amapiano, hakuna hata mmoja aliyepata nafasi katika tuzo za Amapiano Awards 2023 huko Afrika Kusini huku wasanii wa Nigeria kama Asake, Davido na Wizkid waking’aa.
“Wasipotuweka kwenye tuzo zao haimaanishi amapiano zilizofanyika Tanzania sio kali au hazina mchango, hivyo tunatakiwa kupambana kuhakikisha tunaenda katika levo kubwa ya kidunia ambayo watakuwa hawana budi kutukubali,” anasema Damian Soul.
Naye G Nako aliyefanya vizuri na nyimbo za amapiano kama Sugga Daddy (2023) na Komando (2023), amesema kila tuzo zinakuwa na malengo yake, hivyo hayo ni matokeo ya waandaaji kwa kuzingatia walikuwa wanataka kufanikisha nini.
“Unajua tuzo sio kipimo cha kufanya vizuri, tuzo nyingine zinaweza kuwa kimkakati, huwezi kujua kwa sababu hizo tuzo hazifanyiki hapa kwetu, lakini sisi tunachojua kuna kazi ambazo zimefanya vizuri hapa na kwingineko,” anasema G Nako.
Ikumbukwe Juni 2023 waandaji wa tuzo za Grammy Marekani, Recording Academy walianzisha kipengele cha ‘Best African Music Perfomance’ ambacho ni maalamu kwa ajili ya aina mbalimbali za muziki kutokea Afrika ikiwemo Bongofleva na Amapiano.

Na Tyla wa Afrika Kusini akaweka rekodi kama msanii wa kwanza kushinda kipengele hicho 2024 kupitia wimbo wake wa amapiano, Water (2023) akiwabwaga wakali kibao akiwemo Davido ambaye aliwania pia na wimbo wa Amapiano, Unavailable (2023).
Mkongwe wa Bongofleva aliyevikwa taji la Mkali wa Rhymes 2004, Afande Sele anasema muziki wa amapiano ni mzuri hasa upande wa midundo ila kwa hapa Bongo ujumbe wake ndio tatizo kwa baadhi ya wasanii kwa kuimba mambo yasiyofaa katika jamii. “Kwa upande wa ujumbe bado ni tatizo, kuna tungo zimejaa matusi, utoto na masihara mengi lakini kama watakuwa na ubunifu kwa kuchanganya na vionjo kidogo vya nyumbani hata katika nyimbo za kuburudisha nadhani wanaweza kufika mbali,” amesema.
Mwimbaji Foby amesema pia amapiano ni muziki mzuri ila wasanii Bongo waache kudai wanafanya muziki huo kisa mashabiki wanataka au kwa sababu ya kibiashara maana kabla ya ujio wa amapiano wasanii walikuwa wanafanya biashara ya muziki.

“Je, ni wasanii wangapi wa Tanzania waliofanya amapiano wamefanikiwa kupata shoo na tuzo za nje?, hata kuwekwa kwenye vipengele tu?! Ni muziki mzuri ila watu kuusifia na kusema unaleta fedha, nakataa hilo kabisa,” anasema Foby.
Mtayarishaji muziki kutoka Combination Sound, Man Water ambaye ni mshindi wa TMA 2014, anasema licha ya kutotengeneza amapiano hana shida na muziki huo ila wasanii Bongo wanapaswa kujua kuwa wanakuza muziki na tasnia ya wenzao.
“Mara nyingi tunaimba kinachotoka sehemu nyingine na kuamini soko lipo kule ila hatujui kama tunakuza masoko yao ingawa kwetu inatusaidia na inaonekana watu wanapata fedha kwa sababu tunaileta kwa lugha yetu na kueleweka.
“Ila mwisho wa siku tunaonekana sio wabunifu, tumekuwa wa kuanzishiwa lakini kama tunalenga biashara, basi acha watu wafanye Amapiano kwa sababu mwisho wa siku muziki ni biashara, watu wanapata fedha,” anasema Man Water.
Naye rapa wa kundi la Kikosi cha Mizinga, Kalapina anadai muziki wa amapiano sio mzuri maana hauwezi kufikisha ujumbe katika jamii kama ilivyo Hip Hop na mbaya zaidi unaharibu vijana kutokana na uchezaji wake.
“Kwangu huu muziki wa amapiano naona kama una upotoshaji mkubwa kwa sababu ni aina ya muziki ambao mwanaume hawezi kucheza hadi ajilegezelegeze na kugeuza macho,” anasema Kalapina aliyevuma na albamu yake, Kufa Au Kupona (2005).

Kwa upande wake Damian Soul anasema ingawa amapiano ni ya Afrika Kusini ila bado Afrika ni moja na muziki hauna mipaka, hivyo yeyote mwenye uelewa na uwezo wa kufanya hamna tatizo lolote wala kosa.
“Amapiano ni muziki wa kitamaduni Afrika Kusini ukichanganyika na House Music, sisi hapa pia tunaweza kufanya japokuwa sio muziki wetu kwa maana ya Tanzania, lakini Kiafrika kama nina maarifa ya muziki kwanini nisifanye?” anasema.
Naye Nikki Mbishi anasema hata baadhi ya wasanii wa Hip Hop wamekimbilia katika amapiano baada ya kuacha kufanya muziki wa harakati za kuikomboa jamii kifra kutokana na kile anachodai ni kuzihofia mamlaka au nyimbo zao kufungiwa.
“Hivyo wasanii wenyewe wanaona bora tuwaimbie walevi tu, ndio wanaimba haya Amapiano, wanaimbia walevi, nyimbo za kulewea pombe,” anasema Nikki Mbishi aliyetoka na albamu yake, Sauti ya Jogoo (2011) chini ya M Lab (Music Laboratory). Ikumbukwe Nikki Mbishi aliyekuwa mshindi wa pili katika shindano la Kilimanjaro Emcee Shujaa 2008 na kuvuma na kibao chake, Play Boy (2010), tangu wakati huo ndiye msanii Bongo aliyetoa albamu nyingi ambazo ni saba akifuatiwa na Harmonize aliyetoa tano.