Wasanii kuokoka watoa neno mashabiki hawawaelewi, wenyewe wafunguka

Muktasari:
- Wapo watu wengi wanaobadilika kiimani na kusahau walikotoka katika maisha ya anasa na starehe ingawa wengine wanadai kuokoka sio lazima iwe kwa mwonekano bali ni kile unachoamini na Mungu ndiye anayejua na sio watu.
INAFAHAMIKA neno ‘Kuokoka’ ni kurudisha imani katiika dini na kuachana na mambo mengi ya kidunia ambayo hayaleti picha nzuri katika jamii.
Wapo watu wengi wanaobadilika kiimani na kusahau walikotoka katika maisha ya anasa na starehe ingawa wengine wanadai kuokoka sio lazima iwe kwa mwonekano bali ni kile unachoamini na Mungu ndiye anayejua na sio watu.
Mwanaspoti limezungumza na baadhi ya wasanii ambao inadaiwa waliokoka lakini wengi wanaona bado mambo yao ni yale yale wakiona wako tofauti na maana ya ‘Kuokoka’.
Hata hivyo, wenyewe wanafunguka juu ya wanayosemwa na watu hasa mitandaoni pale wanapoona posti zao wakiwa katika mavazi yao au sehemu za starehe na kuwasema vibaya hawajaokoka na wako na maisha yale yale waliyoyazoea.
Irene Uwoya
Msanii wa Bongo Movies ambaye alitangaza kuokoka mwaka 2024. Licha ya kutangaza huko, wengi wamekuwa wakimshangaa kwa kudai matendo yake ya zamani hajabadilika, kama mavazi, kujiremba, kwenda sehemu za starehe na kuigiza tamthilia hasa vipande vinavyohusu mapenzi ambavyo havistahili.
Hata hivyo, mwenyewe anafunguka;
“Mimi hili nilijua tu. Kabla hata sijaingia kwenye kuokoka, nilijua yatasemwa mengi na wapo watakaonibeza na kunijaji nilivyo baada ya kutangaza kuokoa. Hivyo niwaambie tu kitu kimoja, watu wenye imani potofu na mimi acha waendelee hivyo, siwezi walazimisha.
“Mimi ninachojua nimeokoka na kuwa mtumishi wa Mungu. Hizo habari za kudai sijabadilika wamuachie Mungu kwanza. Hadi kufikia hapa nimejitahidi sana. Kuna baadhi ya matendo yangu yamebadilika na kumrudia Mungu zaidi Kwa kufanya matendo yaliyo mema.”
Elizabeth Michael ‘Lulu’
Msanii wa Bongo Movies aliyetangaza kuokoka mwaka 2016. Naye amekuwa asiyeaminika kama ameokoka kutokana na mavazi yake na baadhi ya starehe anazofanya. Mwenyewe anasema;
“Eee, mwenzangu mimi sijaanza kusemwa leo, kuokoka kwangu hakuendani na matendo yangu. Yaani watu wamesema weeee, wakanyamaza na sasa wameibuka tena kusema. Mie namshukuru tu Mungu kwa hili na sijutii kuokoka kwangu na hata wakisema vyovyote mimi sijali, ilimradi namwomba Mungu na mambo yangu yanaenda vizuri tu wao waache waendelee kuangalia matendo.”
Mainda Suka
Msanii mkongwe wa filamu na maigizo ambaye aliokoka tangu mwaka 2013. Ameingia kwenye madai ya kutobadilika matendo, akipenda kucheza muziki hasa wa Singeli na kukata mauno akiwa kwenye mkusanyiko wa watu, starehe za hapa na pale ila mwenyewe anasema;
“Mimi nimempokea Yesu kitambo sana na watu kusema ni kawaida yao ilimradi mimi najua nimeokoka na kufuata taratibu zote za dini yangu. Unajua mwanzoni nilipotangaza kuokoka, watu walikuwa wanaona kama namtania Mungu, ila nimeokoka kikwelikweli. Baadhi ya watu wanashindwa kuniamini kwa sababu hupenda kujichanganya sana kwenye mikusanyiko ya watu wa kila aina. Kuokoka siyo ukae tu kama kisiki jamani khaa, mavazi yangu na furaha sehemu nilipo haviwezi kunivua wokovu wangu.”
Hemed PHD
Msanii maarufu wa filamu aliyetangaza kuokoka mwaka 2018. Kutokana na matendo yake, anaonekana hajaokoka kwani anapenda starehe. Hata hivyo, anasema;
“Tatizo la watu wanataka ukisema umeokoa basi uwe mchafu, ukae tu nyumbani uimbe nyimbo za injili au usome tu Quran. Jamani imani ya mtu akijikubali inatosha, kwanza wapo ambao ukiokoka halafu ujiweke wa ovyo usionekana kwenye matukio hao hao wataanza kukusema, ila niseme tu mimi nimeamua kuokoka na kubadilika kitabia wanaoona sijabadilika basi hao wachawi tu.”
Kajala
Ni mwigizaji wa Bongo Movie. Alitangaza ameokoka na kuamua kumrudia Mungu tangu mwaka 2018. Hata hivyo, wengi hawaamini kama ameokoka kutokana na bado anaonekana kufanya starehe, kuvaa mavazi yenye ushawishi na hapa anasema;
“Bana weee, Binadamu sio wa kuwaendekeza, hawajaanza kutoamini leo wala jana kama nimeokoka kutokana na baadhi ya mavazi yangu wakati mwingine au ninaposhiriki kwenye starehe, jamani wokovu sio kujitia unyonge muda wote, mie nimeokoka najitambua watu waache kuhukumu.”
Blandina Chagula ‘Johari’
Mwigizaji wa Bongo Movie. Alitangaza kuokoka tangu mwaka 2018 na kusema ameamua kubadili mfumo wa maisha yake na kuishi maisha mapya, naye anasema haya :
“Yes wapo baadhi ya watu, wanakataaga na kushindwa kuamini kama mimi nimeokoka kutokana na wanavyoniona sipo kama wale walokole waliowazoea. Johari mimi nimeachana na mambo mengine sana ya ajabu niliyokuwa nafanya huko nyuma. Sasa hao wanaotokea kusema siendani na matendo mimi nachojua moyoni mwangu nimeokoka nafanya mambo mema ya kumpendeza Mungu na siwezi kujibweteka ulokole sio lazima uwe hivyo “.
Wapo pia wasanii walioamua kumrudia Mungu ‘kuokoka’ na bado wameendelea kushikilia misimamo yao na hawajabadilika tangu wameingia huko.
Mwanamuziki Hafsa Kazinja, ambaye aliamua kuokoka tangu mwaka 2015 na sasa hivi anaimba nyimbo za injili.
Pia aliyewahi kuwa msanii Suma Lee aliyetamba na wimbo wake wa “Hakunaga” pia alitangaza kuachana na muziki mwaka 2015 na kuamua kumrudia Mungu, pamoja na Msanii Snura Mushi mwaka jana, 2024, alitangaza kumrudia Mungu.