Wasanii kupima afya bure
Muktasari:
- Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Dk Peter Kisenge amesema, tukio hilo linaanza mwezi huu wa Desemba 2024 hadi Januari mwakani, kila wikiendi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika Kliniki ya JKCI Kawe iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari jijini.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), iliyoko Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, imetangaza huduma ya kupima moyo bure kwa wasanii wa filamu nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Dk Peter Kisenge amesema, tukio hilo linaanza mwezi huu wa Desemba 2024 hadi Januari mwakani, kila wikiendi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika Kliniki ya JKCI Kawe iliyopo Kawe jengo la Mkapa Health Plaza barabara ya Tuari jijini.
Kisege amesema, wameamua kutoa huduma hiyo kwa nia ya kuokoa wasanii wengi wanaopata maradhi ya moyo na kukosa matibabu ya haraka.
"Taasisi ya Moyo tumeamua kushirikiana na nyie wasanii wote ili kuweza kuwasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa, na tumeamua kufanya zoezi hili la kupima katika kliniki yetu ya Kawe kila Jumamosi na Jumapili ambapo tutatoa matibabu bure sababu afya ndio kitu cha msingi, hatutaki kusikia labda msanii ameanguka akiimba, au ameanguka akiwaaigiza sababu tukigundua," amesema Daktari huyo aliyeongeza;
"Na kwa kuwa wasanii ni kioo cha jamii, basi watatusaidia sana kuwaeleza wengine jinsi ya kujikinga na haya magonjwa yanayochangia vifo, duniani kote, magonjwa yasiyoambukiza yanaua watu karibia milioni 17 kwa hapa nchini , yanachangia asilimia 9 na serikali inatumia hela nyingi sana sababu watu wengi hawajui wana shinikizo la damu."
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, amezungumza kama Mwakilishi wa Wasanii na kuushukuru uongozi wa Muhimbili pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kujua umuhimu wa Wasanii wa Filamu na kuamua kuwashika Mikono katika natibabu ya maradhi ya moyo.
"Ni jambo jema Dokta Kisenge anaungana na wasanii, na amekuja kuiokoa kiwanda cha filamu chote bila kujali huyu msanii mchanga au mkongwe, hii kauli ya kusema kupima bure ni haina siasa bali ameangalia afya kwanza ambayo inayoleta amani katika taifa letu.
"Ametupa muelekeo wa tasnia ya maisha tunavyotakiwa kuishi, nasi watanzania tunapenda neno bure, hivyo niwaombe wasanii wenzangu tujitokeze kwa wingi tukapime leo hii kujigundua afya utaishi kwa umakini na tahadhari, kama hujapima kila kitu utakachokifanya utaona ni sahihi kwako kwani hujui afya yako" amesema Steve Nyerere.